Ruka hadi kwenye maudhui
Hadithi zenye maelezo

Uislamu

Hadithi 22

Hakika wewe utaiendea jamii ya watu wa kitabu (Mayahudi na Wakristo), utakapowajia basi waite kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لِمُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ، حِينَ بَعَثَهُ إِلَى الْيَمَنِ: «إِنَّكَ سَتَأْتِي قَوْمًا أَهْلَ كِتَابٍ، فَإِذَا جِئْتَهُمْ فَادْعُهُمْ إِلَى أَنْ يَشْهَدُوا أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللهِ، فَإِنْ هُمْ أَطَاعُوا لَكَ بِذَلِكَ، فَأَخْبِرْهُمْ أَنَّ اللهَ قَدْ فَرَضَ عَلَيْهِمْ خَمْسَ صَلَوَاتٍ فِي كُلِّ يَوْمٍ وَلَيْلَةٍ، فَإِنْ هُمْ أَطَاعُوا لَكَ بِذَلِكَ، فَأَخْبِرْهُمْ أَنَّ اللهَ قَدْ فَرَضَ عَلَيْهِمْ صَدَقَةً تُؤْخَذُ مِنْ أَغْنِيَائِهِمْ فَتُرَدُّ عَلَى فُقَرَائِهِمْ، فَإِنْ هُمْ أَطَاعُوا لَكَ بِذَلِكَ، فَإِيَّاكَ وَكَرَائِمَ أَمْوَالِهِمْ، وَاتَّقِ دَعْوَةَ الْمَظْلُومِ، فَإِنَّهُ لَيْسَ بَيْنَهُ وَبَيْنَ اللهِ حِجَابٌ».
Imepokelewa Kutoka kwa bin Abbasi -Radhi za Allah ziwe juu yao- Amesema: Alisema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kumwambia Muadhi Ibn Jabal, alipomtuma kwenda Yemen: "Hakika wewe utaiendea jamii ya watu wa kitabu (Mayahudi na Wakristo), utakapowajia basi waite kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Ikiwa watakutii kwa hilo, basi waeleze kuwa Mwenyezi Mungu amewalazimisha juu yao swala tano katika kila usiku na mchana, ikiwa watakutii kwa hilo, basi waeleze kuwa Mwenyezi Mungu amewalazimisha juu yao zaka, huchukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kurudishwa kwa mafukara wao, ikiwa watakutii kwa hilo, basi jiepushe na mali zao za thamani, na ogopa maombi ya mwenye kudhulumiwa, kwani maombi hayo hayana baina yake na Mwenyezi Mungu kizuizi".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Alipomtuma Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- Muadhi Ibn Jabal -Radhi za Allah ziwe juu yake- kwenda katika miji ya Yemen kama mlinganizi wa kuwaita watu kwa Mwenyezi Mungu na kama mwalimu, alimuweka wazi kuwa atakumbana na jamii ya Wakristo; ili awe na maandalizi, kisha aanze katika kuwaita kwake na mambo muhimu zaidi kisha yanayofuatia, Atawaita kurekebisha itikadi kwanza; washuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu; Kwa sababu wao kwa itikadi hiyo yakuwa hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake; wataingia katika Uislamu, ikiwa watatii hilo basi awaamrishe wasimamishe swala; kwani huo ndio wajibu mkubwa baada ya tauhidi, Watakapoisimamisha awaamrishe matajiri wao kutoa zaka ya mali zao kuwapa mafukara wao, kisha akamtahadharisha na kuchukua mali bora; kwa sababu ya wajibu ni mali ya kati na kati, Kisha akamuusia aiepuke dhulma; asijekumuombewa dua mbaya aliyemdhulumu, kwani dua yake hupokelewa.

Mafunzo
  1. Maana ya kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, ni kumfanya Allah kuwa wa pekee kwa ibada, na kuacha kuabudu visivyokuwa Yeye.
  2. Maana ya kushuhudia kuwa Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu; Ni kumuamini yeye na yale aliyokuja nayo na kumsadikisha, nakuwa yeye ni wa mwisho katika Wajumbe wa Mwenyezi Mungu kuja kwa wanadamu.
  3. Nikuwa kujadiliana na msomi mwenye hoja tata si sawa na kujadiliana na mjinga; Ndio maana alimtanabahisha Muadhi kwa kumwambia: "Hakika wewe unakwenda katika jamii ya watu wa kitabu".
  4. Kuna umuhimu wa muislamu kuwa na uelewa katika dini yake; ili asalimike na upotovu wa wenye kumtia utata, na hii inakuwa kwa kutafuta elimu.
  5. Ubatili wa dini ya Mayahudi na Wakristo baada ya kutumwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, nakuwa wao si miongoni mwa watakao okoka siku ya Kiyama mpaka waingie katika dini Uislamu, na wamuamini Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-.
Marejeo

صحيح البخاري (2/ 119) (1458)، (2/ 128) (1496)، (9/ 114) (7372). صحيح مسلم (1/ 50) (19). فتح الباري لابن حجر (13/ 349). الملخص في شرح كتاب التوحيد، لصالح فوزان (ص54). الجديد في شرح كتاب التوحيد، لمحمد القرعاوي (ص64).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Kafaulu ikiwa atakuwa mkweli

