Imepokelewa kutoka kwa Anas -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe ju yake-: Yakuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu Kiyama, akasema: Lini Kiyama? Akasema: “Umetayarisha nini kwa ajili yake?” Akasema: Hapana, isipokuwa ninampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake rehema na amani ziwe juu yake. Akasema: “Wewe uko pamoja na unayempenda.” Anas akasema: Hakuna lililotufurahisha zaidi ya kauli ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake: “Wewe uko pamoja na unayempenda.” Anas akasema: Mimi ninampenda Mtume rehema na amani ziwe juu yake na Abubakari na Omari, na ninataraji kuwa pamoja nao kutokana na mapenzi yangu kwao, hata kama nisipofanya sawa na matendo yao.
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Bedui mmoja anayeishi jangwani alimuuliza Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Je, saa ya Kiyama itatokea wakati gani?
Basi rehema na amani ziwe juu yake akamwambia: Umeiandalia mambo gani mema?
Akasema muulizaji: Sikutayarisha jambo kubwa kwa ajili yake isipokuwa ninampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wala hakutaja ibada nyinginezo za moyo, za kimwili, au za kifedha. Kwa sababu zote ni matawi ya upendo unaotokana na hayo, na kwa sababu upendo wa dhati humsukuma mtu kujitahidi kufanya matendo mema.
Mtume rehema na amani ziwe juu yake akamwambia: Wewe utakuwa pamoja na unayempenda peponi.
Maswahaba wa Mtume rehema na amani ziwe juu yake wakafurahishwa sana na habari hii njema.
Kisha Anas radhi za Allah ziwe juu yake akaeleza kuwa hakika anampenda Mtume rehema na amani ziwe juu yake na Abubakari na Omari, na anatarajia kuwa pamoja nao, hata kama amali zake si kama amali zao.
Mafunzo
Hekima ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika kumjibu muulizaji, kwani alimuongoza katika yale yanayomhusu na kumuokoa, nayo ni: kujiandaa na Akhera kwa yenye manufaa na matendo mema.
Mwenyezi Mungu ameficha kwa waja wake elimu ya kujua Kiyama, ili mtu aendelee kuwa tayari na kujiandaa kukutana na Mwenyezi Mungu.
Fadhila za kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na watu wema miongoni mwa waumini, na onyo la kuwapenda washirikina.
Kauli yake rehema na amani ziwe juu yake: Wewe utakuwa pamoja na umpendaye. Kinachokusudiwa sio usawa wa daraja na hadhi, bali ni kuwa, wao watakuwa Peponi kiasi kwamba kila mmoja wao ataweza kumuona mwenzake, hata kama sehemu hiyo iko mbali.
Kumuelekeza Muislamu kuzingatia yale yaliyo bora na yenye manufaa kwake, na kuacha kuuliza juu ya yale ambayo hayamnufaishi.
Marejeo
صحيح البخاري (5/ 12) (3688).
صحيح مسلم (4/ 2032) (2639).
بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (1/ 435).
كنوز رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (6/ 177).
المعجم الأوسط، للطبراني (1/ 131).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (1/ 342).
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Hivi nikuhadithieni hadithi kuhusu Dajali ambayo hajawahi kuhadithia Nabii yeyote watu wake! Hakika yeye ni chongo, na hakika atakuja akiwa pamoja na mfano wa pepo na moto, anayoisema kuwa ni pepo huo ndio moto, na hakika mimi ninakutahadharisheni kama alivyo watahadharisha Nabii Nuhu watu wake".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Anawaeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake Maswahaba zake kuhusu Dajali, sifa zake, na dalili zake, kwa mambo ambayo hakuna Nabii yeyote aliyetangulia kuyasimulia kabla yake, miongoni mwa hayo ni:
Chongo wa jicho.
Na Mwenyezi Mungu kampa kitu mfano wa Pepo na Moto, kulingana na mtazamo wa macho.
Bali Pepo yake ni Moto na Moto wake ni Pepo, mwenye kumtii atamuingiza katika Pepo hii kama watu wanavyoiona, lakini uhalisia wake ni Moto wenye kuunguza, na atakayemuasi atamuingiza Motoni kama watu wanavyouona, lakini kwa uhalisia ni Pepo nzuri. Kisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake akatuonya dhidi ya fitina yake kama vile Nuhu alivyowaonya watu wake kuhusu hilo.
Mafunzo
Ukubwa wa fitina ya Dajali.
