Ruka hadi kwenye maudhui
Hadithi zenye maelezo

Sifa za Swala.

Hadithi 18

Yakwamba Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- Alikuwa akinyanyua mikono yake usawa wa mabega yake anapofungua swala,

عَن ابْنِ عُمَرَ رضي الله عنهما: أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ يَرْفَعُ يَدَيْهِ حَذْوَ مَنْكِبَيْهِ إِذَا افْتَتَحَ الصَّلَاةَ، وَإِذَا كَبَّرَ لِلرُّكُوعِ، وَإِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ الرُّكُوعِ، رَفَعَهُمَا كَذَلِكَ أَيْضًا، وَقَالَ: «سَمِعَ اللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ، رَبَّنَا وَلَكَ الحَمْدُ»، وَكَانَ لاَ يَفْعَلُ ذَلِكَ فِي السُّجُودِ.
Na kutoka kwa Ibn Omari Radhi za Allah ziwe juu yake na baba yake: Yakwamba Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- Alikuwa akinyanyua mikono yake usawa wa mabega yake anapofungua swala, na anapotoa takbira ya kurukuu, na anaponyanyua kichwa chake kutoka katika rukuu anainyanyua pia, na akasema: "Sami'a llaahu liman hamidahu" Yaani: Amemsikia Mwenyezi Mungu yule aliyemuhimidi, "Rabbanaa walakal hamdu" Mola wetu Mlezi na sifa njema ni zako, na alikuwa hafanyi hivyo katika sijida.
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Mtume, rehema na amani ziwe juu yake alikuwa akinyanyua mikono yake katika sehemu tatu wakati wa kuswali, usawa wa mabega ni: Pale panapounga kati ya mfupa wa bega na mkono. Sehemu ya kwanza: Anapofungua swala wakati wa takbira ya kuhirimia swala. Sehemu ya pili: Anapotoa takbira kwa ajili ya rukuu. Sehemu ya tatu: Anaponyanyua kichwa chake kutoka katika rukuu, na akasema: Sami'allahu liman hamidah, Rabbanaa walakal hamdu. Amemsikia Mwenyezi Mungu mwenye kumhimidi, Mola wetu Mlezi, na sifa njema ni zako. Na alikuwa hanyanyui mikono yake wakati wa kuanza kusujudu, wala wakati wa kunyanyua kutoka katika sijida.

Mafunzo
  1. Katika hekima za kunyanyua mikono ndani ya swala, ni pambo la swala, na ni kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu.
  2. Imethibiti kutoka kwake rehema na amani ziwe juu yake, kuwa alinyanyua mikono yake katika nafasi ya nne, kama ilivyokuja katika riwaya ya Abuu Humaid Al-Sa'idi kwa Abuu Daudi na wengineo, ambayo ni wakati wa kusimama kutoka tashahudi ya kwanza. katika swala ya rakaa tatu na nne.
  3. Imethibiti vile vile kutoka kwake rehema na amani zimshukie, pia alikuwa akinyanyua mikono yake usawa wa masikio yake bila ya kuyagusa, kama ilivyo katika riwaya ya Maliki bin Al-Huwairith katika Sahihi mbili: “Yakwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani zimshukie, alikuwa akinyanyua mikono yake mpaka inalingana na masikio yake.”
  4. Na kukusanya kati ya kusema: "Sami'allaahu liman hamidah, na kusema: "Rabbanaa walakal hamdu, hii ni maalumu kwa Imamu na anayeswali peke yake, ama maamuma yeye atasema: Rabbanaa walakal hamdu, pekee.
  5. Kusema: Rabbanaa walakal hamdu “Mola wetu Mlezi na sifa njema ni zako” baada ya kurukuu ni sahihi kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake, kuna namna nne, na hii ni mojawapo, na ni bora kwa mtu afuatilie namna hizi zote, ili wakati mwingine analeta hii, na wakati mwingine analeta hii.
Marejeo

صحيح البخاري (1/ 148) (735). صحيح مسلم (1/ 292) (390). الإلمام بشرح عمدة الأحكام، لإسماعيل الأنصاري (1/ 122). تيسير العلام شرح عمدة الأحكام، للبسام (ص151). تنبيه الأفهام شرح عمدة الأحكام، لابن عثيمين (2/ 192).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Alinifundisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake, namna ya tashahudi iletwayo ndani ya sala, na kiganja changu kikiwa kati ya viganja vyake, kama anavyonifundisha sura ndani ya Qur'ani

