ImepokelewaKutoka kwa Jabir radhi za Allah ziwe juu yake yeye na baba yake, hakika yeye alimsikia Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akisema: "Anapoingia mtu nyumbani kwake akamtaja Mwenyezi Mungu wakati wa kuingia kwake na wakati wa chakula chake, Shetani husema: Hakuna malazi kwenu, wala chakula cha usiku, na anapoingia na hakumtaja Mwenyezi Mungu wakati wa kuingia kwake, Shetani husema: Mmepata malazi, na asipomtaja Mwenyezi Mungu wakati wa chakula chake, husema: Mmepata malazi na chakula cha usiku".
Imepokelewa Imamu MuslimDarajaSahihi
Maelezo
Ameamrisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kumtaja Allah wakati wa kuingia nyumbani na kabla ya kupata chakula, nakuwa mtu akimtaja Mwenyezi Mungu kwa kusema: (Bismillaah) -Naanza kwa jina la Mwenyezi Mungu- wakati wa kuingia nyumbani kwake na wakati wa chakula chake, Shetani husema kuwaambia wasaidizi wake: Hamna bahati leo ya kupata malazi wala chakula cha usiku ndani ya nyumba hii ambayo mwenye nyumba kajilinda kutokana nanyi kwa kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ama mtu akiingia nyumbani kwake na akawa hakumtaja Mwenyezi Mungu wakati wa kuingia kwake wala wakati wa kupata kwake chakula, Shetani huwaeleza wasaidizi wake kuwa wamepata mahali pa kulala, na chakula cha usiku ndani ya nyumba hii.
Mafunzo
Ni sunna kumtaja Mwenyezi Mungu wakati wa kuingia nyumbani na wakati wa chakula, kwani Shetani hulala ndani ya majumba, na hula katika chakula cha wenye nyumba ikiwa hawatomtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Shetani humfuatilia mwanadamu katika matendo yake na harakati zake na katika mambo yake yote, akijisahau kumtaja Allah papo hapo hupata lengo lake kwake.
Kumtaja Allah humfukuza Shetani.
Kila Shetani anawafuasi na ana vipenzi ambao huchukua ushauri wake na kufuata amri yake.
Marejeo
صحيح مسلم (3/ 1598) (2018).
بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (2/ 50).
تطريز رياض الصالحين، لفيصل المبارك (ص467).
شرح رياض الصالحين، لابن عثيمين (4/ 190).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (1/ 700).
Kutoka kwa Abuu Huraira -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Anasema Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka: Mimi nipo katika dhana ya mja wangu kwangu, na Mimi nipo naye wakati anaponitaja, atakaponitaja ndani ya nafsi yake nami nitamtaja ndani ya nafsi yangu, na akinitaja katika umati nami nitamtaja katika umati bora kuliko huo, na akisogea kwangu shibri (futi) moja na mimi ninasogea karibu naye kwa mita nzima, na akisogea kwangu kwa mita moja mimi ninasogea kwake kwa zaidi ya mita moja (Baa'a) na akinijia kwa kutembea basi mimi nitamjia kwa mchakamchaka"
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
Mimi nipo katika dhana ya mja wangu kwangu, nitampeleka mja wangu kulingana na dhana yake kwangu na hii ni kwa kutaraji mazuri na kutaraji msamaha, na nitamfanyia yote anayoyataraji kutoka kwangu katika mambo ya kheri au mengineyo; na mimi niko pamoja naye kwa kumhurumia na kumuwezesha na kumuongoza na kumlea na kumuunga mkono pindi anaponitaja.
Akinitaja ndani ya nafsi yake akiwa peke yake amejitenga kwa kunisabihi na kunitukuza au kwa kinginecho; basi nami nitamtaja ndani ya nafsi yangu.
Na akinitaja katika kundi la watu; basi nami nitamtaja katika kundi kubwa na zuri kuliko hilo.
Na atakayesogea kwa Mwenyezi Mungu kwa kiwango cha shibri (futi) moja basi Mwenyezi Mungu humzidishia na kuzidi kujiweka karibu zaidi kwa kiasi cha dhiraa (mita).
Na akijiweka karibu naye kwa kiasi cha dhiraa (mita) anajiweka naye kwa kiasi cha zaidi ya mita moja (Baa'a).
