Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 65 · Aya ya 1

At-Talaaq 65:1

الطلاق

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلنَّبِىُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ ٱلنِّسَآءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا۟ ٱلْعِدَّةَ ۖ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ رَبَّكُمْ ۖ لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِنۢ بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّآ أَن يَأْتِينَ بِفَـٰحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ ۚ وَتِلْكَ حُدُودُ ٱللَّهِ ۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ ٱللَّهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُۥ ۚ لَا تَدْرِى لَعَلَّ ٱللَّهَ يُحْدِثُ بَعْدَ ذَٰلِكَ أَمْرًا

Maana

Ewe Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wanaoweza kuanza eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi hakika amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Mwenyezi Mungu ataleta jambo jingine baada ya haya.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Ewe Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya. [1]

[1] Ewe Nabii! Mkitaka kuwapa talaka wanawake, basi wapeni talaka kwa kukabiliana na eda zao, (yaani wakati wa tahara kabla ya kuwaingilia), na idhibitini eda, na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe watalaka katika nyumba zao walimo pewa talaka. Wasitoke humo ila ikiwa wamefanya kitendo kichafu wazi. Hukumu hizo zilizo tangulia ni alama za Mwenyezi Mungu amezifanya ni sharia kwa waja wake. Na Mwenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui pengine Mwenyezi Mungu labda ataleta jambo usilo litaraji baada ya talaka hiyo, na wakapendana.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Ewe Mtume! Pindi mnapotaka, (wewe na Waumini), kuwapa talaka wake zenu, basi wapeni talaka wakiwa kwenye hali ya kukabili kipindi cha kukaa eda- (yaani kwenye hali ya usafi ambao hakukupatikana kuingiliwa), au katika hali ya mimba iliyodhahiri- na mshike hesabu ya eda, mpate kujua muda wa kuwarejea iwapo mtataka kuwarejea, na muogopeni Allah Mtukufu, Mola wenu. Wala msiwatoe wanawake waliopewa talaka kwenye majumba wanayokaa mpaka eda zao zimalizike, nazo ni hedhi tatu kwa asiyekuwa mdogo ambaye hajaanza kutokwa na damu na kwa aliyekatika damu kwa uzee na kwa mwenye mimba. Na haifai kwa wanawake hao kutoka majumbani mwao wenyewe isipokuwa watakapofanya kitendo kiovu cha wazi kama vile uzinifu. Na hizo ndizo hukumu za Allah Mtukufu alizozipitisha kwa waja Wake. Na Mwenye kuzikiuka hukumu za Allah Mtukufu, basi huyo amejidhulimu nafsi yake na ameipeleka mahali pa maangamivu. Hujui, (ewe mtoaji talaka), kwamba Allah Mtukufu huenda, baada ya talaka hiyo, Akaleta jambo usilolitazamia ukaja ukamrudia.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

At-Talaaq

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net