عَنِ ابْنَ مَسْعُودٍ رضي الله عنه قَالَ: عَلَّمَنِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، وَكَفِّي بَيْنَ كَفَّيْهِ، التَّشَهُّدَ، كَمَا يُعَلِّمُنِي السُّورَةَ مِنَ القُرْآنِ: «التَّحِيَّاتُ لِلَّهِ، وَالصَّلَوَاتُ وَالطَّيِّبَاتُ، السَّلاَمُ عَلَيْكَ أَيُّهَا النَّبِيُّ وَرَحْمَةُ اللَّهِ وَبَرَكَاتُهُ، السَّلاَمُ عَلَيْنَا وَعَلَى عِبَادِ اللَّهِ الصَّالِحِينَ، أَشْهَدُ أَنْ لاَ إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ، وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ». وفي لفظ لهما: «إِنَّ اللهَ هُوَ السَّلَامُ، فَإِذَا قَعَدَ أَحَدُكُمْ فِي الصَّلَاةِ فَلْيَقُلْ: التَّحِيَّاتُ لِلَّهِ وَالصَّلَوَاتُ وَالطَّيِّبَاتُ السَّلَامُ عَلَيْكَ أَيُّهَا النَّبِيُّ وَرَحْمَةُ اللهِ وَبَرَكَاتُهُ، السَّلَامُ عَلَيْنَا وَعَلَى عِبَادِ اللهِ الصَّالِحِينَ، فَإِذَا قَالَهَا أَصَابَتْ كُلَّ عَبْدٍ لِلَّهِ صَالِحٍ فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ، أَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ، وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، ثُمَّ يَتَخَيَّرُ مِنَ الْمَسْأَلَةِ مَا شَاءَ».
Kutoka kwa bin Masoud radhi za Allahi ziwe juu yake amesema: Alinifundisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake, namna ya tashahudi iletwayo ndani ya sala, na kiganja changu kikiwa kati ya viganja vyake, kama anavyonifundisha sura ndani ya Qur'ani: "Attahiyyaatu lillaahi, wasswalawaatu wattwayyibaatu, assalaamu a'laika ayyuhan nabiyyu, warahmatullaahi wabarakaatuh, assalaamu a'lainaa wa a'laa ibaadillaahi sswaalihiin, ash-hadu anlaa ilaaha illa llaahu, wa ash-hadu anna Muhammadan 'abduhu warasuuluhu" Tafsiri yake: Maamkizi (Amani) ni ya Mwenyezi Mungu, na swala na vile vilivyo vizuri, amani iwe juu yako ewe Nabii na rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake, amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Mwenyezi Mungu, nashuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, na ninashuhudia kuwa Muhammadi ni mja wake na ni mjumbe wake. Na katika lafudhi yao nyingine: "Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Amani, atakapokaa mmoja wenu katika swala basi na aseme: Attahiyyaatu lillaahi, wasswalawaatu wattwayyibaatu, assalaamu a'laika ayyuhan nabiyyu, warahmatullaahi wabarakaatuh, assalaamu a'lainaa wa a'laa ibaadillaahi sswaalihiin, akisema hivyo, basi dua hii itampata kila mja mwema wa Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini, ash-hadu anlaa ilaaha illa llaahu, wa ash-hadu anna Muhammadan 'abduhu warasuuluhu, kisha baada ya hapo atachagua maombi yoyote anayotaka kuomba".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Mtume Rehema na amani ziwe juu yake alimfundisha bin Masoud Radhi za Allah ziwe juu yake tashahudi inayosemwa ndani ya swala, akiwa kaweka mkono wake ndani ya mikono yake, ili asogeze karibu umakini wa bin Masoud. Na alifanya hivyo kama anavyomfundisha sura ndani ya Qur'ani jambo linaloonyesha kuwa Mtume Rehema na amani ziwe juu yake aliitilia umuhimu tashahudi kwa matamshi na maana yake pia. Akasema: "Attahiyyaatu lillaah" (Maamkizi Mema ni ya Mwenyezi Mungu): Nayo ni kila kauli au kitendo kinachojulisha kutukuza, vyote hivyo vinastahiki kufanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. "Swala": Nazo ni swala zinazofahamika za Faradhi na za sunna zote hizo ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. "Mambo mazuri": Nayo ni maneno na matendo na sifa njema zinazojulisha ukamilifu, zote hizo zinamstahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu. "Amani iwe kwako ewe Nabii na Rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake": Hii ni dua yake ya kuomba amani na uzima dhidi ya kila maafa na yenye kuchukiza, na kuomba ziada na wingi kutoka katika kila kheri. "Amani iwe juu yetu na kwa waja wema wa Mwenyezi Mungu": Hii ni dua ya kuomba uzima kwa kila mwenye kuswali na kwa kila mja mwema aliye mbinguni na ardhini. "Ninashuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu": Yaani ninakiri kukiri kwenye kuondoa shaka kabisa yakuwa hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. "Na kuwa Muhammadi ni mja wake na ni Mtume wake": Ninakiri kwake kuwa ni mja na kapewa ujumbe wa mwisho. Kisha akamhimiza Mtume Rehema na amani ziwe juu yake mwenye kuswali achague katika dua aitakayo.

