Ruka hadi kwenye maudhui
Tafsir As-Saadi - Swahili · At-Talaaq
Sura ya 65

At-Talaaq

Hii ni tarjama ya tafsiri ya as-Saʿdī kama IslamHouse.com inavyoichapisha katika saadi.islamenc.com, iliyosomwa kutoka kurasa za tovuti hiyo. Tovuti haisemi ni nani aliyeitafsiri kwa lugha nyingine wala inafuata toleo gani lililochapishwa, na haitaji masharti ya kuchukua matini yake, kwa hiyo haki ya kuionyesha haijathibitishwa. Hakuna aliyeilinganisha na kitabu kilichochapishwa, na hakuna mwanazuoni aliyeihakiki. Kila kifungu kipo kando ya aya inazozifafanua, ambazo ni matini ya Qur’ani ya Tanzil, inavyoonekana huko; aya ambayo tovuti haitoi ufafanuzi wake yenyewe inakaa pamoja na kifungu kilichotangulia, na faharasa inataja kila aya ya aina hiyo. Sabīl haikuandika wala kutafsiri kwa lugha nyingine chochote kati yake.

Maandishi kutokasaadi.islamenc.comIslamHouse.comnone stated (the site names no licence and no terms for taking its text)ilichukuliwa 2026-10-22

Aya ya 1

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلنَّبِىُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ ٱلنِّسَآءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا۟ ٱلْعِدَّةَ ۖ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ رَبَّكُمْ ۖ لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِنۢ بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّآ أَن يَأْتِينَ بِفَـٰحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ ۚ وَتِلْكَ حُدُودُ ٱللَّهِ ۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ ٱللَّهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُۥ ۚ لَا تَدْرِى لَعَلَّ ٱللَّهَ يُحْدِثُ بَعْدَ ذَٰلِكَ أَمْرًا 1

{1} Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema, akimwambia Nabii wake [Muhammad] - rehema na amani na Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - na akiwaambia Waumini pia: "Ewe Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake." Yaani, mnapotaka kuwapa talaka, basi itafuteni talaka hiyo jambo linalokubaliwa kisheria, wala msifanye haraka kutoa talaka wakati sababu yake inapatikana bila ya kuangalia amri ya Mwenyezi Mungu. Bali "wapeni talaka katika wakati wa eda zao." Yaani, ampe talaka hali ya kuwa mke huyo yu safi, na kwamba hakuwa ameingiliana naye katika hali yake ya usafi hiyo. Hii ndiyo talaka ambayo eda yake huwa wazi kabisa. Tofauti na ikiwa atamtaliki akiwa katika hedhi. Hedhi hiyo haitahesabiwa ambayo alimtaliki ndani yake, na hilo litamsababishia eda kuwa ndefu. Vile vile ikiwa atamlatiki hali ya kuwa yu safi lakini aliingiliana naye. Hapo hatakuwa salama kutokana na ujauzito, na wala haitakuwa wazi ni eda ipi atakaa. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu aliamrisha uhesabiwe muda wa eda; kwa kuhesabu hedhi ikiwa ni katika wale wanaopata hedhi, au kuhesabu miezi ikiwa si katika wale wanaopata hedhi na wala hana mimba. Kwa maana katika kuihesabu kuna kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu, haki ya mume aliyepeana talaka, haki ya yule atakayemuoa baadaye, na haki yake mke huyu ya kupewa matunzo na mengineyo. Kwa hivyo, muda wake wa eda utadhibitiwa vyema, itajulikana hali yake vizuri zaidi, na zitajulikana haki zinazoambatana nayo na kile ambacho ni chake ndani yake. Amri hii ya kuhesabu eda anaambiwa mume na mke ikiwa ni katika wanawake wanaojukumishwa na sheria. Vinginevyo, basi anaambiwa mlezi wake. Na kauli yake: "Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi." Yaani, katika mambo yenu yote, na mhofuni katika mambo ya wake waliopewa talaka. “Msiwatoe katika nyumba zao" katika muda wa eda. Bali anapaswa kukaa katika nyumba ambayo mume wake alimtaliki akiwa ndani yake. "Wala wasitoke wenyewe" ama katazo la kuwatoa, ni kwa sababu kuwapa nyumba ni wajibu wa mume kwa mke ili akamilishe eda yake, ambayo ni moja ya haki zake. Na ama katazo kutoka mwenyewe, ni kwa sababu katika kutoka kwake kuna kupoteza haki ya mume na kutoilinda, na katazo hili la kutomtoa na kutoka kwake katika nyumba litaendelea hadi kukamilika kwa muda wa eda. "Ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi" unaohitaji watolewe, kwa manaa unawasababishia watu wa nyumba hiyo madhara ikiwa hatatoka; kama vile madhara kwa maneno na vitendo vichafu. Basi katika hali hii, inaruhusiwa kwa waume kuwatoa. Kwa sababu yeye mwenyewe ndiye aliyejisababishia kutolewa. Na kukalishwa nyumbani alikokuwa amekalishwa kulikuwa kwa sababu ya kumfurahisha mawazo yake na kumfanyia upole. Haya ni kuhusiana na mwanamke aliyetalikiwa talaka ya kurudiana bila ya kufunga nikaa mpya. Ama yule aliyetalikiwa talaka ya kurudiana kwa nikaa mpya, huyo hailazimu kupewa mahali pa kukaa, kwa kwa sababu makazi yatafuatana na kupewa matumizi ya kila siku. Na matumizi ya kila siku ni lazima apewe mwanamke aliyetalikiwa talaka isiyohitaji nikaa mpya ili kurudiana si ile anayohitaji nikaa mpya. "Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu" ambayo aliwawekea waja wake na akawawekea hiyo kuwa sheria na akawaamrisha kushikamana nayo na kusimamia hapo, "Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu" kwa kutosimamia hapo, bali aliikiuka au aliipuuza sana, "basi hakika amejidhulumu nafsi yake" haki yake, na akapoteza fungu lake katika kufuata mipaka ya Mwenyezi Mungu, ambayo ni ndiyo sababu ya kutengenea katika dunia na akhera. "Hujui; labda Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya." Yaani, Mwenyezi Mungu ameweka sheria ya eda na akaiweka kuanza baada ya talaka kwa sababu ya hekima mbalimbali kubwa. Miongoni mwake ni kwamba huenda Mwenyezi Mungu akaleta rehema na mapenzi katika moyo wa aliyetoa talaka, kwa hivyo akamrudisha yule aliyempa talaka, kisha wakaendelea kuishi vyema. Na hilo linawezekana katika kipindi cha eda. Au huenda alimpa talaka kutokana na sababu aliyoisababisha mke huyo, kisha ikaisha katika muda wa eda, kwa hivyo, wakarudiana kwa sababu ya kutokuwepo sababu ya talaka ile. Na miongoni mwa hekima ni kwamba muda wa eda utupu wa tumbo lake kutokana na ujauzito wa mumewe.