An-Nisaa 4:77
النساءأَلَمْ تَرَ إِلَى ٱلَّذِينَ قِيلَ لَهُمْ كُفُّوٓا۟ أَيْدِيَكُمْ وَأَقِيمُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ وَءَاتُوا۟ ٱلزَّكَوٰةَ فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ ٱلْقِتَالُ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَخْشَوْنَ ٱلنَّاسَ كَخَشْيَةِ ٱللَّهِ أَوْ أَشَدَّ خَشْيَةً ۚ وَقَالُوا۟ رَبَّنَا لِمَ كَتَبْتَ عَلَيْنَا ٱلْقِتَالَ لَوْلَآ أَخَّرْتَنَآ إِلَىٰٓ أَجَلٍ قَرِيبٍ ۗ قُلْ مَتَـٰعُ ٱلدُّنْيَا قَلِيلٌ وَٱلْـَٔاخِرَةُ خَيْرٌ لِّمَنِ ٱتَّقَىٰ وَلَا تُظْلَمُونَ فَتِيلًا
Je, hukuwaona wale walioambiwa: ‘Izuieni mikono yenu, na mshike Swala na mtoe Zaka.’ Na pindi walipoamrishwa kupigana, mara kundi moja miongoni mwao likawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa hofu kubwa zaidi. Na wakasema: ‘Mola wetu Mlezi! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti ungetuahirishia kiasi ya muda kidogo hivi!’ Sema: ‘Starehe ya dunia ni ndogo, na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kucha Mungu. Wala hamtadhulumiwa hata kijiuzi kilicho ndani ya uwazi wa kokwa ya tende.’
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Je, huwaoni wale walio ambiwa: Izuieni mikono yenu, na mshike Swala na mtoe Zaka. Na walipo amrishwa kupigana, mara kundi moja kati yao liliwaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa khofu kubwa zaidi. Na wakasema: Mola Mlezi wetu! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti unge tuakhirishia kiasi ya muda kidogo hivi! Sema: Starehe ya dunia ni ndogo, na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamngu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa kokwa ya tende. [77]
[77] Ewe Muhammad! Hebu huwaangalii ukawastaajabia wale walio taka kupigana kabla ya kuja ruhusa, wakaambiwa: Bado haujafika wakati wa vita. Basi izuieni mikono yenu msipigane. Bali shughulikieni kushika Swala, na kutoa Zaka. Na Mwenyezi Mungu alipo waamrisha wapigane kikawa kikundi kimoja kati yao kikawa kinawaogopa watu kama kumkhofu Mwenyezi Mungu, au zaidi. Wakasema kwa kuona ni mageni hayo: Kwa nini ukatuamrisha kupigana? Wao walidhani kuwa kuamrishwa vita kunahimiza ajali yao, na kwa hivyo wakasema: Hebu lau ungeli tungojea muda kidogo tupate kustarehe na ulimwengu! Waambie: Songeni mbele mkapigane hata ikiwa mtakufa mashahidi, kwani starehe ya dunia, ingawa ni kubwa vipi, ni chache ukilinganisha na starehe ya Akhera. Na Akhera ni bora na kubwa zaidi kwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, na huko mtakuja lipwa kwa vitendo vyenu vya duniani, wala hampunguziwi hata chembe katika ujira wenu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya wale walioambiwa, kabla ya kuruhusiwa kupigana jihadi, «Izuieni mikono yenu kupigana na maadui wenu washirikina. Na jilazimisheni kutekeleza yale mliyofaradhiwa ya Swala na Zaka»? Na Allah Mtukufu Alipowafaradhia kupigana, kulitokea kundi la watu katika wao iliobadilika hali yao wakawa wana hofu ya kuwaogopa watu kama vile wanavyomuogopa Allah Mtukufu au zaidi na wakawa wanaidhihirisha hofu kubwa iliyowaingia na kusema, «Ewe Mola wetu, kwa nini ulitufaradhia kupigana? Lau wewe ungetupa muhula mpaka muda mchache.» Wakitumai kupata starehe ya maisha ya ulimwengu. Waambie, ewe Mtume, Starehe ya ulimwengu ni chache, na Akhera na yaliyomo ndani ni makubwa zaidi na ni yenye kusalia zaidi kwa mwenye kuwa na uchamungu, akafanya alioamrishwa na akajiepusha na aliokatazwa. Na Mola wako Hatamdhulumu yoyote, hata kama ni kadiri ya uzi unaokuwako kwenye mwanya wa koko ya tende.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net