Mafunzo
  1. Mahala pa tashahudi hii ni wakati wa kukaa baada ya sijida ya mwisho katika kila swala, na baada ya rakaa ya pili katika swala za rakaa tatu na nne.
  2. Uwajibu wa tashahudi katika swala, na inafaa akatoa tashahudi kwa lafudhi yoyote katika lafudhi za tashahudi katika zile zilizothibiti kutoka kwa Mtume Rehema na amani ziwe juu yake.
  3. Inafaa kuomba dua ndani ya swala kwa jambo alitakalo mtu madam si dhambi.
  4. Inapendeza kuanza kujiombea mwenyewe kwanza katika dua.
Marejeo

صحيح البخاري (8/ 59) (6265). صحيح مسلم (1/ 301) (402). الإلمام بشرح عمدة الأحكام، لإسماعيل الأنصاري (1/ 168). تيسير العلام شرح عمدة الأحكام، للبسام (ص206). خلاصة الكلام شرح عمدة الأحكام، لفيصل آل مبارك (ص94).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Linganeni sawa katika sijida, na asikunjue mmoja wenu mikono yake kama anavyokunjua mbwa

عن أَنَس بن مالك رضي الله عنه عَنْ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: «اعْتَدِلُوا في السجود، ولا يَبْسُطْ أحدكم ذِرَاعَيْهِ انْبِسَاطَ الكلب».
Kutoka kwa Anas bin Maliki -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake- Amesema: "Linganeni sawa katika sijida, na asikunjue mmoja wenu mikono yake kama anavyokunjua mbwa".
Wamekubaliana Bukhaariy na MuslimDarajaSahihi
Maelezo

Ameamrisha Nabii -Rehema na Amani ziwe juu yake- kulingana katika sijida, na hii nikuwa, ili mwenye kuswali awe na muonekano mzuri katika sijida, kiasi kwamba aweke viganja vyake katika ardhi, na anyanyue miundi yake na aiweke mbali na mbavu zake, kwasababu hali hii ndio anuani ya uchangamfu na hamu vinavyohitajika ndani ya swala, na ni kwasababu muonekano huu mzuri unaviwezesha viungo vya kusujudu vyote kuchukua nafasi yake katika ibada. Na akakatazwa kunyoosha mikono miwili katika sijida; kwasababu hii ni dalili ya uvivu na uchovu, na kuna kujifananisha na mbwa, nako nikujifananisha na kisichofaa.

Marejeo

- صحيح البخاري -الجامع الصحيح-؛ للإمام أبي عبد الله محمد بن إسماعيل البخاري، عناية محمد زهير الناصر، دار طوق النجاة، الطبعة الأولى، 1422هـ. - صحيح مسلم؛ للإمام مسلم بن الحجاج، حققه ورقمه محمد فؤاد عبد الباقي، دار عالم الكتب، الرياض، الطبعة الأولى، 1417هـ. - الإلمام بشرح عمدة الأحكام للشيخ إسماعيل الأنصاري -مطبعة السعادة- الطبعة الثانية 1392ه. - تنبيه الأفهام شرح عمدة الأحكام -محمد بن صالح العثيمين -رحمه الله- مكتبة الصحابة -الشارقة- الإمارات العربية المتحدة، الطبعة الأولى، 1426هـ. - تيسير العلام شرح عمدة الأحكام -عبد الله البسام- تحقيق محمد صبحي حسن حلاق -مكتبة الصحابة- الشارقة، الطبعة العاشرة، 1426هـ.

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Rudi kaswali, kwani wewe hujaswali