عَنْ طَلْحَةَ بْنِ عُبَيْدِ اللهِ رضي الله عنه قَالَ: جَاءَ رَجُلٌ إِلَى رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مِنْ أَهْلِ نَجْدٍ ثَائِرُ الرَّأْسِ، نَسْمَعُ دَوِيَّ صَوْتِهِ، وَلَا نَفْقَهُ مَا يَقُولُ حَتَّى دَنَا مِنْ رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَإِذَا هُوَ يَسْأَلُ عَنِ الْإِسْلَامِ، فَقَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «خَمْسُ صَلَوَاتٍ فِي الْيَوْمِ وَاللَّيْلَةِ» فَقَالَ: هَلْ عَلَيَّ غَيْرُهُنَّ؟ قَالَ: «لَا، إِلَّا أَنْ تَطَّوَّعَ، وَصِيَامُ شَهْرِ رَمَضَانَ»، فَقَالَ: هَلْ عَلَيَّ غَيْرُهُ؟ فَقَالَ: «لَا، إِلَّا أَنْ تَطَّوَّعَ»، وَذَكَرَ لَهُ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الزَّكَاةَ، فَقَالَ: هَلْ عَلَيَّ غَيْرُهَا؟ قَالَ: «لَا، إِلَّا أَنْ تَطَّوَّعَ»، قَالَ: فَأَدْبَرَ الرَّجُلُ، وَهُوَ يَقُولُ: وَاللهِ، لَا أَزِيدُ عَلَى هَذَا، وَلَا أَنْقُصُ مِنْهُ، فَقَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «أَفْلَحَ إِنْ صَدَقَ».
Kutoka kwa Twalha bin Ubeidi LLah -Radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Alikuja mtu mmoja kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kutoka maeneo ya Najid, kichwa chake kikiwa kimetimka, tunasikia mvumo wa sauti yake, na wala hatuelewi anasema nini, mpaka akasogea karibu na Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- ghafla akaanza kuuliza kuhusu Uislamu, akasema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- "Swala tano mchana na usiku" Akasema: Je kuna la wajibu juu yangu zaidi ya hayo? Akasema: "Hapana ila kama utajitolea" Akasema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- "Na kufunga mwezi wa ramadhani" Akasema: Je kuna la wajibu juu yangu zaidi ya hilo? Akasema: "Hapana ila kama utajitolea" Akasema na akamtajia Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- zaka, akasema: Je kuna la wajibu juu yangu zaidi ya hilo? Akasema: "Hapana ila kama utajitolea" Akageuka na kuondoka yule bwana huku akisema: Wallahi sitozidisha juu ya hayo wala sitopunguza, Akasema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- "Kafaulu ikiwa atakuwa mkweli".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Mtu mmoja miongoni mwa watu wa Najdi alikuja kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake na nywele zake zikiwa zimetimkatimka na sauti yake ikiwa juu, wala haeleweki anasema nini, mpaka alipomkaribia Mtume rehema na amani ziwe juu yake akauliza kuhusu faradhi za Uislamu? Basi Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, akaanza na swala, na akamwambia kuwa Mwenyezi Mungu amemfaradhishia kuswali swala tano katika kila mchana na usiku. Akasema: Je, ninalazimika kuswali swala zingine zaidi ya hizi tano? Akasema: Hapana, labda kama utajitolea kuswali swala za sunna. Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Na miongoni mwa ibada alizokuwajibishia Mwenyezi Mungu juu yako ni kufunga mwezi wa Ramadhani. Yule bwana akasema: Je, ninalazimika kufunga funga zingine zaidi ya swaumu ya Ramadhani? Akasema: Hapana, ila kama utajitolea kufunga. Kisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake akamtajia Zaka Yule bwana akasema: Je, ninalazimika chochote katika sadaka baada ya zaka ya faradhi? Akasema: Hapana, ila kama utajitolea. Baada ya mtu huyo kusikia faradhi hizo kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake aligeuka na kuapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa atashikamana nazo bila ya kuongeza wala kupunguza, akasema rehema na amani zimshukie baada ya kauli yake hiyo: Ikiwa bwana huyu atakuwa mkweli kwa alichoapia, basi atakuwa miongoni mwa waliofaulu.

Mafunzo
  1. Upole wa sheria ya Kiislamu na urahisi wake kwa wanaoitekeleza.
  2. Muamala wake mzuri rehema na amani ziwe juu yake kwa mtu huyu, kwani alimpa nafasi ya kumsogelea na kumuuliza maswali.
  3. Kuanza na mambo muhimu zaidi kisha yanayofuata kwa umuhimu wakati wa kuwalingania watu kwa Mwenyezi Mungu.
  4. Uislamu ni itikadi na matendo, matendo hayawezi kufaa bila imani, wala imani haiwezi kufaa bila matendo.
  5. Umuhimu wa matendo haya nakuwa matendo haya ni miongoni mwa nguzo za imani.
  6. Swala ya Ijumaa imejumuishwa katika sala tano za faradhi; Kwa sababu ni badala ya swala ya adhuhuri siku ya Ijumaa kwa wale ambao ni wajibu kwao.
  7. Mtume, rehema na amani ziwe juu yake alianza mafundisho yake kwa kutilia mkazo faradhi za Uislamu, ambazo ni nguzo zake baada ya Shahada mbili. Kwa sababu muulizaji alikuwa Muislamu, na hakutaja Hija kwa sababu tukio hili lilikuwa kabla ya kufaradhishwa kwake, au kwa sababu wakati wake ulikuwa haujafika.
  8. Ikiwa mtu atajiwekea mipaka katika yale yaliyo wajibu kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, atafaulu, lakini hii haimaanishi kuwa si Sunna kufanya hivyo kwa hiari; Kwa sababu sala za hiari hukamilisha sala za faradhi Siku ya Kiyama.
Marejeo