Na akija kwa Mwenyezi Mungu akiwa anatembea Yeye anamjia kwa mchakamchaka.
Mja atakapojiweka karibu na Mola wake Mlezi kwa kumtii na kuelekea kwake, basi Mola Mlezi Mtukufu humzidishia ukaribu ikiwa ni malipo kulingana na amali yake.
Kila unapozidi kukamilika uja (utumwa) wa muumini kwa Mola wake Mlezi Mwenyezi Mungu Mtukufu hujiweka karibu naye, hivyo, kipawa cha Mwenyezi Mungu na thawabu zake ni nyingi kuliko amali za mja na tabu zake, na uhalisia nikuwa thawabu za Mwenyezi Mungu ni nyingi kuliko amali kwa kutazama namna na wingi wake.
Muumini huwa na dhana nzuri, na kutenda mema, na kwenda mbio na kuzidisha mpaka atakapokutana na Mwenyezi Mungu.
Mafunzo
Hadithi hii ni katika yale anayoyapokea Mtume rehema na amani ziwe juu yake kutoka kwa Mola wake, na huitwa Hadithil Qudsi, au Hadithil ilaahi, nayo ni ile ambayo matamshi yake na maana yake inatoka kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa haina mambo maalumu kama ya Qur'ani ambayo inajitofautisha na maneno mengine, kama kisomo chake kutumika kama ibada, na kujitwaharisha kwa ajili yake, na kutoa changamoto, na maswala ya kisayansi na mengineyo.
Amesema Al-Ajurri: Hakika wanaofuata haki humsifu Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa yale aliyojisifu kwayo Mtukufu, na kwa yale aliyomsifu kwayo mtume wake rehema na amani ziwe juu yake, na kwa yale waliyomsifu kwayo Maswahaba radhi za Allah ziwe juu yao, na huu ndio msimamo wa wanachuoni katika wale waliofuata muongozo na wala hawakuzua. Mwisho. Wanaofuata Sunna (Ahlus Sunna) wanamthibitishia Mwenyezi Mungu yale aliyoyathibitisha yeye mwenyewe juu ya nafsi yake miongoni mwa majina na sifa, pasina kupotosha wala kukanusha, wala kuuliza namna yake, wala kupiga mfano, na wanamkanushia Mwenyezi Mungu yale aliyoyakanusha yeye mwenyewe juu ya nafsi yake, na wananyamaza katika yale ambayo haukuja uthibitisho wala kanusho, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Hakuna chochote mfano wake, naye ni msikivu Mwenye kuona".
Kumdhania Allah vizuri ni lazima kuambatane na matendo, amesema Al-Hassan Al-Basari: Hakika muumini alimdhania vizuri Mola wake hivyo akafanya matendo mazuri, na hakika muovu alimdhania vibaya Mola wake kwa hivyo akafanya matendo maovu.
Amesema Qurtubi: Inasemekana kuwa: Maana ya "Dhana ya mja wangu kwangu" ni dhana ya kujibiwa wakati wa kuomba dua, na dhana ya kukubaliwa wakati wa kuomba toba, na dhana ya kusamehewa wakati wa kuomba msamaha, na dhana ya kulipwa wakati wa kufanya ibada kwa sharti zake kwa kushikamana na ahadi za kweli, na ndio mana ni lazima kwa kila mtu ajitahidi kuyasimamia yale aliyo na yakini nayo kuwa hakika Mwenyezi Mungu atamkubalia na atamsamehe; kwa sababu yeye mwenyewe aliahidi hivyo na yeye haendi kinyume na ahadi, akiitakidi au kudhani kuwa Mwenyezi Mungu hatomkubalia nakuwa hayo hayatomnufaisha, huku ndiko kukata tamaa na rehema za Mwenyezi Mungu ambako ni katika madhambi makubwa, na atakayekufa katika hali hiyo atawakilishwa katika kile alichodhania kama ilivyokuja katika baadhi ya riwaya za hadithi iliyotajwa, "Basi mja wangu na anidhanie mimi akatavyo" anasema: Na ama dhana ya kusamehewa ikiwa ni pamoja na mtu kuendelea na madhambi huo ndio ujinga halisi na ni kujidanganya.