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه: أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ دَخَلَ المَسْجِدَ فَدَخَلَ رَجُلٌ، فَصَلَّى، فَسَلَّمَ عَلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَرَدَّ وَقَالَ: «ارْجِعْ فَصَلِّ، فَإِنَّكَ لَمْ تُصَلِّ»، فَرَجَعَ يُصَلِّي كَمَا صَلَّى، ثُمَّ جَاءَ، فَسَلَّمَ عَلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَقَالَ: «ارْجِعْ فَصَلِّ، فَإِنَّكَ لَمْ تُصَلِّ» ثَلاَثًا، فَقَالَ: وَالَّذِي بَعَثَكَ بِالحَقِّ مَا أُحْسِنُ غَيْرَهُ، فَعَلِّمْنِي، فَقَالَ: «إِذَا قُمْتَ إِلَى الصَّلاَةِ فَكَبِّرْ، ثُمَّ اقْرَأْ مَا تَيَسَّرَ مَعَكَ مِنَ القُرْآنِ، ثُمَّ ارْكَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ رَاكِعًا، ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَعْدِلَ قَائِمًا، ثُمَّ اسْجُدْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ سَاجِدًا، ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ جَالِسًا، وَافْعَلْ ذَلِكَ فِي صَلاَتِكَ كُلِّهَا».
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-: Ya kwamba Mtume rehema na amani ziwe juu yake aliingia msikitini kisha akaingia mtu mmoja, akaswali, kisha akamsalimia Mtume rehema na amani ziwe juu yake, akajibu salamu, na akasema: "Rudi kaswali, kwani wewe hujaswali", akarudia kuswali kama alivyoswali mwanzo, kisha akaja, akamsalimia Mtume rehema na amani ziwe juu yake, akasema: "Rudi kaswali kwani wewe hujaswali" (akafanya hivyo) Mara tatu, akasema: "Namuapa yule aliyekutuma kwa haki, siwezi kuswali vizuri zaidi ya hivyo, basi naomba nifundishe, akasema: "Utakaposimama katika swala basi toa takbira (sema: Allaahu Akbaru), kisha soma kiasi chepesi ulichonacho katika Qur'ani, kisha rukuu mpaka utulizane ukiwa umerukuu, kisha nyanyuka mpaka ulingane wima, kisha sujudu mpaka utulizane ukiwa umesujudu, kisha nyanyuka mpaka utulizane ukiwa umekaa, na ufanye hivyo katika swala yako yote".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Aliingia Mtume rehema na amani ziwe juu yake msikitini, akaingia baada yake mtu mmoja akaswali rakaa mbili haraka haraka, na hakutulizana katika kisimamo chake na rukuu yake na sijida yake, na alikuwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake akimfuatilia katika swala yake, akaja kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake akiwa kakaa pembezoni mwa msikiti, akamsalimia, akamjibu salamu, na akasema kumwabia: Nenda karudie swala; kwani wewe hujaswali. Akarudi na akaswali haraka kama alivyoswali mwanzo, kisha akaja akamsalimia Mtume rehema na amani ziwe juu yake, akasema kuwambia: Rudi kaswali; kwani wewe hujaswali, alifanya hivyo mara tatu. Yule bwana akasema: Namuapa yule aliyekutuma kwa haki, siwezi kufanya vizuri zaidi ya hivyo, basi nifundishe, akasema rehema na amani ziwe juu yake: Utakaposimama katika swala basi toa takbira ya kuhirimia swala, kisha soma mama wa Qur'ani (Suratul-Faatiha) na kile atakachotaka Mwenyezi Mungu ukisome, kisha rukuu mpaka utulizane ukiwa umerukuu kwa kuweka viganja vyako juu ya magoti yako na unyooshe mgongo wako na umakinike katika rukuu yako, kisha nyanyuka na unyooshe mgongo wako mpaka mifupa irudi katika viungo vyake na ulingane sawa ukiwa wima, kisha sujudu mpaka utulizane ukiwa umesujudu kwa kuliweka sawa paji la uso na pua, na mikono miwili na magoti mawili na ncha za vidole vya miguu miwili juu ya ardhi, kisha nyanyuka mpaka utulizane ukiwa umekaa kati ya sijida mbili, kisha fanya hivyo katika kila rakaa ndani ya swala yako.

Mafunzo
  1. Nguzo hizi za swala hazidondoki kwa kusahau wala kwa ujinga, kwa dalili ya kuamrishwa mwenye kuswali kurudia, na wala hakutosheka Mtume rehema na amani ziwe juu yake na kumfundisha pekee.
  2. Kutulia ni nguzo miongoni mwa nguzo za swala.
  3. Amesema Nawawi: Na hapa nikuwa atakayepunguza baadhi ya wajibu za swala basi haitoswihi swala yake.
  4. Amesema Nawawi: Na ndani ya hili kuna kumhurumia mwenye kujifunza na mjinga na kuwa mpole kwake, na kumuwekea wazi maswala na kufupisha makusudio, na kufupisha katika haki zake yale ya muhimu pasina yale yenye kukamilisha, ambayo yanategemea mpaka kuyahifadhi na kuyatekeleza.
  5. Amesema Nawawi: Na hapa nikuwa Mufti akiulizwa kuhusu jambo na kukawa na jambo jingine muhimu zaidi analolihitajia muulizaji lakini hakuliulizia basi ni sunna alieleze, na hii inakuwa ni katika nasaha na si katika kuzungumza yasiyomuhusu.
  6. Fadhila za kukiri mapungufu, kwa kauli yake: "Siwezi kufanya vizuri zaidi ya hivyo, basi nifundishe".
  7. Amesema bin Hajari: Hapa kuna kuamrisha mema na kukataza maovu, na mwenye kujifunza kumuomba mwalimu amfundishe.
  8. Sunna ya kutoa salamu wakati wa kukutana, na uwajibu wa kuitikia, na kwamba inapendeza kukutana mara kwa mara hata kama muda utakaribiana, na kwamba ni lazima kuitikia kwa kila mara.
Marejeo