صحيح البخاري (1/ 18) (46). صحيح مسلم (1/ 40) (11). كنوز رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين. بهجة الناظرين، لسليم الهلالي (2/ 346). نزهة المتقين، لمجموعة من الباحثين (2/ 857). شرح رياض الصالحين، لابن عثيمين (5/ 242).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka washuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe swala, na watoe zaka

عَنِ ابْنِ عُمَرَ رضي الله عنهما أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: «أُمِرْتُ أَنْ أُقَاتِلَ النَّاسَ حَتَّى يَشْهَدُوا أَنْ لاَ إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ، وَيُقِيمُوا الصَّلاَةَ، وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ، فَإِذَا فَعَلُوا ذَلِكَ عَصَمُوا مِنِّي دِمَاءَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ إِلَّا بِحَقِّ الإِسْلاَمِ، وَحِسَابُهُمْ عَلَى اللَّهِ».
Na imepokewa kutoka kwa bin Omari -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake yeye na baba yake -kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na Amani ziwe juu yake - amesema: "Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka washuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe swala, na watoe zaka, pindi watakapofanya hivyo watakuwa wamezikinga kutokana nami damu zao na mali zao isipokuwa kwa haki ya uislamu na hesabu yao itakuwa juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Anaeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa Mwenyezi Mungu alimuamrisha kupigana na washirikina mpaka washuhudie kuwa hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake asiye na mshirika, na wamshuhudilie Muhammadi rehema na amani ziwe juu yake utume, na kuyafanyia kazi makusudio ya shahada hii, ikiwemo kuhifadhi swala tano usiku na mchana, na wawape zaka za faradhi wastahiki wake. Wakifanya mambo haya basi Uislamu utakinga damu zao na mali zao, haitokuwa halali kuwaua isipokuwa watakapofanya uhalifu au kosa la jinai watakalostahiki kwalo kuuawa kwa mujibu wa hukumu za Uislamu, kisha siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atasimamia hesabu yao kwani yeye ndiye ajuaye siri zao.

Mafunzo
  1. Hukumu zote huenda kulingana na kile kichodhihiri, na Allah ndiye msimamizi wa siri.
  2. Umuhimu wa kufikisha ujumbe wa tauhidi nakuwa ndio ujumbe wa kwanza katika ufikishaji.
  3. Hadithi hii haimaanishi kuwalazimisha washirikina kuingia katika Uislamu, bali wamepewa uhuru wa kuchagua kati ya kuingia katika Uislamu au kutoa Jizia (Kodi); ikiwa watakataa na wakataka kuzuia ujumbe wa Uislamu, kukawa hakuna namna nyingine zaidi ya kuwapiga vita kwa mujibu wa hukumu za kiislamu.
Marejeo

صحيح البخاري (1/ 14) (25). صحيح مسلم (1/ 53) (22). التحفة الربانية في شرح الأربعين حديثًا النووية، لإسماعيل السعدي (ص23). شرح الأربعين النووية، لابن عثيمين (ص125).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

"Umeniuliza kuhusu jambo kubwa, lakini nijepesi kwa yule atakayefanyiwa wepesi na Mwenyezi Mungu Mtukufu