Himizo la kumtaja Mwenyezi Mungu ndani ya nafsi yako na kwa ulimi wako vyote kwa pamoja, yaani mtu ndani ya nafsi yake na moyo wake amuogope Mwenyezi Mungu na akumbuke utukufu wake na haki zake na awe na matarajio kwake na amtukuze na ampende na amdhanie vizuri na amtakasie matendo, na atamke kwa ulimi: Sub-haanallaah (Ametakasika Mwenyezi Mungu) Al-hamdulillaah (Kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu, na Laa ilaaha illa llaah (Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu), Allaahu Akbaru (Mwenyezi Mungu Mkubwa), Laa haulaa walaa quwwata illaa billaah (Hapana ujanja wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu).
Amesema bin Abii Hamza: Atakayemtaja akiwa na hofu basi atampa amani, au akiwa mpweke basi atamfariji.
Shibri: Ni urefu wa kuanzia kidole cha mwisho mpaka kidole gumba wakati wa kukunjua kiganja, na Dhiraa: Ni urefu wa kuanzia ncha yakidole cha kati mpaka katika mfupa wa kiwiko, na Baa'a: Ni urefu wa dhiraa mbili za mtu na muundi wake na upana wa kifua chake; ambayo ni kiasi cha Dhiraa nne.
Marejeo
صحيح البخاري (9/ 121) (7405).
صحيح مسلم (4/ 2067) (2675).
كنوز رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (17/ 151).
شرح رياض الصالحين، لابن عثيمين (5/ 516).
منار القاري شرح مختصر صحيح البخاري، حمزة محمد (5/ 372).
الجواب الكافي لمن سأل عن الدواء الشافي أو الداء والدواء (ص25).
بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (2/ 510).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (2/ 983).
Kutoka kwa Abuu Huraira -radhi za Allah ziwe juu yake- yakwamba Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Anafunga shetani juu ya kisogo cha kichwa cha mmoja wenu, pindi anapolala, mafundo matatu, anafunga katika kila fundo usiku kucha na husema : basi lala, pindi anapoamka na akamtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu linafunguka fundo moja, akitawadha, linafunguka fundo jingine, na akiswali, yanafunguka mafundo yake yote, anaamka akiwa na uchangamfu na moyo mkunjufu, na vinginevyo basi anaamka akiwa na nafsi chafu tena mvivu".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Anaeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake hali ya shetani na mapambano yake na mwanadam anayetaka kusimama kwa ajili ya swala ya usiku au Alfajiri.
Muumini anapokwenda kulala shetani hufunga katika kisogo chake -yaani mwisho wa kichwa chake- mafundo matatu.
Muumini atakapoamka na akamtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akawa hajatii wasi wasi wa shetani; fundo moja hufunguka.
Akitawadha linafunguka fundo jingine.
Na ikiwa atasimama akaswali yatafunguka mafundo yote matatu, na atakuwa na uchangamfu wa nafsi; na kufurahi kwake kwa yale aliyoafikishwa na Mwenyezi Mungu katika ibada, akijipa bishara kwa yale aliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu katika thawabu na msamaha, ikiwa ni pamoja na hivyo vilivyomuondokea katika mafundo ya shetani na vikwazo vyake, na asipofanya hivyo atakuwa na nafsi chafu, atakuwa na moyo wenye huzuni, mvivu katika mambo ya kheri na mambo mema; kwa sababu atakuwa kafungwa kwa pingu za shetani, na atakuwa kawekwa mbali na kumkaribia Rahmani (Mwingi wa rehema).
Mafunzo
Shetani siku zote anakwenda mbio katika njia zote za mwanadam; ili azuie kati yake na kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mja hawezi kusalimika na shetani isipokuwa kwa kutaka msaada kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwa kuchukua sababu za kinga na ulinzi.
Kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu kunaleta uchangamfu katika nafsi na kunakunjua kifua, na hufukuza uvivu na kupoa, na huondoa matatizo na hasira; kwa sababu humfukuza shetani, na hili ni katika wasi wasi wake.
Muumini hufurahishwa na taufiki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutekeleza ibada zake, na anasononeka kwa uzembe wake katika kupunguza daraja za fadhila na ukamilifu.
Kujisahahu na kukaa katika maasi ni katika matendo ya shetani na kupambia kwake.