صحيح البخاري (1/ 152) (757). صحيح مسلم (1/ 298) (397). تيسير العلام، للبسام (ص167). تنبيه الأفهام، للعثيمين (2/ 213). الإفهام في شرح عمدة الأحكام، عبد العزيز بن باز (ص203). الإلمام بشرح عمدة الأحكام، لإسماعيل الأنصاري (1/ 138).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Alikuwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake akifungua swala kwa takbira (Allaahu Akbaru) na kisomo kwa kuanza na Alhamdulillaahi Rabbil a'alamiin

عَنْ عَائِشَةَ أُمِّ المُؤْمِنين رَضيَ اللهُ عنها قَالَتْ: كَانَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَسْتَفْتِحُ الصَّلَاةَ بِالتَّكْبِيرِ، وَالقِرَاءَةِ، بِـ الحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ العَالَمِينَ، وَكَانَ إِذَا رَكَعَ لَمْ يُشْخِصْ رَأْسَهُ وَلَمْ يُصَوِّبْهُ، وَلَكِنْ بَيْنَ ذَلِكَ، وَكَانَ إِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ الرُّكُوعِ لَمْ يَسْجُدْ حَتَّى يَسْتَوِيَ قَائِمًا، وَكَانَ إِذَا رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ السَّجْدَةِ لَمْ يَسْجُدْ حَتَّى يَسْتَوِيَ جَالِسًا، وَكَانَ يَقُولُ فِي كُلِّ رَكْعَتَيْنِ التَّحِيَّةَ، وَكَانَ يَفْرِشُ رِجْلَهُ اليُسْرَى وَيَنْصِبُ رِجْلَهُ اليُمْنَى، وَكَانَ يَنْهَى عَنْ عُقْبَةِ الشَّيْطَانِ، وَيَنْهَى أَنْ يَفْتَرِشَ الرَّجُلُ ذِرَاعَيْهِ افْتِرَاشَ السَّبُعِ، وَكَانَ يَخْتِمُ الصَّلَاةَ بِالتَّسْلِيمِ.
Imepokelewa kutoka kwa Aisha mama wa waumini radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Alikuwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake akifungua swala kwa takbira (Allaahu Akbaru) na kisomo kwa kuanza na Alhamdulillaahi Rabbil a'alamiin, na alikuwa anaporukuu hanyanyui wala hainamishi kichwa chake, lakini kati na kati, na alikuwa anaponyanyua kichwa chake kutoka katika rukuu hasujudu mpaka alingane wima, na alikuwa anaponyanyua kichwa chake kutoka katika sijida hasujudu mpaka alingane sawa kwa kukaa, na alikuwa akisoma tahiyatu kila baada ya raka mbili, na alikuwa akiutandika mguu wake wa kushoto na kuusimamisha mguu wake wa kulia, na alikuwa akikataza mkao wa Shetani, na akikataza mtu kulaza mikono yake kama wanyama wakali, na alikuwa akihitimisha swala kwa salamu
Imepokelewa Imamu MuslimDarajaSahihi
Maelezo

Ameeleza Mama wa waumini Aisha radhi za Allah ziwe juu yake sehemu ya swala ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake yakwamba alikuwa akifungua swala yake kwa takbira ya kufungua swala, akisema: "Allaahu Akbaru", na akifungua kisomo kwa suratul Faatiha. "Alhamdulillaah Rabbil A''alamiin..." Na alikuwa anaporukuu baada ya kisimamo, hainui kichwa chake na wala hakishushi wakati wa rukuu, bali anakifanya kilingane sawa kikiwa kimenyooka, na akinyanyua kichwa chake kutoka katika rukuu ananyooka wima kabla hajasujudu, na akinyanyua kichwa chake kutoka katika sijida ya kwanza, hasujudu sijida ya pili mpaka atuliazane akiwa amekaa. Na alikuwa akikaa baada ya kila rakaa mbili kwa ajili ya tahiyatu, na anasema: "Attahiyyatu lillaahi was swalawaatu wat twayyibaatu...", na alikuwa anapokaa baina ya sijida mbili au kwa ajili ya tahiyatu analaza mguu wake wa kushoto na kuukalia, na anasimamisha mguu wake wa kulia. Na anamkataza mwenye kuswali kukaa ndani ya swala yake kama mkao wa Shetani, nao ni kulaza miguu yake yote miwili katika Ardhi, na kukaa kwa pande zake mbili za nyuma, au kuambatanisha makalio yake na Ardhi na akasimamisha miguu yake na kuweka mikono yake katika Ardhi kama anavyoitandaza mbwa, au akalaza mwenye kuswali mikono yake kwa kuinyoosha katika sijida kama anavyoilaza mnyama mkali. Na alikuwa akihitimisha swala yake kwa salamu: "Assalaam alaikum warahmatullah" upande wa kulia mara moja na mara nyingine upande wa kushoto.