Kuokoka kutokana na fitina ya Dajali kupo katika imani ya kweli, na kukimbilia kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kutafuta hifadhi kwa Mwenyezi Mungu dhidi yake katika tashahudi ya mwisho, na kuhifadhi aya kumi za mwanzo wa Suratul-Kahf.
Pupa kubwa ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake kwa umma wake, alipowawekea wazi Waislamu sifa za Dajali ambazo hakuna mtume kabla yake aliyewahi kuzieleza.
Marejeo
صحيح البخاري (4/ 134) (3338).
صحيح مسلم (4/ 2250) (2936).
عن أنس بن مالك رضي الله عنه مرفوعاً: أخبر النبي صلى الله عليه وسلم : "أنه يأتي فيسجد لربه ويحمده [لا يبدأ بالشفاعة أولا]، ثم يقال له: "ارفع رأسك وقل يُسمع، وسَلْ تُعط، واشفع تُشفَّع".
Kutoka kwa Anasi bin Maliki -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Hadithi Marfu'u: Alieleza Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- "kwamba yeye atakuja asujudu kwa Mola wake na amtukuze [hatoanza na kuomba utetezi kwanza], kisha ataambiwa: "Nyanyua kichwa chako na sema yasikilizwe, na omba upewe, na taka utetezi utetewe".
Wamekubaliana Bukhaariy na MuslimDarajaSahihi
Maelezo
Atakuja Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na Amani ziwe juu yake- siku ya kiyama atasujudu kwaajili ya Mwenyezi Mungu, na aombe, kisha amuidhinishe Mwenyezi Mungu katika utetezi mkubwa, na aseme Mola wake kumwambia: Omba upewe, na taka utetezi utetewe, Yaani ombi lako ni lenye kukubalika na utetezi wako ni wenye kukubalika.
Marejeo
1- القول المفيد على كتاب التوحيد، دار ابن الجوزي، المملكة العربية السعودية، الطبعة: الثانية, محرم، 1424ه.
2- صحيح البخاري، المحقق: محمد زهير بن ناصر الناصر، الناشر: دار طوق النجاة (مصورة عن السلطانية بإضافة ترقيم ترقيم محمد فؤاد عبد الباقي)، الطبعة: الأولى، 1422هـ.
3- صحيح مسلم، المحقق: محمد فؤاد عبد الباقي، الناشر: دار إحياء التراث العربي – بيروت.
Kutoka kwa Ubada bin -Radhi za Allah ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume Rehema na amani za Allah ziwe juu yake amesema: "Atakaye shuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu yeye pekee asiye na mshirika nakuwa Muhammadi ni mjumbe wake na ni mja wake, nakuwa Issa ni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na neno lake alilolipeleka kwa Mariam na ni roho toka kwake, na pepo ni kweli na moto ni kweli, atamuingiza Mwenyezi Mungu peponi kulingana na yale aliyokuwa nayo katika matendo".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Anatueleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- yakuwa atakayetamka neno la tauhidi kwa kujua maana yake, kwa kuyafanyia kazi madhumuni yake, na akashuhudia utumwa wa Muhammadi -Rehema na amani ziwe juu yake- na ujumbe wake, na akakiri utumwa wa Issa na ujumbe wake, Na kuwa Mwenyezi Mungu alimuumba kwa kauli yake "Kuwa" na akawa, na kuwa yeye ni roho miongoni mwa roho alizoziumba Mwenyezi Mungu, Na akamtenga mbali mama yake kwa yale waliyomnasibisha nayo Mayahudi, Nakuwa atakayeamini pepo kuwa ni kweli, na kuwa Moto ni kweli, akaitakidi uwepo wake, nakuwa hizo ni neema za Mwenyezi Mungu na adhabu yake, Na atakayekufa katika imani hiyo; basi mafikio yake ni Peponi hata kama alikuwa mzembe katika ibada, na anamadhambi.
Mafunzo
Mwenyezi Mungu Mtukufu kamuumba Issa mwana wa Mariamu kwa neno (Kuwa) bila baba.
Kinachowakusanya pamoja kati ya Issa (Yesu) na Muhammadi amani iwe juu yao wote ni kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu na Mitume wake, basi wao wote wawili ni Mitume hawasemi uongo, na ni waja wala hawaabudiwi.
Ubora wa tauhidi na kufuta kwake madhambi, nakuwa mafikio ya mtu wa tauhidi ni Peponi, hata kama yakajitokeza kwake baadhi ya madhambi.
Marejeo
صحيح البخاري (4/ 165) (3435).