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ رضي الله عنه قَالَ: كُنْتُ مَعَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي سَفَرٍ، فَأَصْبَحْتُ يَوْمًا قَرِيبًا مِنْهُ وَنَحْنُ نَسِيرُ، فَقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللهِ أَخْبِرْنِي بِعَمَلٍ يُدْخِلُنِي الجَنَّةَ وَيُبَاعِدُنِي عَنِ النَّارِ، قَالَ: «لَقَدْ سَأَلْتَنِي عَنْ عَظِيمٍ، وَإِنَّهُ لَيَسِيرٌ عَلَى مَنْ يَسَّرَهُ اللَّهُ عَلَيْهِ، تَعْبُدُ اللَّهَ وَلاَ تُشْرِكْ بِهِ شَيْئًا، وَتُقِيمُ الصَّلاَةَ، وَتُؤْتِي الزَّكَاةَ، وَتَصُومُ رَمَضَانَ، وَتَحُجُّ البَيْتَ» ثُمَّ قَالَ: «أَلاَ أَدُلُّكَ عَلَى أَبْوَابِ الخَيْرِ: الصَّوْمُ جُنَّةٌ، وَالصَّدَقَةُ تُطْفِئُ الخَطِيئَةَ كَمَا يُطْفِئُ الْمَاءُ النَّارَ، وَصَلاَةُ الرَّجُلِ مِنْ جَوْفِ اللَّيْلِ» قَالَ: ثُمَّ تَلاَ: «{تَتَجَافَى جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ}، حَتَّى بَلَغَ {يَعْمَلُونَ}» ثُمَّ قَالَ: «أَلاَ أُخْبِرُكَ بِرَأْسِ الأَمْرِ كُلِّهِ وَعَمُودِهِ، وَذِرْوَةِ سَنَامِهِ؟» قُلْتُ: بَلَى يَا رَسُولَ اللهِ، قَالَ: «رَأْسُ الأَمْرِ الإِسْلاَمُ، وَعَمُودُهُ الصَّلاَةُ، وَذِرْوَةُ سَنَامِهِ الجِهَادُ» ثُمَّ قَالَ: «أَلاَ أُخْبِرُكَ بِمَلاَكِ ذَلِكَ كُلِّهِ؟» قُلْتُ: بَلَى يَا نَبِيَّ اللهِ، فَأَخَذَ بِلِسَانِهِ قَالَ: «كُفَّ عَلَيْكَ هَذَا» فَقُلْتُ: يَا نَبِيَّ اللهِ، وَإِنَّا لَمُؤَاخَذُونَ بِمَا نَتَكَلَّمُ بِهِ؟ فَقَالَ: «ثَكِلَتْكَ أُمُّكَ يَا مُعَاذُ، وَهَلْ يَكُبُّ النَّاسَ فِي النَّارِ عَلَى وُجُوهِهِمْ أَوْ عَلَى مَنَاخِرِهِمْ إِلاَّ حَصَائِدُ أَلْسِنَتِهِمْ».
Kutoka kwa Muadhi bin Jabali -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Tulikuwa pamoja na Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika safari, nikajikuta siku moja niko karibu naye tukiwa tunatembea, nikasema: Ewe Mtume wa Allah nieleze ibada ambayo nikiifanya itaniingiza peponi, na itaniweka mbali na moto, akamjibu: "Umeniuliza kuhusu jambo kubwa, lakini nijepesi kwa yule atakayefanyiwa wepesi na Mwenyezi Mungu Mtukufu: ni kumuabudu Mwenyezi Mungu bila kumshirikisha na chochote, na kusimamisha swala, na kutoa zaka, na kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kuhiji. kisha akasema Mtume: Je, nikujulishe milango ya kheri? Funga ni kinga, na sadaka inaondosha madhambi kama maji yanavyo uzima moto, na swala ya mtu katikati ya usiku, kisha akasoma kauli ya Mwenyezi Mungu: "Mbavu zao zinaachana na vitanda..." mpaka alipo fikia mwisho wa aya "wanao jua". Kisha akasema Mtume: Je nikueleze kichwa cha mambo yote na nguzo yake na kilele chake? nikajibu ndio ewe mjumbe wa Allah, akasema: Kichwa cha mambo yote ni Uislam, na nguzo yake ni Swala, na kilele chake ni Jihadi. kisha akasema: Je nikujulishe kinacho yahifadhi na kuyatunza matendo hayo? nikasema ndio ewe Mtume wa Allah, akaushika ulimi wake kisha akasema: uzuwie ulimi wako, nikamuuliza: Ewe Mtume wa Allah je tutahesabiwa kwa kila tunacho kizungumza? Akasema: akukose mamako, hakuna kitakacho waingiza watu wengi motoni kama chumo za ndimi zao".
Imepokelewa na Tirmidhiy, Ibn Majah na AhmadDarajaSahihi kwa mkusanyiko wa njia zake
Maelezo