Mafunzo
  1. Kumebainishwa kiasi kidogo cha namna ya swala ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake.
  2. Uwajibu wa takbira ya kuhirimia swala, inayoharamisha kila kauli au kitendo kinachopingana na kauli za swala na vitendo vyake, na kwamba kinyume na namna hiyo hakuna namna nyingine inayofaa kuingia ndani ya swala.
  3. Uwajibu wa kusoma Suratul Faatiha.
  4. Uwajibu wa kurukuu, na jambo bora zaidi ndani yake ni kulingana sawa, bila kuinuka, wala kuinama.
  5. Uwajibu wa kuinuka kutoka katika rukuu, na uwajibu wa kulingana sawa katika kisimamo baada yake.
  6. Uwajibu wa kusujudu, na uwajibu wa kunyanyuka kutoka katika kusujudu, na kulingana sawa wakati wa kukaa baada yake.
  7. Sheria ya kulaza mguu wa kushoto kwa mwenye kuswali na kusimamisha mguu wa kulia katika kukaa ndani ya swala, ama katika tahiyatu ya mwisho katika swala ambayo ina tahiyatu mbili kama Magharibi na Ishaa, sheria ni kukalia kalio moja (Tawaruku), na zimekuja hadithi zingine kuhusu hilo.
  8. Katazo la kujifananisha na Shetani katika kukaa kwake, na hiyo ni mtu kukaa juu ya makalio yake na kulaza miguu yake juu ya Ardhi, au akaisimamisha na akakaa kati kati yake ikiwa katika Ardhi.
  9. Katazo la kujifananisha na wanyama washambuliao katika kutandaza mikono yake, nayo ni kutandaza mikono yake mwenye kuswali katika Ardhi, kwani hilo ni ishara ya uvivu na udhaifu.
  10. Katazo la kujifananisha na Shetani na wanyama katika vitendo vyao.
  11. Uwajibu wa kuhitimisha swala kwa salamu, nayo ni dua kwa wenye kuswali na waliohudhuria na wema wasiokuwepo kwa kuwaombea amani dhidi ya kila shari na mapungufu.
  12. Uwajibu wa kutulizana ndani ya swala.
Marejeo

صحيح مسلم (1/ 357) (498). شرح النووي على مسلم (4/ 213). سبل السلام، لمحمد الصنعاني (1/ 248 ). توضيح الأحكام مِن بلوغ المرام، لعبد الله البسام (2/ 172). فتح ذي الجلال والإكرام شرح بلوغ المرام، لابن عثيمين (2/ 51). تنبيه الأفهام شرح عمدة الأحكام، لابن عثيمين (2/ 189). تيسير العلام شرح عمدة الأحكام، لعبد الله البسام (ص145).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Nimeamrishwa nisujudu kwa viungo saba

عن ابنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما عن النبيِّ صلى الله عليه وسلم قال: «أُمِرْتُ أَنْ أَسْجُدَ عَلَى سَبْعَةِ أَعْظُمٍ: عَلَى الْجَبْهَةِ وَأَشَارَ بِيَدِهِ عَلَى أَنْفِهِ، وَالْيَدَيْنِ، وَالرُّكْبَتَيْنِ، وَأَطْرَافِ الْقَدَمَيْنِ، وَلَا نَكْفِتَ الثِّيَابَ وَالشَّعَرَ».
Imepokelewa kutoka kwa bin Abbas -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao -kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu-Rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - amesema: "Nimeamrishwa nisujudu kwa viungo saba, kwa paji la uso, na akaashiria kwa mkono wake katika pua yake, na mikono miwili na magoti mawili, na ncha za miguu miwili, na wala tusizikunje nguo na nywele".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo

Anabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa Mwenyezi Mungu kamuamrisha wakati wa swala asujudu kwa viungo saba katika viungo vya mwili; navyo ni: Cha kwanza: Paji la uso: Nao ni ubapa wa uso ulioko juu ya pua na macho mawili, Na akaashiria -Rehema na amani ziwe juu yake- kwa mkono wake katika pua yake, akieleza kuwa paji la uso na pua ni kiungo kimoja katika vile saba, na akitia msisitizo kwa mwenye kusujudu kuwa agusishe pua yake katika ardhi. Cha pili: na cha tatu: Ni mikono miwili. Cha nne na cha tano: Ni magoti mawili. Cha sita na cha saba: Ni vidole vya miguu miwili. Na akatuamrisha tusizifunge nywele zetu, au kuzikunja kunja nguo zetu katika ardhi wakati wa kusujudu kwa kuilinda ardhi (Isiguse paji la uso); bali tuziache mpaka zidondoke katika ardhi, ili zisujudu pamoja viungo.

Mafunzo
  1. Uwajibu wa kusujudu katika swala juu ya viungo saba.
  2. Karaha ya kukusanya nguo na nywele ndani ya swala.
  3. Ni wajibu kwa mwenye kuswali atulizane ndani ya swala yake, na hii ni kwa kuweka viungo saba vya kusujudu juu ya ardhi, na atulizane hapo mpaka alete dua zote zilizopangwa na sheria.
  4. Katazo la kufunga nywele hili ni maalumu kwa wanaume pasina wanawake; kwa sababu mwanamke ndani ya swala ameamrishwa kujisitiri
Marejeo

صحيح البخاري (1/ 162) (812). صحيح مسلم (1/ 354) (490). المنهاج شرح صحيح مسلم، للنووي (4/ 206). مرقاة المفاتيح شرح مشكاة المصابيح، لعلي القاري (2/ 718). سبل السلام شرح بلوغ المرام، للصنعاني (1/ 270). توضيح الأحكام مِن بلوغ المرام، لعبد الله البسام (2/ 229). فتح ذي الجلال والإكرام شرح بلوغ المرام، لابن عثيمين (2/ 115). منار القاري، لحمزة قاسم (2/ 202).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Utakaposujudu basi weka viganja vyako, na unyanyue viwiko vyako

عَنِ الْبَرَاءِ رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: «إِذَا سَجَدْتَ، فَضَعْ كَفَّيْكَ وَارْفَعْ مِرْفَقَيْكَ».
Kutoka kwa Suhaib -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani ziwe juu yake: "Utakaposujudu basi weka viganja vyako, na unyanyue viwiko vyako".
Imepokelewa Imamu MuslimDarajaSahihi
Maelezo

Amebainisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake hali ya mikono miwili katika sijida ya swala, nayo ni kwa kuviweka vizuri viganja vyake katika ardhi na aviweke vidole vikiwa vimefungamanishwa kuelekea kibla, na viwe viwiko viwili -maungio ya mkono na muundi wake- viwe vimenyanyuka na viko mbali na kugusa Ardhi, na vimeachanishwa na mbavu.

Mafunzo
  1. Jambo la wajibu kwa mwenye kuswali ni kuweka viganja vyake juu ya Ardhi, na viganja viwili ni viungo katika viungo saba vya kusujudu.
  2. Ni sunna kunyanyua miundi ya mikono isiguse Ardhi, na machukizo ya kuilaza kama anavyolaza mnyama mkali mikono yake.
  3. Sheria ya kuonyesha uchangamfu na nguvu na hamu katika ibada.
  4. Mwenye kusali akiegemea viungo vyake vyote vya kusujudu, kila kiungo kitachukua haki yake katika ibada.
Marejeo

صحيح مسلم (1/ 356) (494). سبل السلام شرح بلوغ المرام، لمحمد الصنعاني (1/ 273). توضيح الأحكام مِن بلوغ المرام، لعبد الله البسام (2/ 235). تيسير العلام شرح عمدة الأحكام، لعبد الله البسام (ص162).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com

Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akisema kati ya sijida mbili: "Allaahumma ghfir lii, warhamnii, wa aafiniii, wahdinii, warzuqniii

عن ابن عباس رضي الله عنهما: كان النبي صلى الله عليه وسلم يقول بين السجدتين: «اللَّهمَّ اغْفِرْ لي، وارْحَمْنِي، وعافِني، واهْدِني، وارزقْنِي».
Imepokewa Kutoka kwa bin Abbas -Radhi za Allah ziwe juu yao yeye na baba yake-: Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akisema kati ya sijida mbili: "Allaahumma ghfir lii, warhamnii, wa aafiniii, wahdinii, warzuqniii".
Imepokelewa na Abu Daud, Tirmidhiy, Ibn Majah na AhmadDarajaNi Nzuri kwa Ushahidi wake mbalimbali
Maelezo

Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akiomba kati ya sijida mbili katika sala yake kwa dua hizi tano ambazo muislamu anazihitajia kwa uhitaji mkubwa, na zimekusanya heri za dunia na akhera, ikiwemo kuomba msamaha na stara ya madhambi na kufutwa kwake, na kumiminiwa rehema, na kusalimishwa na mambo yenye utata na matamanio na maradhi na magonjwa, na kumuomba Allah uongofu katika haki na kudumu katika hilo, na kupewa imani na elimu na matendo mema, na mali nzuri ya halali.