صحيح مسلم (1/ 57) (28).
الملخص في شرح كتاب التوحيد، لصالح الفوزان (ص25).
الجديد في شرح كتاب التوحيد، لمحمد القرعاوي (ص36).
Kutoka kwa Swafwan bin Muhrizi amesema: Mtu mmoja alisema kumwambia bin Omari radhi za Allah ziwe juu yao, ulimsikia akisema nini Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu kunong'ona? Akasema: nilimsikia akisema: "Atasogezwa muumini siku ya Kiyama karibu na Mola wake Mlezi Aliyetakasika na Kutukuka, kisha atamuwekea pazia lake, hapo atamuonyesha wazi madhambi yake ili akiri, kisha atasema: Je wayajua? Atasema: Ndiyo Mola wangu ninayajua, atasema: Basi hakika mimi nilikusitiri madhambi haya ulipokuwa duniani, na mimi ninakusamehe madhambi hayo leo hii, hapo atapewa faili la mema yake, na ama makafiri na wanafiki, wataitwa hadharani mbele ya kadamnasi, (kisha patasemwa) hawa ndio waliompinga Mwenyezi Mungu"
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu Mwenyezi Mungu kunong'ona na mja wake muumini siku ya Kiyama, akasema:
Atasogezwa muumini siku ya Kiyama karibu na Mola wake Mlezi kisha atamuwekea pazia lake la kumkinga na watu walioko katika kisimamo, hakuna atakayeona katika pazia hilo zaidi yake, hapo atamwambia:
Je walijua dhambi fulani na fulani... atamtaka akiri madhambi yake yaliyokuwa kati ya mja na Mola wake Mlezi.
Naye atasema: Ndiyo, ewe Mola Mlezi.
Mpaka atakapofadhaika muumini na kuogopa, Mtukufu atamwambia: Mimi niliyasitiri kwako madhambi haya duniani, na mimi leo hii ninayasamehe kwa ajili yako, hapo atapewa faili la mema yake.
Na ama kafiri na mnafiki wataitwa mbele ya kadamnasi: Hawa ndiyo waliomkadhibisha Mola wao Mlezi, basi tambueni kuwa laana za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya madhalimu.
Mafunzo
Fadhila za Mwenyezi Mungu na rehema zake kwa waumini kwa kuwasitiri duniani na Akhera.
Himizo la kumsitiri muumini kwa kadiri iwezekanavyo.
Matendo ya waja yote anayakusanya Mola Mlezi wa waja, yeyote atakayekuta kheri basi na amshukuru Mwenyezi Mungu, na atakayekuta kinyume na hivyo basi asimlaumu yeyote ila nafsi yake, naye atakuwa chini ya maamuzi ya Mwenyezi Mungu.
Amesema bin Hajari: Hadithi nyingi zimeonyesha kuwa waumini wenye maasi siku ya Kiyama watakuwa katika sehemu mbili: Sehemu ya kwanza: Ni yule ambaye maasi yake yatakuwa kati yake na Mola wake Mlezi, ikaonyesha hadithi ya bin Omari kuwa sehemu hii pia itakuwa imegawanyika katika sehemu mbili: Kuna sehemu ambayo maasi yake yatakuwa yamesitiriwa duniani, haya ambayo anayasitiri Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama, na sehemu hii ndiyo iliyotajwa katika hadithi, na sehemu nyingine: Ni wale ambao maasi yao yatakuwa wazi, ikaonyesha maana ya hadithi hii kuwa watakuwa kinyume na hao. Na sehemu ya pili: Ni wale ambao maasi yao yatakuwa kati yao na waja, nao wamegawanyika sehemu mbili pia: Kuna sehemu mabaya yao yatazidi mema yao, hawa watadondoka motoni na watatoka kwa utetezi, na sehemu nyingine: Ni wale yaliolingana sawa mabaya yao na mema yao, hawa hawatoingia peponi mpaka kipite kisasi baina yao.
Marejeo
صحيح البخاري (6/ 74) (4685).
صحيح مسلم (4/ 2120) (2768).
شرح رياض الصالحين، لابن عثيمين (3/ 323).
كنوز رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (7/ 12).
بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (1/ 501).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (1/ 390).
جامع العلوم والحكم في شرح خمسين حديثا من جوامع الكلم، لابن رجب الحنبلي (1/ 452).
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Nilimsikia Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akisema: "Ataikamata Mwenyezi Mungu ardhi, na ataikunja mbingu kwa mkono wake wa kulia kisha atasema: Mimi ndiye Mfalme; wako wapi wafalme wa ardhi?"