Amesema Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake: Tulikuwa pamoja na Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika safari, siku moja nikawa karibu naye tukiwa tunatembea, nikasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nieleze amali itakayoniingiza Peponi na kuniweka mbali na moto, akasema: Bila shaka umeuliza kuhusu jambo kubwa kulifanya kwake katika nafsi, na bila shaka ni jepesi na ni rahisi mno kwa atakayerahisishiwa na Mwenyezi Mungu kulifanya; tekeleza faradhi za Uislamu; Ya kwanza: Umuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na wala usimshirikishe na chochote. Ya pili: Usimamishe swala tano za faradhi mchana na usiku: Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Ishaa, kwa sharti zake na nguzo zake na wajibu wake. Ya tatu: Utoe zaka ya wajibu, nayo ni ibada ya mali ya wajibu kwa kila mali iliyofikia kiwango katika sheria, na wanapewa wastahiki wake. Ya nne: Ufunge mwezi wa Ramadhani, nako ni kujizuia na kula na kunywa na mengineyo katika mambo yenye kufunguza kwa nia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu, kuanzia kuchomoza kwa Alfajiri mpaka kuzama kwa Jua. Ya tano: Utaizuru nyumba kwa kwenda Makka ili kutimiza ibada, kwa lengo la kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kisha akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Je nikufahamishe kuhusu njia inayokufikisha katika milango ya heri? Nayo ni kwa kutekeleza faradhi na sunna hizo: Ya kwanza: Ni funga ya hiyari, nayo inamzuia mtu kuingia katika maasi, nayo ni kwa kuvunjavunja matamanio, na kuzidhoofisha nguvu. Ya pili: Sadaka ya kujitolea inazima madhambi baada ya kuyafanya na huyaondosha na kufuta athari zake. Ya tatu: Swala ya tahajudi katika theluthi ya mwisho ya usiku, kisha akasoma rehema na amani ziwe juu yake kauli yake Mtukufu: "Hunyanyuka mbavu zao" Yaani: Hujiweka mbali, na "malazi" Yaani: Mahali pa kulala, "wakimuomba Mola wao Mlezi" Yaani: kwa swala na dhikri na kusoma Qur'ani na dua, "kwa hofu na tamaa, na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa, hakuna nafsi ijuayo yale waliyofichiwa, katika yale yenye kutuliza macho" Yaani: Yale yenye kutuliza macho yao siku ya Kiyama na katika pepo miongoni mwa neema, "ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyafanya". Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hivi nikueleze msingi wa dini? na nguzo yake inayosimamia? na kiini cha kilele chake? Akasema Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake: Ndio, nieleze ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Kichwa cha mambo yote ni: Uislamu nao ni shahada mbili, na kwa shahada hizi mbili ndio mtu anapata msingi wa dini. Na nguzo yake: Ni swala, hakuna Uislamu bila swala, kama ambavyo nyumba haiwezi kusimama pasina nguzo, atakaye swali dini yake itakuwa na nguvu na itanyanyuka; Na kiini cha kilele chake na kimo chake ni Jihadi na kutoa juhudi katika kupambana na maadui wa dini ili kulinyanyua neno la Mwenyezi Mungu. Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hivi nikuelezeni umadhubuti na ufanisi wa yaliyopita? Mtume rehema na amani ziwe juu yake akashika ulimi, na akasema: Zuia huu na wala usizungumze yale yasiyokuhusu. Akasema Muadhi: Je atatuchukulia makosa na kutuhesabu Mola wetu Mlezi na kutuadhibu kwa kila tunachozungumza?! Akasema rehema na amani ziwe juu yake: Amekupoteza mama yako! Na makusudio yake si kumuombea dua mbaya, bali ni katika maneno ya waarabu yaliyokuwa yakitumika kumtanabahisha mtu kuwa jambo hili unatakiwa kulichukulia tahadhari kubwa na kulielewa, kisha akasema; na unadhani ni kipi kitawatupa watu na kuwadondosha kwa nyuso zao ndani ya moto zaidi ya chumo za ndimi zao, ikiwemo ukafiri na kumzulia mtu machafu na matusi na utesi na usengenyaji, na uongo na mfano wa hayo.

Mafunzo
  1. Pupa ya Maswahaba radhi za Allah ziwe juu yao ya kutaka kujifunza, na ndio maana maswali yao yalikuwa ni mengi sana kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake.
  2. Utambuzi wa Maswahaba radhi za Allah ziwe juu yao kwa kujua kwao kuwa matendo ni sababu ya kuingia Peponi.
  3. Swali lililotoka kwa Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake ni swali zito; kwa sababu kwa uhalisia ndio siri ya uhai na uwepo wa kila kitu, kila kilichopo katika dunia kwanzia wanadam au majini lengo lake la mwisho ima iwe Pepo, ama motoni, na ndio maana swali hili likawa zito.
  4. Kuingia kwake peponi kumefungamanishwa na kuzitekeleza nguzo tano za Uislamu, nazo ni: Shahada mbili na swala na zaka na swaumu na Hija.
  5. Kichwa cha dini na jukumu ghali na wajibu mkubwa ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kwa kumuabudu yeye peke yake asiye na mshirika.
  6. Huruma ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwa kuwafungulia milango ya kheri ili wajiongezee sababu za malipo na kusamehewa madhambi.
  7. Fadhila za kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa ibada za sunna baada ya kutekeleza faradhi.
  8. Swala katika Uislamu ni sawa na nguzo linayosimamia hema, Uislamu unaondoka kwa kudondoka kwake, kama linavyodondoka hema kwa kudondoka kwa nguzo.
  9. Ulazima wa kuhifadhi ulimi kwa yale yanayomdhuru mtu katika dini yake.
  10. Kuuzuia ulimi na kuudhibiti na kuufunga ndio msingi wa kheri zote.
Marejeo

سنن الترمذي (4/ 362) (2616). سنن ابن ماجه (5/ 116) (3973). مسند أحمد (36/ 344) (22016). التحفة الربانية، لإسماعيل الأنصاري (ص67). شرح الأربعين النووية، للعثيمين (ص291). الأحاديث الأربعين النووية مع ما زاد عليها ابن رجب وعليها الشرح الموجز المفيد، لعبد الله بن صالح المحسن (ص57).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Usimuue, kwani ukimuuua basi yeye atakuwa katika nafasi yako kabla hujamuua, na wewe utakuwa katika nafasi yake kabla hajasema neno lake alilolisema