Mambo haya matatu -Kumtaja Mwenyezi Mungu, na udhu, na swala- humfukuza shetani.
Shetani kufunga mwisho wa kichwa pekee; ni kwa sababu ndio kituo cha nguvu, na ndio sehemu ya kutolea maamuzi, akifunga mahali hapo huweza kuitawala roho ya mwanadam, na kumtia usingizi.
Amesema Imam bin Hajari Al-Asqalaani: Umetajwa usiku katika kauli yake: "Tumia usiku huu" Inaonyesha hili ni maalumu kwa usingizi wa usiku.
Amesema bin Hajar Al-Asqalani: Hakuna dhikri makhsusi ambayo haitoshelezi nyingine, bali kila kinachofaa kuitwa dhikri kinatosheleza, na inaingia ndani yake kusoma Qur'ani, kusoma hadithi za Mtume, na kujishughulisha na kusoma elimu ya Kisheria, na jambo bora zaidi lililotajwa ni kauli ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Atakayeshituka usiku kutoka usingizini akasema: "Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika, ufalme ni wake na sifa njema ni zake, naye juu ya kila kitu ni muweza, kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu, na ametakasika Mwenyezi Mungu, na hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Mkubwa, na hapana ujanja wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha akasema: Ewe Mola wangu, nisamehe, au akiomba dua yake itaitikiwa, na akitawadha utakubaliwa udhu wake" Kaipokea Bukhari.
Marejeo
صحيح البخاري (2/ 52) (1142).
صحيح مسلم (1/ 538) (776).
بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (2/ 328).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (2/ 834).
كنوز رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (15/ 305).
فتح الباري شرح صحيح البخاري، لأحمد العسقلاني (10/ 564).
طرح التثريب في شرح التقريب، العراقي (3/ 82).
Kutoka kwa Saad bin Abii Waqas radhi za Allah ziwe juu yake, amesema: Tulikuwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu rehema na amani ziwe juu yake, akasema: "Je anashindwa mmoja wenu kuchuma kila siku mema elfu moja?" Akamuuliza muulizaji miongoni mwa waliokuwa naye kwenye kikao: "Vipi anaweza kuchuma mmoja wetu mema elfu moja?" Akasema: "Atasema Sub-haana llahi mara mia moja (100), kisha ataandikiwa mema elfu (1000), au atafutiwa makosa elfu moja (1000)".
Imepokelewa Imamu MuslimDarajaSahihi
Maelezo
Maswahaba walimuuliza Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Hivi hawezi mmoja wenu kupata katika kila siku mema elfu moja?! Akasema mmoja kati ya waliokaa naye: Ni vipi atapata mtu mema elfu moja kwa siku kwa wepesi? Akasema: Aseme: "Sub-haana llaah" Yaani: Ametakasika Mwenyezi Mungu, mara mia moja; basi hapo ataandikiwa mema elfu moja; kwa sababu jema moja hulipwa mara kumi mfano wake, au yatafutwa kwake makosa elfu moja.
Mafunzo
Himizo la kufanya mazuri; kwa sababu ndio ngazi ya kumfikisha mtu katika utiifu.
Ubora wa kufanya tasbihi (kusema: Sub-haana llaah) na kumtaja Mwenyezi Mungu, na kwamba kazi hii nyepesi ambayo haimgharimu mtu chochote, anapata malipo makubwa kupitia amali hiii.
Hima ya Maswahaba katika kuziendea kheri pasina kuchelewa.
Kuzidishwa kwa mema mpaka mara kumi mfano wake, na hiyo ni kama kauli yake Mtukufu: "Yeyote atakayekuja na jema moja basi atalipwa mara kumi mfano wake" [Al-An'aam:160], na hii ndio daraja ya chini kabisa ya kuzidishiwa, kwani imekuja kuwa ziada hufika mpaka mia saba mara dufu.
Imekuja katika baadhi ya riwaya badala ya (Au) imekuja (Na) katika kauli yake: Au amfutie kwake...Anasema Al-Qaari: Herufi (Wau/na) inaweza kuja ikimaanisha (Au) na riwaya zote hazipingani, maana yake ni kana kwamba: Atakayelisema neno hilo, ataandikiwa mema elfu moja, na asipoandikiwa basi anafutiwa baadhi ya makosa na anachuma malipo kwa sehemu nyingine, na inawezekana kuwa kwa maana ya (Wau/na) au kwa maana ya (Bal/bali) basi hapo atakusanyiwa mambo yote, na fadhila za Mwenyezi Mungu ni pana mno, mwisho wa kunukuu, yaani: Maana yake nikuwa ataandikiwa mema elfu moja na atafutiwa kwake madhambi elfu moja.