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Ameeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu Mtukufu ataikamata Ardhi na kuikusanya, na ataikunja Mbingu kwa mkono wake wa kulia na aikunjekunje na aiondoe na aimalize, kisha asema: Mimi ndiye Mfalme, wako wapi wafalme wa Ardhini?!
Mafunzo
Ukumbusho wa kuwa Ufalme wa Mwenyezi Mungu ndio wenye kubakia, na Ufalme wa asiyekuwa yeye ni wenye kuondoka.
Utukufu wa Mwenyezi Mungu na Ukubwa wa kudura zake na mamlaka yake na ukamilifu wa Ufalme wake.
Marejeo
صحيح البخاري (6/ 126) (4812)، صحيح مسلم (4/ 2148) (2787)، فتح الباري (13/367)، عمدة القاري شرح صحيح البخاري (23/ 101)، البحر المحيط الثجاج (43/324).
Imepokelewa kutoka kwa Abdullahi Bin Amrou -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Birika langu ukubwa wake ni sawa na mwendo wa mwezi mzima, maji yake ni meupe kuliko maziwa, na harufu yake ni nzuri kuliko ya Miski, Vikombe vyake ni kama idadi ya nyota za mbinguni, yeyote atakaye kunywa kwenye birika hilo hatopatwa na kiu milele"
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Ametoa habari Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa yeye atakuwa na Birika siku ya Kiyama urefu wa Birika hilo ni sawa na mwendo wa miguu wa mwezi mzima, na upana wake hivyo hivyo, Na kuwa maji yake ni meupe kulio maziwa, Na kuwa harufu yake ni nzuri kuliko harufu ya Miski, Na Mabirika yake ni mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi wake, Atakaye kunywa katika Mabirika hayo hatopatwa na kiu milele.
Mafunzo
Birika la Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- ni mkusanyiko mkubwa wa maji wanaokwenda kunywa humo waislamu miongoni mwa watu wa umma wake siku ya kiyama.
Kupata neema kwa mwenye kunywa katika Birika na kwa hivyo hatopata kiu milele.
Marejeo
صحيح البخاري (8/ 119) (6579)، صحيح مسلم (4/ 1793) (2292)، المفهم (6/91)، فتح الباري (11/472)، التنوير شرح الجامع الصغير (5/387)، فتح المنعم شرح صحيح مسلم (9/125).
Imepokelewa kutoka kwa Asmaa Bint Abii Bakari-Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote na baba yake- amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na amani ziwe juu yake: "Kwa hakika mimi nitakuwa kwenye Birika langu namtazama kila mwenye kuja kwangu kunywa, na kuna watu watafukuzwa, na nitasema: Ewe Mola wangu huyu anatokana na mimi na ni katika umma wangu, basi ataambiwa: Hivi unajua waliyoyafanya baada yako? Namuapia Mwenyezi Mungu, hawakuacha kurudi nyuma na kutoka katika dini yao."
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Anaweka wazi Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- yakuwa siku ya Kiyama yeye atakuwa kwenye Birika lake ili amuone kila mwenye kuja kwenye Birika katika watu wa umma wake. Na watachukuliwa watu wakiwa karibu na Mtume -Amani iwe juu yake- basi atasema: Ewe Mola wangu hao ni wangu na nikatika umma wangu, Basi kutasemwa: Je unajua walichofanya baada ya wewe kuachana nao? Namuapia Mwenyezi Mungu hawakuwacha kurudi nyuma na kutoka katika dini yao, hivyo basi hao siyo watu wako wala si katika umma wako.
Mafunzo
Huruma ya Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-kwa umma wake na kuwatilia umuhimu.
Hatari ya kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume-Rehema na amani ziwe juu yake.
Himizo la kushikamana na sunna za Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake.
Marejeo
صحيح البخاري (8/ 121) (6593)، صحيح مسلم (4/ 1793) (2292)، عمدة القاري (23/144)، البحر المحيط الثجاج (37/322).
Kila hadithi, daraja, maelezo na funzo hapa vinaonyeshwa kama HadeethEnc.com inavyovichapisha, kwa masharti yake ya kuchapisha upya. Daraja halimtaji aliyelitoa. Tafsiri na maelezo ni ya waandishi wake wenyewe, na baadhi hutaja hukumu; wahakiki wa Sabīl hawajavichunguza. Hadithi ya Kiarabu ndiyo matini. Chanzo: HadeethEnc.com