عَنْ المِقْدَادِ بْنَ عَمْرٍو الكِنْدِيَّ رضي الله عنه: أَنَّهُ قَالَ لِرَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أَرَأَيْتَ إِنْ لَقِيتُ رَجُلًا مِنَ الكُفَّارِ فَاقْتَتَلْنَا، فَضَرَبَ إِحْدَى يَدَيَّ بِالسَّيْفِ فَقَطَعَهَا، ثُمَّ لاَذَ مِنِّي بِشَجَرَةٍ، فَقَالَ: أَسْلَمْتُ لِلَّهِ، أَأَقْتُلُهُ يَا رَسُولَ اللَّهِ بَعْدَ أَنْ قَالَهَا؟ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «لاَ تَقْتُلْهُ» فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّهُ قَطَعَ إِحْدَى يَدَيَّ، ثُمَّ قَالَ ذَلِكَ بَعْدَ مَا قَطَعَهَا؟ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «لاَ تَقْتُلْهُ، فَإِنْ قَتَلْتَهُ فَإِنَّهُ بِمَنْزِلَتِكَ قَبْلَ أَنْ تَقْتُلَهُ، وَإِنَّكَ بِمَنْزِلَتِهِ قَبْلَ أَنْ يَقُولَ كَلِمَتَهُ الَّتِي قَالَ».
Kutoka kwa Mikidadi bin Amri Al-Kindi radhi za Allah ziwe juu yake: Ya kwamba yeye alisema kumuuliza Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- Unaonaje ikiwa nitakutana na mtu miongoni mwa makafiri, tukapigana, akapiga moja ya mikono yangu kwa upanga akaukata, kisha akajificha katika mti, akasema: Nimejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, je nimuue ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu baada ya kuwa amelisema neno hilo? Akasema: "Usimuue" Nikasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kakata moja ya mikono yangu, Kisha akasema hivyo baada ya kuwa kaukata?! Akasema: "Usimuue, kwani ukimuuua basi yeye atakuwa katika nafasi yako kabla hujamuua, na wewe utakuwa katika nafasi yake kabla hajasema neno lake alilolisema".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Mikidadi bin Aswadi radhi za Allah ziwe juu yake alimuuliza Mtume rehema na amani ziwe juu yake pindi atakapokutana na mtu miongoni mwa makafiri katika mapambano, wakapambana kwa mapanga, mpaka yule kafiri akakata mmoja kati ya mikono yake kwa upanga, kisha kafiri akamkimbia na akajikinga katika mti, akasema: Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, je, ni halali kwangu kumuua baada yakuwa amekata mkono wangu? Mtume rehema na amani ziwe juu yake akamwambia: Hapana, usimuuwe. Akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, lakini yeye kakata moja ya mikono yangu, pamoja na hivyo bado tu nisimuuwe?! Akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Hapana, usimuuwe, kwa sababu tayari damu yake ishakuwa haramu, kwa sababu ikiwa utamuua baada ya kusilimu kwake; basi hakika yeye atakuwa katika nafasi yako ya kulindwa damu kwa Uislamu wake, na wewe utakuwa katika nafasi yake, itakuwa halali damu yako kwa kukuua kwa kisasi kwa sababu ya kumuuwa.

Mafunzo
  1. Yatakayejitokeza kwake yanayoonyesha kuingia katika Uislamu kama kauli au kitendo, ni haramu kumuua.
  2. Atakaposilimu mmoja kati ya makafiri wakati wa vita, basi damu yake itakingwa, na ni lazima kutomuua, isipokuwa tukibaini kinyume na hilo.
  3. Ni lazima muislamu matamanio yake yafuate sheria na si mihemuko na kutaka kulipiza kisasi.
  4. Amesema bin Hajari: Inafaa kuuliza matatizo kabla hayajatokea, kwa kuzingatia kauli sahihi kuwa kisa hiki aliuliza kabla jambo halijatokea, ama yaliyopokelewa kutoka kwa baadhi ya wema waliotangulia kulichukia hilo, hilo linatafsirika kuwa hutokea mara chache sana, ama yanayowezekana kutokea kwa kawaida ni sheria kuyaulizia ili yafahamike.
Marejeo

صحيح البخاري (5/ 85) (4019). صحيح مسلم (1/ 95) (95). نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (1/ 359). بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (1/ 461). كنوز رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (6/ 345). المعجم الوسيط، (2/ 815).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao na kufanyiana kwao upole, ni kama mfano wa kiwiliwili, kinapopata tabu kiungo kimoja vinaitana kwa ajili ya hicho kimoja viungo vyote kwa kukesha na maumivu

عَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «مَثَلُ الْمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ وَتَعَاطُفِهِمْ مَثَلُ الْجَسَدِ، إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالسَّهَرِ وَالْحُمَّى».
kutoka kwa Nu'man Bin Bashiri -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na amani ziwe juu yake -: "Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao na kufanyiana kwao upole, ni kama mfano wa kiwiliwili, kinapopata tabu kiungo kimoja vinaitana kwa ajili ya hicho kimoja viungo vyote kwa kukesha na maumivu".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Anabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa inatakiwa kuwa hali ya waislamu baadhi yao kwa baadhi katika kupendeleana kheri na kuhurumiana na kusaidizana na kuteteana, na kuudhika kwa yale madhara yanayowafika, kama mfano wa kiwiliwili kimoja, kikiugua kiungo kimoja, mwili mzima unashiriki kwa kukesha na maumivu pia.

