Al-Maaida 5:13
المائدةفَبِمَا نَقْضِهِم مِّيثَـٰقَهُمْ لَعَنَّـٰهُمْ وَجَعَلْنَا قُلُوبَهُمْ قَـٰسِيَةً ۖ يُحَرِّفُونَ ٱلْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِۦ ۙ وَنَسُوا۟ حَظًّا مِّمَّا ذُكِّرُوا۟ بِهِۦ ۚ وَلَا تَزَالُ تَطَّلِعُ عَلَىٰ خَآئِنَةٍ مِّنْهُمْ إِلَّا قَلِيلًا مِّنْهُمْ ۖ فَٱعْفُ عَنْهُمْ وَٱصْفَحْ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلْمُحْسِنِينَ
Basi kwa sababu ya kuvunja kwao agano lao, tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahali pake, na walisahau sehemu katika yale waliyokumbushwa kwayo. Na huachi kutambua hiyana kutoka kwao, isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na uwaache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala pake, na wamesahau sehemu ya yale waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua khiana kutokana nao, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema. [13]
[13] Basi kwa sababu ya Wana wa Israili kuvunja agano lao ndio wakastahiki kufukuzwa kutokana na rehema ya Mwenyezi Mungu. Nyoyo zao zikawa ngumu, si laini za kupokea Haki; na wakaingia kupotoa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyomo katika Taurati kutokana na maana yake ya asli, na yafuate yanayo wafikiana na wapendavyo wao. Wakaachilia mbali pande kubwa ya mambo waliyo amrishwa katika Taurati !! Na wewe, Mtume, huachi kuona kila namna ya khadaa na uvunjaji wa ahadi kwa hawa Wana wa Israili, isipo kuwa kwa wachache tu miongoni mwao ambao wanakuamini wewe. Hao hawakhuni wala hawadanganyi. Basi, ewe Mtume! Yasamehe yaliyo pita kutokana na watu hawa, na wachilia mbali, bali wafanyie wema. Kwani Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Kwa sababu ya hawa Mayahudi kuvunja ahadi zao zilizotiliwa mkazo, tuliwafukuza kutoka kwenye rehama yetu na tukazijaalia nyoyo zao kuwa ngumu, hazilainiki kwa Imani, wanayageuza maneno ya Allah Mtukufu ambayo Alimteremshia Mûsã, nayo ni Taurati, na wakaacha kuitumia sehemu ya yale waliyokumbushwa nayo. Na utaendelea, ewe Mtume, kupata kutoka kwa Mayahudi uhaini na uvunjaji ahadi, kwani wao wako kwenye njia ya mababu zao, isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi samehe kwa mabaya wanayokutendea na usiwe na chuki juu yao. Hakika Allah Mtukufu Anampenda anayefanya uzuri wa kusamehe na kutokuwa na chuki kwa aliyemfanyia ubaya.(Hivi ndivyo vile watu wapotovu wanapata njia ya kufikia malengo yao mabaya kwa kuyapotoa maneno ya Allah Mtukufu na kuyapa maana ambayo siyo yake. Wakishindwa kupotoa na kugeuza maana, wanayaacha yale yasioafikiana na matamanio yao katika sheria ya Allah Mtukufu ambayo hawatathibiti juu yake isipokuwa wachache waliyohifadhiwa na Allah Mtukufu kati yao).
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net