Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 4 · Aya ya 78

An-Nisaa 4:78

النساء

أَيْنَمَا تَكُونُوا۟ يُدْرِككُّمُ ٱلْمَوْتُ وَلَوْ كُنتُمْ فِى بُرُوجٍ مُّشَيَّدَةٍ ۗ وَإِن تُصِبْهُمْ حَسَنَةٌ يَقُولُوا۟ هَـٰذِهِۦ مِنْ عِندِ ٱللَّهِ ۖ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَقُولُوا۟ هَـٰذِهِۦ مِنْ عِندِكَ ۚ قُلْ كُلٌّ مِّنْ عِندِ ٱللَّهِ ۖ فَمَالِ هَـٰٓؤُلَآءِ ٱلْقَوْمِ لَا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ حَدِيثًا

Maana

Popote mtakapokuwa, mauti yatawafikia, hata kama mtakuwa katika ngome zilizoimarishwa. Na likiwapata zuri, wanasema: Hili limetoka kwa Mwenyezi Mungu. Na likiwapata ovu, wanasema: Hili limetoka kwako wewe. Sema: Yote hayo yanatokana na Mwenyezi Mungu. Basi wana nini watu hawa hata hawakaribii kufahamu maneno?

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Popote mlipo mauti yatakufikieni, na hata mkiwa katika ngome zilizo na nguvu. Na likiwafikilia jema wanasema: Hili limetoka kwa Mwenyezi Mungu. Na likiwafikilia ovu wanasema: Hili limetoka kwako wewe. Sema: Yote yanatokana na Mwenyezi Mungu. Basi wana nini watu hawa hata hawakaribii kufahamu maneno? [78]

[78] Hakika hayo mauti mnayo yakimbia yatakukuteni popote pale mlipo, na hata mkikaa ndani ya ngome zilizo jengwa madhubuti imara. Na hao wenye imani legevu na dhaifu husema pindi wapatapo ushindi na ngawira: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na pindi wapatapo lawama au kushindwa wao hukwambia wewe: Ewe Muhammad! Haya yanatokana na wewe. Haya si lolote ila kukufanya kuwa wewe ni mkorofi, na kukutupia lawama wewe badala ya nafsi zao. Basi waambie: Kila linalo kupateni, mnalo lipenda na mnalo lichukia, linatokana na kudra ya Mwenyezi Mungu, na linatokana na majaribio yake na mitihani yake. Wana nini watu hawa madhaifu hata hawajakaribia kujua usawa wa maneno wanayo ambiwa?

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Popote mliopo mtafikiwa na kifo, pawe ni mahali popote pale mnapokuwa, muda wenu ukikoma, hata kama mupo ndani ya ngome zilizoimarishwa zilizoko mbali na kiwanja cha mapambano na mapigano. Na wakipatikana na mambo ya kuwafurahisha ya starehe ya maisha haya (ya ulimwenguni), wanayanasibisha kwa Allah Mtukufu kuwa Ndiye Aliyewapatia, na watokewapo na matukio wanayoyachukia, wanayanasibisha kwa Mtume Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, kuwa yamesababishwa na yeye kwa ujinga wao na kwa fikira zao kuwa yeye amewaletea nuksi. Na hawakujua kwamba yote yanatoka kwa Allah Mtukufu Peke Yake, kwa uamuzi Wake na makadirio Yake. Basi kwa nini wao hawakaribii kuelewa maneno yoyote unayowaelezea?

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

An-Nisaa

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net