Al-Maaida 5:32
المائدةمِنْ أَجْلِ ذَٰلِكَ كَتَبْنَا عَلَىٰ بَنِىٓ إِسْرَٰٓءِيلَ أَنَّهُۥ مَن قَتَلَ نَفْسًۢا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِى ٱلْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ ٱلنَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَآ أَحْيَا ٱلنَّاسَ جَمِيعًا ۚ وَلَقَدْ جَآءَتْهُمْ رُسُلُنَا بِٱلْبَيِّنَـٰتِ ثُمَّ إِنَّ كَثِيرًا مِّنْهُم بَعْدَ ذَٰلِكَ فِى ٱلْأَرْضِ لَمُسْرِفُونَ
Kwa sababu ya hayo, tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba mwenye kuiua nafsi bila ya nafsi hiyo kuiua nyingine, au kufanya uharibifu katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kuiweka hai, basi ni kama amewaweka hai watu wote. Na hakika walikwishawajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha hakika wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi. [32]
[32] Kwa sababu ya uasi huo na kupenda kwa baadhi ya watu kuwafanyia uadui wenginewe, ndio tukawajibisha kumuuwa muuwaji, kwani mwenye kumuuwa mtu bila ya sababu zinazo pasa kisasi, au bila ya kufanya uharibifu katika nchi, ni kama amewauwa watu wote. Yeye huyo amemwaga damu za watu, na amewashajiisha wengine wafanye kama hayo. Kwa hivyo kumuuwa mmoja ni kama kuwauwa watu wote kwa kujiletea maudhiko ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Na mwenye kumhuisha mtu kwa kumlipia kisasi, basi ni kama amewahuisha watu wote kwa kuhifadhi damu ya wanaadamu isimwagwe ovyo. Huyo anastahiki thawabu nyingi kutokana na Mola wake Mlezi. Sisi tumewatumia Mitume wetu kutilia mkazo hukumu yetu kwa dalili na hoja. Kisha baadaye wengi miongoni mwa Wana wa Israili walipindukia mipaka katika uharibifu wao katika nchi. Maneno haya yanaonyesha kuwa kumfanyia uadui mtu mmoja ni kuwafanyia jamii ya watu, na kulipa kisasi ndio kuhuisha jamii. Katika Sharia ya Kiislamu kisasi ni haki ya waliy-amri, yaani aliye mkhusu maiti. Akipenda atasamehe achukue fidiya, na akipenda atataka kisasi na akitimize. Naye anapo samehe anayo haki ya kumfedhehesha mkosefu akiwa amekithiri uwovu wake na uharibifu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Kwa sababu ya uhalifu huu wa mauaji, tuliwaekea sheria Wana wa Isrãîl kwamba yoyote mwenye kumuua mtu pasi na sababu ya kulipiza kisasi au ya uharibifu katika ardhi, kwa aina yoyote kati ya aina za uharibifu zinazopelekea mauaji, kama ushirikina na uharamia, atakuwa ni kama kwamba amewaua watu wote kwa jinsi atakavyostahili mateso makubwa kutoka kwa Allah Mtukufu, na kwamba yule atakayejizuia asiue mtu ambaye Allah Mtukufu Ameharamisha kuuawa, ni kama kwamba amewahuisha watu wote. Hivyo basi, kulinda heshima ya binadamu mmoja ni kulinda heshima ya binadamu wote. Hakika Mitume wetu waliwajia Wana wa Isrãîl kwa hoja na dalili juu ya usawa wa yale waliyowalingania kwayo ya kumuamini Mola wao na kuyatekeleza yale yaliyofanywa wajibu kwao na Mola wao. Kisha, wengi kati yao, baada ya kujiwa na Mitume ni wenye kupita mipaka ya Allah Mtukufu kwa kuyafanya yaliyoharamishwa na Allah Mtukufu na kuyaacha maamrisho yake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net