Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 6 · Aya ya 1

Al-An'aam 6:1

الأنعام

ٱلْحَمْدُ لِلَّهِ ٱلَّذِى خَلَقَ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضَ وَجَعَلَ ٱلظُّلُمَـٰتِ وَٱلنُّورَ ۖ ثُمَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ

Maana

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye aliumba mbingu na ardhi, na akafanya giza mbalimbali na nuru. Kisha wale waliokufuru wanawafanya wengine kuwa sawa na Mola wao Mlezi.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya wengine sawa na Mola wao Mlezi. [1]

[1] Kuhimidiwa, yaani kusifiwa na kutajwa kwa wema, ni kwa Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi, na akaumba, kwa kudra yake, giza na mwangaza, kwa manufaa ya waja wake, na kuambatana na hikima yake. Tena pamoja na neema zote hizi nzuri hawa makafiri wanakwenda mshirikisha Mwenyezi Mungu, na wakawafanya wengineo ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada!! Aya hii tukufu ni ishara ya ubora wa kuumba, na ubora wa kuumba unaonyesha Umoja na Upweke wa Mwenye kuumba na utukufu wake. Kwani mbingu na nyota zake, na sayari zake, na jua, na mwezi - vyote hivyo ni ushahidi wa Umoja wake. Na ardhi na viliomo ndani yake, navyo ni wanyama, mimea na visio na uhai, na milima na mabonde, na rutuba na ukame, na viliomo chini ya ardhi maadeni magumu na yanayo tiririka, na bahari na viliomo ndani yake kama lulu na vilio hai - vyote hivyo vinaonyesha Umoja wa Mwenye kuumba. Na giza la kila namna, kama giza la jabali, na bahari, na mapango, na ukungu ulio funga moja kwa moja hata mtu akiutoa mkono wake anakaribia kuwa asiouone - pia vyote hivyo vinaonyesha ujuzi usio kuwa na mfano, wa kuanzisha kuumba, wa Mwenyezi Mungu Aliye viumba. Hali kadhaalika nuru, na sababu zake mbali mbali, kama nuru ya jua, na mwangaza wa mwezi, na mwangaza wa nyota ... vyote hivyo vinaonyesha uanzishaji wa Mwenyezi Mungu wa kuumba bila ya kiigizo.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Sifa njema zote ni za Allah Mtukufu, Mwenye sifa ambazo zote ni sifa za ukamilifu, Mwenye neema za nje na za ndani, za kidini na za kidunia, Ambaye Aliumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, Aliumba giza na mwangaza kwa kupishana usiku na mchana. Katika hili pana ishara ya utukufu wa Allah Mtukufu, (Aliyetukuka) na kuwa Yeye Peke Yake Anastahiki kuabudiwa. Haifai kwa yoyote kumshirikisha mwengine na Yeye. Na pamoja na uwazi huu, makafiri wanamfanya sawa mwingine na Allah Mtukufu na wanamshirikisha na Yeye.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-An'aam

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net