Mafunzo
  1. Ni lazima kuziheshimu haki za waislamu na kuhimiza kuwasaidia na kuhurumiana wao kwa wao.
  2. Ni lazima kwa watu wa imani kuwe na mapenzi na kuteteana.
Marejeo

صحيح البخاري (8/ 10) (6011). صحيح مسلم (4/ 1999) (2586). نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، مجموعة من الباحثين (1/ 246). بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (1/ 317). كنوز رياض الصالحين، مجموعة من الباحثين (4/ 405). تطريز رياض الصالحين، لفيصل آل مبارك (ص173). المعجم الوسيط (1/ 492).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Umejengwa uislamu kwa mambo matano

عَنْ عَبْدِ اللهِ بنِ عُمَر رضي الله عنهما قال: قال رسولُ الله صلى الله عليه وسلم: «بُنِيَ الْإِسْلَامُ عَلَى خَمْسٍ: شَهَادَةِ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ، وَأَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، وَإِقَامِ الصَّلَاةِ، وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ، وَحَجِّ الْبَيْتِ، وَصَوْمِ رَمَضَانَ».
kutoka kwa Abdullahi bin Amry -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Umejengwa uislamu kwa mambo matano: Kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammadi ni Mja wake na Mtume wake, na kusimamisha swala, na kutoa zaka, na kuhiji nyumba tukufu, na kufunga ramadhani".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Ameufananisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- Uislamu na jengo madhubuti kwa nguzo zake tano zenye kulibeba jengo hilo, na mambo mengine ya Uislamu kama nyenzo zenye kulikamilisha jengo hilo, Na nguzo ya kwanza katika nguzo hizo ni: Shahada mbili; Kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, hizo mbili ni nguzo moja; kila moja haitengani na nyingine, mja anazitamka kwa kukiri umoja wa Mwenyezi Mungu na kustahiki kwake kuabudiwa yeye pekee pasina mwingine, na kufanyia kazi makusudio ya nguzo hii, na kwa kuamini utume wa Muhammadi -Rehema na amani ziwe juu yake- kwa kumfuata yeye. Na nguzo ya pili: Ni kusimamisha swala, nazo ni swala tano za faradhi usiku na mchana: Alfajiri, Adhuhuri, lasiri, Maghribi, na Ishaa, kwa sharti zake na nguzo zake na wajibu wake. Na nguzo ya tatu: Ni kutoa zaka ya lazima, nayo ni ibada ya mali ya wajibu katika kila mali iliyofikia kiwango maalumu katika sheria, ambayo hupewa wastahiki wake. Na nguzo ya nne: Ni Hija, nayo nikutia nia ya kwenda Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada, kwa kumuabudu Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka. Na nguzo ya tano: Ni kufunga mwezi wa Ramadhani, nako ni kujizuia na kula na kunywa na vinginevyo miongoni mwa vyenye kufunguza kwa nia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu, kuanzia kuchomoza kwa Alfajiri mpaka kuzama jua.

Mafunzo
  1. Nguzo mbili zinakwenda sambamba, haikubaliki moja mpaka iwe na nyingine; ndio maana akazifanya kuwa nguzo moja.
  2. Shahada mbili ndio msingi wa Dini, haikubaliki kauli wala amali ila kwa shahada hizo.
Marejeo

صحيح البخاري (1/ 11) (8)، صحيح مسلم (1/ 45) (16)، و(1/ 88) (82)، فتح الباري لابن رجب (1/ 22)، جامع العلوم والحكم (1/147)، شرح الأربعين لابن العطّار (ص 62)، شرح الأربعين النووية لعبد الكريم الخضير (ص 87)، فتح القوي المتين في شرح الأربعين للعباد (ص 29)، شرح الأربعين النووية لصالح آل الشيخ (ص 91 - 95)، التحفة الربانية لإسماعيل الأنصاري (ص 12).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Yeyote atakayefanya wema katika Uislamu basi hatoadhibiwa kwa yale aliyoyatenda katika zama za ujinga, na yeyote atakaye tenda maovu akiwa katika Uislamu ataadhibiwa kwa makosa yake ya mwanzo na ya mwisho

عَنِ ابْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ، قَالَ: قَالَ رَجُلٌ: يَا رَسُولَ اللهِ، أَنُؤَاخَذُ بِمَا عَمِلْنَا فِي الْجَاهِلِيَّةِ؟ قَالَ: «مَنْ أَحْسَنَ فِي الْإِسْلَامِ لَمْ يُؤَاخَذْ بِمَا عَمِلَ فِي الْجَاهِلِيَّةِ، وَمَنْ أَسَاءَ فِي الْإِسْلَامِ أُخِذَ بِالْأَوَّلِ وَالْآخِرِ».
Imepokelewa hadithi kutoka kwa bin Masoud -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-, amesema: Alisema mtu mmoja: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hivi sisi tutaadhibiwa kwa tuliyoyafanya katika zama za ujinga kabla yakuwa waislamu?Akasema "Yeyote atakayefanya wema katika Uislamu basi hatoadhibiwa kwa yale aliyoyatenda katika zama za ujinga, na yeyote atakaye tenda maovu akiwa katika Uislamu ataadhibiwa kwa makosa yake ya mwanzo na ya mwisho".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Anatuwekea wazi Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- ubora wa kuingia katika Uislamu, Na kuwa mwenye kusilimu na uislamu wake ukawa mzuri na akawa mtakasifu na mkweli, basi hatoadhibiwa kwa makosa aliyoyafanya kabla ya uislamu, Na atakaye fanya uovu akiwa katika uislamu, yaani kwa kuwa mnafiki au akatoka katika dini yake, basi huyo ataadhibiwa kwa aliyoyafanya akiwa bado hajaingia katika uislamu na ataadhibiwa pia kwa yale aliyoyafanya akiwa katika uislamu.