Marejeo
صحيح مسلم (4/ 2073) (2698).
بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (2/ 507).
مرقاة المفاتيح، لعلي القاري (4/ 1594).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (2/ 980).
مرعاة المفاتيح شرح مشكاة المصابيح، لعبيد الله المباركفوري (7/ 454).
Na kutoka kwa Abuu Musa -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani ziwe juu yake: "Mfano wa yule anayemtaja Mola wake na yule asiyemtaja Mola wake, ni mfano wa aliyehai na aliyekufa", Na tamko la Muslim: "Mfano wa nyumba anayotajwa Mwenyezi Mungu ndani yake, na nyumba asiyotajwa Mwenyezi Mungu ndani yake, ni mfano wa aliyehai na aliyekufa".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeDarajaSahihi
Maelezo
Anaeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake tofauti kati ya yule anayemtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu na kati ya yule asiyemtaja, kuwa ni mfano wa tofauti iliyopo kati ya aliyehai na aliyekufa katika manufaa yake na uzuri wa muonekano wake, hivyo mfano wa yule anayemtaja Mola wake ni mfano wa aliyehai ambaye muonekano wake umependeza kwa kuwa na nuru ya uhai, na anamanufaa, na mfano wa yule asiyemtaja Mwenyezi Mungu ni mfano wa maiti ambaye muonekano wake umeharibika, na ndani yake kumebatilika, na hana manufaa ndani yake.
Na vile vile nyumba inasifiwa kwa sifa ya kuwa hai endapo wakazi wake wanamtaja Mwenyezi Mungu, na vinginevyo itakuwa nyumba mfu kwa kubweteka wakazi wake na kutomtaja Mwenyezi Mungu; na nyumba ikiitwa hai na maiti wanakusudiwa wakazi wa nyumba hiyo.
Mafunzo
Himizo la kumtaja Mwenyezi Mungu na tahadhari ya kughafilika na hilo.
Dhikri ndio uhai wa roho kama ambavyo roho ni uhai wa mwili.
Katika muongozo wa Mtume rehema na amani ziwe juu yake ni kupiga mifano ili kusogeza karibu maana.
Amesema Imam Nawawi: Hapa kuna wito wa kuja katika kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya nyumba, nakuwa haiachwi tupu pasina kumtaja Mwenyezi Mungu.
Amesema Nawawi: Na pia kuwa na umri mrefu katika utiifu ni fadhila hata ikiwa maiti atahama kwenda katika kheri zaidi; kwa sababu aliyehai anampata na kumzidi kwa yale anayoyafanya katika mambo ya kumtii Mwenyezi Mungu.
Marejeo
صحيح البخاري (8/ 86) (6407).
صحيح مسلم (1/ 539) (779).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، (2/ 982).
شرح رياض الصالحين، لابن عثيمين (5/ 516).
Imepokelewa kutoka kwa Jabiri -radhi za Allah ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Atakayesema: Sub-haanallaahi wabihamdi, (Ametakasika Mwenyezi Mungu Mtukufu na sifa njema ni zake) ataoteshewa mti wa mtende peponi".
Imepokelewa Imamu TirmidhiyDarajaSahihi
Maelezo
Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake yakuwa atakayesema: "Ametakasika Mwenyezi Mungu" ninamtakasa "Mtukufu" kwa dhati yake na sifa zake na vitendo vyake "na sifa njema ni zake" zikiwa zimeambatanishwa na kuegemeza sifa za ukamilifu wake Mtukufu; atasimikiwa na kupandiwa mti wa mtende katika ardhi ya Pepo kwa kila mara atakayosema.
Mafunzo
Himizo la kukithirisha kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu, na miongoni mwake: Ni kufanya tasbihi na tahmidi (kumtukuza na kumsifu).
Pepo ni pana, na kwamba mimea yake ni tasbihi na tahmidi (Kumtuza na kumsifu), na hii ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na neema yake.