Mafunzo
  1. Sheria ya kuomba dua hii katika kikao kati ya sijida mbili.
  2. Ubora wa dua hizi kwa kukusanya heri za dunia na akhera.
Marejeo

سنن أبي داود (2/ 138) (850). سنن الترمذي (1/ 317) (284). سنن ابن ماجه (2/ 64) (898). مسند أحمد (5/ 72) (2895). مشكاة المصابيح، للتبريزي (1/ 283). سبل السلام شرح بلوغ المرام، لمحمد الصنعاني (1/ 274). توضيح الأحكام مِن بلوغ المرام، لعبد الله البسام (2/ 240).

Hadithi hii kwenye HadeethEnc.com
8 kati ya 18
Hadithi 18
  1. Yakwamba Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- Alikuwa akinyanyua mikono yake usawa wa mabega yake anapofungua swala,
  2. Alinifundisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake, namna ya tashahudi iletwayo ndani ya sala, na kiganja changu kikiwa kati ya viganja vyake, kama anavyonifundisha sura ndani ya Qur'ani
  3. Linganeni sawa katika sijida, na asikunjue mmoja wenu mikono yake kama anavyokunjua mbwa
  4. Rudi kaswali, kwani wewe hujaswali
  5. Alikuwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake akifungua swala kwa takbira (Allaahu Akbaru) na kisomo kwa kuanza na Alhamdulillaahi Rabbil a'alamiin
  6. Nimeamrishwa nisujudu kwa viungo saba
  7. Utakaposujudu basi weka viganja vyako, na unyanyue viwiko vyako
  8. Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akisema kati ya sijida mbili: "Allaahumma ghfir lii, warhamnii, wa aafiniii, wahdinii, warzuqniii
  9. Niliswali pamoja na Mtume rehema na amani ziwe juu yake, alikuwa akitoa salaam kuliani kwake: "Assalaam alaikum warahamatullah wabarakaatuh", na kushotoni kwake: "Assalaam alaikum warahmatullah
  10. Yakwamba Mtume rehema na amani ziwe juu yake alisoma katika rakaa mbili za (sunna ya) Alfajiri {Qul yaa ayyuhal kaafiruun} na {Qul huwallaahu ahad}
  11. Enyi watu! Bila shaka nimefanya hivi ili muige na mjifunze swala yangu
  12. Pindi mtakaposwali basi nyoosheni safu zenu, kisha akuongozeni mmoja wenu, atakapotoa takbira basi toeni takbira
  13. Namuapa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake, hakika mimi ndiye mtu niliyekaribu zaidi kwenu nyinyi swala yangu kufanana na swala ya Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, bila shaka hii ndio ilikuwa swala yake mpaka alipoondoka duniani
  14. Mwizi mbaya zaidi kuliko watu wote, ni yule anayeiba swala yake" Akasema: Ataiba vipi swala yake? Akasema: "Hatimizi rukuu zake wala sijida zake
  15. Alikuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- anaponyanyua mgongo wake kutoka katika rukuu anasema: "Sami'allaahu liman hamidah
  16. Yakwamba Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- alikuwa akisema kati ya sijida mbiliL "Rabbigh-firlii, Rabbigh-firlii
  17. Huyo ni Shetani anaitwa Khinzab, ukimuhisi basi haraka sana taka ulinzi kutoka kwa Allah dhidi yake, na uteme kushotoni kwako mara tatu
  18. Nilikuwa nikimuona Mtume rehema na amani ziwe juu yake akitoa salamu kuliani kwake, na kushotoni kwake, mpaka ninaona weupe wa shavu lake

Kila hadithi, daraja, maelezo na funzo hapa vinaonyeshwa kama HadeethEnc.com inavyovichapisha, kwa masharti yake ya kuchapisha upya. Daraja halimtaji aliyelitoa. Tafsiri na maelezo ni ya waandishi wake wenyewe, na baadhi hutaja hukumu; wahakiki wa Sabīl hawajavichunguza. Hadithi ya Kiarabu ndiyo matini. Chanzo: HadeethEnc.com