Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 7 · Aya ya 44

Al-A'raaf 7:44

الأعراف

وَنَادَىٰٓ أَصْحَـٰبُ ٱلْجَنَّةِ أَصْحَـٰبَ ٱلنَّارِ أَن قَدْ وَجَدْنَا مَا وَعَدَنَا رَبُّنَا حَقًّا فَهَلْ وَجَدتُّم مَّا وَعَدَ رَبُّكُمْ حَقًّا ۖ قَالُوا۟ نَعَمْ ۚ فَأَذَّنَ مُؤَذِّنٌۢ بَيْنَهُمْ أَن لَّعْنَةُ ٱللَّهِ عَلَى ٱلظَّـٰلِمِينَ

Maana

Na watu wa Bustanini watawanadi watu wa Motoni, "Sisi tumeshakuta yale aliyotuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Na je, nyinyi pia mmekuta yale aliyowaahidi Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli?" Watasema: "Ndiyo!" Basi mtangazaji atatangaza kati yao kwamba, "Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu."

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi tumekuta aliyo tuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta aliyo kuahidini Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia: Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu, [44]

[44] Watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni kwa kuwaambia: Sisi tumekwisha ona thawabu alizo tuahidi Mola Mlezi wetu kuwa ni kweli. Je, nyinyi hiyo adhabu aliyo kuahidini Mola Mlezi wenu mmeiona kuwa ni kweli? Nao watajibu: Naam, Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia watu wa Peponi na watu wa Motoni: Laana, yaani kunyimwa na kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu, ndio malipo ya wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na upotovu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Watu wa Peponi, baada ya kuingia humo, watawaita watu wa Motoni wawaambie, «Sisi tumeshapata kuwa ni kweli tuliyoahidiwa na Mola wetu, kupitia ndimi za Mitume Wake, kuhusu kuwalipa wanaomtii. Je, nyinyi mumeyapata mliyoahidiwa na Mola wenu, kupitia ndimi za Mitume Wake, kuwa ni kweli kuhusu kuwaadhibu wanaomuasi?» Hapo watu wa Motoni watawajibu watu wa Peponi wakiwaambia, «Ndio, kwa kweli tumeyapata yale Aliyotuahidi Mola wetu kuwa ni kweli.» Hapo Atatangaza mwenye kutangaza, akiwa kati baina ya watu wa Peponi na watu wa Motoni akisema, «Laana ya Allah Mtukufu iwashukie watu madhalimu» ambao walikiuka mipaka ya Allah Mtukufu na wakamkanusha Allah Mtukufu na Mtume Wake.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-A'raaf

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net