Umetajwa mtende pekee katika hadithi pasina miti mingine; kwa sababu ya wingi wa faida zake na uzuri wa matunda yake; na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu amepiga mfano wa muumini na imani yake ndani ya Qur'ani kwa mti huo.
Marejeo
سنن الترمذي (5/ 456) (3464).
مرعاة المفاتيح شرح مشكاة المصابيح، للمباركفوري (7/ 464).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (2/ 985).
مشكاة المصابيح، للتبريزي (2/ 713).
Kutoka kwa Ka'b Bin Ujrah Radhi za Allah ziwe juu yake kutoka kwa Mtume rehema na amani za Allah ziwe juu yake alisema: "Adh-kari za baada ya sala ya faradhi hapati hasara msomaji au mfanyaji wake, kusema Sub-haana llahi mara thelathini na tatu (33), Al-hamdulillahi mara thelethini na tatu (33), Allahu Akbaru mara thelathini na nne (34)".
Imepokelewa Imamu MuslimDarajaSahihi
Maelezo
Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu Adhkari (Dua) hatopata hasara wala kujuta msemaji wake, bali maneno haya yanathawabu, na yanakuja kwa kufuatana, na husemwa baada ya swala za faradhi, nayo ni:
"Sub-haana llaah" -Ametakasika Mwenyezi Mungu- mara thelathini na tatu, yaani ametakasika Mtukufu na kila mapungufu.
"Na Alhamdulillaah" Mara thelathini na tatu, nako ni kumsifu Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu uliotimia pamoja na kumpenda na kumtukuza.
"Allaahu Akbaru" Mara thelathini na nne, Mwenyezi Mungu ni mkubwa mno na ni Mtukufu na Mwenye nguvu kuliko kila kitu.
Mafunzo
Fadhila za kusema Sub-haanallaah, na Alhamdulillaah, na Allaahu Akbar, maneno haya ndio mema yenye kubakia.
Marejeo
صحيح مسلم (1/ 418) (596).
بهجة الناظرين شرح رياض الصالحين، لسليم الهلالي (2/ 501).
نزهة المتقين شرح رياض الصالحين، لمجموعة من الباحثين (2/ 976).
مرقاة المفاتيح شرح مشكاة المصابيح، لعلي القاري (2/ 766).
تيسير العلام، للبسام (ص227).
فيض القدير شرح الجامع الصغير، لزين الدين المناوي (5/ 525).
عن أبي مالكٍ الأشعريِّ رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: «الطُّهُورُ شَطْرُ الْإِيمَانِ، وَالْحَمْدُ لِلهِ تَمْلَأُ الْمِيزَانَ، وَسُبْحَانَ اللهِ وَالْحَمْدُ لِلهِ تَمْلَآنِ -أَوْ تَمْلَأُ- مَا بَيْنَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ، وَالصَّلَاةُ نُورٌ، وَالصَّدَقَةُ بُرْهَانٌ، وَالصَّبْرُ ضِيَاءٌ، وَالْقُرْآنُ حُجَّةٌ لَكَ أَوْ عَلَيْكَ، كُلُّ النَّاسِ يَغْدُو، فَبَايِعٌ نَفْسَهُ فَمُعْتِقُهَا أَوْ مُوبِقُهَا».
Imepokelea kutoka kwa Abii Maalik Al-Ash-ariy Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe ju yake- amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu Rehema na Amani ziwe juu yake: "Twahara ni nusu ya imani, na kusema Al-hamdulillah neno hilo hujaza mizani, na neno Sub-hanallah neno Alhamdulillah maneno hayo mawili hujaza mizani- au hujaza- sehemu iliyopo kati ya Mbingu na Ardhi na Swala ni nuru, na sadaka ni dalili ya imani, na subira ni mwangaza, na Qur'ani ni hoja kwako au hoja dhidi yako, watu wote huamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kutafuta riziki kuna mwenye kuwa na msimamo na kumtii Mwenyezi Mungu, na akawa ni mwenye kuikomboa nafsi yake kutoingia motoni, na miongoni mwao kuna mwenye kuangukia kwenye maasi na akaangamia na kuingia motoni".
