Al-Maaida 5:12
المائدةوَلَقَدْ أَخَذَ ٱللَّهُ مِيثَـٰقَ بَنِىٓ إِسْرَٰٓءِيلَ وَبَعَثْنَا مِنْهُمُ ٱثْنَىْ عَشَرَ نَقِيبًا ۖ وَقَالَ ٱللَّهُ إِنِّى مَعَكُمْ ۖ لَئِنْ أَقَمْتُمُ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتَيْتُمُ ٱلزَّكَوٰةَ وَءَامَنتُم بِرُسُلِى وَعَزَّرْتُمُوهُمْ وَأَقْرَضْتُمُ ٱللَّهَ قَرْضًا حَسَنًا لَّأُكَفِّرَنَّ عَنكُمْ سَيِّـَٔاتِكُمْ وَلَأُدْخِلَنَّكُمْ جَنَّـٰتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ ۚ فَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ مِنكُمْ فَقَدْ ضَلَّ سَوَآءَ ٱلسَّبِيلِ
Na hakika Mwenyezi Mungu alichukua agano la Wana wa Israili. Na tukawatumia kutokana nao wakuu kumi na wawili. Na Mwenyezi Mungu akasema: 'Kwa yakini Mimi niko pamoja nanyi. Mkisimamisha Swala, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, hakuna shaka nitawafutia mabaya yenu na nitawaingiza katika mabustani yapitayo mito chini yake. Kwa hivyo mwenye kukufuru miongoni mwenu baada ya hayo, basi bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa.'
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na Mwenyezi Mungu alifanya agano na Wana wa Israili. Na tukawateulia kutokana nao wakuu kumi na mbili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa yakini Mimi ni pamoja nanyi. Mkisali, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, hapana shaka nitakufutieni maovu yenu na nitakuingizeni katika mabustani yapitayo mito kati yake. Lakini atakaye kufuru miongoni mwenu baada ya hayo bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa. [12]
[12] Mwenyezi Mungu alichukua ahadi kutokana na Wana wa Israili kuwa watamsikia na watamt'ii. Akawateulia marais thinaashara (kumi na mbili) kutokana miongoni mwao ili itimie hiyo ahadi. Na Yeye Mwenyezi Mungu akawaahidi ahadi ya nguvu kuwa atakuwa pamoja nao, atawasaidia na atawanusuru ikiwa watashika Swala kama ipasavyo, na watatoa Zaka walizo faridhiwa, na watawasadiki Mitume wake wote, na watawanusuru, na watatoa mali kwa ajili ya mambo ya kheri. Na kwamba pindi wakifanya hayo basi Mwenyezi Mungu atawafutia dhambi zao, na atawatia katika Bustani zake zipitazo mito kati yake. Na mwenye kukufuru, na akavunja ahadi baada ya hayo, basi huyo amepotoka na hakufuata njia iliyo kaa sawa iliyo nyooka.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na kwa hakika Allah Mtukufu Alichukua kwa Wana wa Isrãîl ahadi ya mkazo kwamba wamtakasiye ibada Yeye Peke Yeke. Na Allah Mtukufu Alimuamrisha Mûsã awawekee wao viongozi kumi na mbili kulingana na idadi ya koo zao, wachukue kwao ahadi ya mkazo ya kumsikiliza na kumtii Allah Mtukufu na Mtume Wake na kukifuata Kitabu Chake. Na Allah Mtukufu Aliwaambia Wana wa Isrãîl, «Mimi niko pamoja nanyi kwa hifadhi yangu na nusura yangu Iwapo mtasimamisha Swala na mtawapa Zaka za faradhi wanaostahiki kupewa na mtawaamini Mitume wangu katika yale wanayoyatolea habari, mtawanusuru na mtatoa katika njia yangu, hakika nitawafutia makosa yenu na nitawaingiza ndani ya mabustani ya Peponi ambayo mito inapita chini ya majumba yake ya fahari.Basi mwenye kuikana ahadi hii, kati yenu, hakika amejiepusha na njia ya haki na kuifuata njia ya upotevu».
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net