Mafunzo
  1. Maswahaba -Radhi za Allah ziwe juu yao- kutilia umuhimu mambo mazito, na hofu yao kwa yale yaliyokuwa kabla ya Uislamu.
  2. Mahimizo ya kudumu kwenye Uislamu.
  3. Ubora na fadhila za kuingia katika uislamu, na kuingia katika uislamu hufuta matendo mabaya yaliyopita.
  4. Mwenye kutoka katika uislamu na mnafiki, atahukumiwa kwa kila kitendo alichokifanya kabla ya kusilimu kwake, na kuhukumiwa kwa dhambi alilofanya kwenye uislamu.
Marejeo

صحيح البخاري (9/ 14) (6921). صحيح مسلم (1/ 111) (120). مشارق الأنوار على صحاح الآثار (2/229). الكواكب الدراري (24/43). عمدة القاري شرح صحيح البخاري (24/ 76).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com
8 kati ya 22
Hadithi 22
  1. Hakika wewe utaiendea jamii ya watu wa kitabu (Mayahudi na Wakristo), utakapowajia basi waite kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu
  2. Kafaulu ikiwa atakuwa mkweli
  3. Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka washuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe swala, na watoe zaka
  4. "Umeniuliza kuhusu jambo kubwa, lakini nijepesi kwa yule atakayefanyiwa wepesi na Mwenyezi Mungu Mtukufu
  5. Usimuue, kwani ukimuuua basi yeye atakuwa katika nafasi yako kabla hujamuua, na wewe utakuwa katika nafasi yake kabla hajasema neno lake alilolisema
  6. Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao na kufanyiana kwao upole, ni kama mfano wa kiwiliwili, kinapopata tabu kiungo kimoja vinaitana kwa ajili ya hicho kimoja viungo vyote kwa kukesha na maumivu
  7. Umejengwa uislamu kwa mambo matano
  8. Yeyote atakayefanya wema katika Uislamu basi hatoadhibiwa kwa yale aliyoyatenda katika zama za ujinga, na yeyote atakaye tenda maovu akiwa katika Uislamu ataadhibiwa kwa makosa yake ya mwanzo na ya mwisho
  9. na hakika yeye hajawahi kusema hata siku moja: Ewe Mola wangu nisamehe makosa yangu siku ya Kiyama
  10. Shetani humjia mmoja wenu na akamwambia: Ni nani aliumba kitu fulani? Mpaka anafikia kusema ni nani alimuumba Mola wako? Basi ikiwa atafikia kuuliza hivyo basi na ajikinge kwa Mwenyezi Mungu na awache kuuliza maswali hayo
  11. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hamdhulumu muumini kwa jema alilofanya, huandikiwa thawabu za wema wake hapa Duniani na hulipwa thawabu hizo huko Akhera
  12. Umekwisha pokea malipo yako kutokana na mema uliyoyatanguliza
  13. Ametuhadithia Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- naye ni mkweli mwenye kukubaliwa: "Kwa hakika mmoja wenu hukusanywa umbile lake kwenye tumbo la mama yake mchana arobaini na nyusiku arobaini
  14. na mimi ndiye ninaitwa Dhwamam Bin Thaalaba ndugu wa Banii Saad Bin Bakri
  15. Mayahudi wameghadhibikiwa, na Wakristo ni wapotofu
  16. Sema: Laa ilaaha illa llahu, nitakutolea ushuhuda wa kusilimu kwa maneno hayo siku ya Kiyama
  17. Hakika haya unayoyasema na kuwalingania watu ni mambo mazuri, ikiwa utatwambia juu ya haya tuliyoyafanya kama yana kafara
  18. Atakayeswali swala yetu na akaelekea kibla chetu na akala kichinjwa chetu basi huyo ni Muislamu mwenye dhima ya Mwenyezi Mungu na dhima ya Mtume wake, msimfanyie hiana Mwenyezi Mungu katika dhima yake
  19. Mtu yeyote atakayesema kumwambia ndugu yake: Ewe kafiri, basi utampata mmoja katika ya hao wawili, ikiwa atakuwa kama alivyosema (litathibiti hilo), na kama si hivyo utarejea kwake
  20. Umejengwa uislamu kwa mambo matano
  21. Waonaje ikiwa nitaswali swala zilizofaradhishwa, na nikafunga Ramadhani, na nikahalalisha kilichokuwa halali na nikaharamisha kilichokuwa haramu
  22. Hakika umeniuliza kuhusu jambo kubwa, lakini nijepesi kwa yule atakayefanyiwa wepesi na Mwenyezi Mungu

Kila hadithi, daraja, maelezo na funzo hapa vinaonyeshwa kama HadeethEnc.com inavyovichapisha, kwa masharti yake ya kuchapisha upya. Daraja halimtaji aliyelitoa. Tafsiri na maelezo ni ya waandishi wake wenyewe, na baadhi hutaja hukumu; wahakiki wa Sabīl hawajavichunguza. Hadithi ya Kiarabu ndiyo matini. Chanzo: HadeethEnc.com