Imepokelewa Imamu MuslimDarajaSahihi
Maelezo
Anafahamisha Mtume Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa twahara na usafi wa nje ambao ni udhu na kuoga ni sharti la usahihi wa swala. Na kuwa neno: "Alhamdulillah hujaza mizani" nako ni kumsifu Mwenyezi Mungu aliyetakasika na machafu, na kumsifia kwa sifa za ukamilifu zitakazopimwa siku ya kiyama na kuijaza mizani ya matendo. Na kuwa neno: "Sub-hanallah na Alhamdulillah" na maneno hayo ni kumtakasa Mwenyezi Mungu na kumsifia kwa sifa zilizokamilika na zilizotimia ambazo anastahiki sifa hizo pamoja kumpenda yeye na kumtukuza hujaza sehemu iliyopo kati ya Mbingu na Ardhi. Na kuwa "Swala ni nuru" ya mja katika moyo wake, na katika uso wake na kaburini mwake na siku ya kufufuliwa kwake. Na kuwa "Sadaka ni ushahidi" Na ni dalili ya ukweli wa imani ya muumini, na tofauti yake na mnafiki ambaye huzuia kutoa sadaka kwa kuwa mnafiki haamini malipo ya kutoa sadaka. Na "kuwa subira ni mwangaza" -na subira ni kuizuia nafsi kutoku papatika na kuwa na hasira, subira ni nuru inayokuwa na joto na kuunguza, kama vile mwanga wa Jua; kwa sababu subira ni tabu kubwa inahitaji kuilazimisha nafsi na kuizuia na kile inachokipenda; hivyo haachi kuwa na mng'ao mtu mwenye subira, mwenye kuongoka na mwenye kudumu katika usahihi, nako ni kusubiri katika kumtii Mwenyezi Mungu, na kutomuasi yeye, na kuwa na subira kwenye matatizo na aina mbalimbali za mambo yenye kuchukiza katika Dunia. Na kuwa "Qur'ani ni hoja kwako wewe" kwa kuisoma na kuifanyia kazi, au yaweza kuwa " Hoja dhidi yako" kwa kuiacha pasina kuifanyia kazi au kuisoma. Kisha akafahamisha Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- yakuwa watu wote huenda mbio na hutawanyika na huamka toka usingizini mwao na wanatoka kwenye majumba yao kwa ajili ya kufanya kazi mbalimbali miongoni mwao kuna wenyekuwa na msimamo katika kumtii Mwenyezi Mungu, hivyo anakuwa ameikomboa nafsi yake na moto, na miongoni mwao kuna mwenye kwenda kinyume na kuacha kumtii Mwenyezi Mungu na akaingia katika maasi, hivyo akaiangamiza na kuingia motoni.
Mafunzo
Twahara zipo aina mbili: Twahara ya nje nayo ni udhu na kuoga, na twahara ya ndani inakuwa kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na matendo mazuri.
umuhimu wa kuzihifadhi swala tano, kwakuwa swala tano ni mwangaza kwa mja hapa Duniani na siku ya Kiyama.
Kutoa sadaka ni dalili ya imani ya kweli.
Umuhimu wa kuifanyia kazi Qur'ani na kuisadikisha ili iwe ni hoja kwako au dhidi yako.
Ikiwa nafsi hutoishughulisha na utiifu itakushughulisha na maasi.
Kila mwanadamu lazima afanye matendo, hivyo ima aikomboe nafsi yake kwa kutii, au aiangamize kwa kufanya maasi.
Na subira inahitaji uvumilivu na kutarajia thawabu, na ndani yake kuna uzito.
Marejeo
صحيح مسلم (1/ 203) (223)، شرح الأربعين لابن دقيق العيد (ص 84)، شرح الأربعين النووية للعثيمين (ص: 231)، الرياض الزكية شرح الأربعين النووية للخضير (ص 293)، فتح القوي المتين في شرح الأربعين للعباد (ص 79)
Kila hadithi, daraja, maelezo na funzo hapa vinaonyeshwa kama HadeethEnc.com inavyovichapisha, kwa masharti yake ya kuchapisha upya. Daraja halimtaji aliyelitoa. Tafsiri na maelezo ni ya waandishi wake wenyewe, na baadhi hutaja hukumu; wahakiki wa Sabīl hawajavichunguza. Hadithi ya Kiarabu ndiyo matini. Chanzo: HadeethEnc.com