Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 253

Al-Baqara 2:253

البقرة

تِلْكَ ٱلرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۘ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ ٱللَّهُ ۖ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَـٰتٍ ۚ وَءَاتَيْنَا عِيسَى ٱبْنَ مَرْيَمَ ٱلْبَيِّنَـٰتِ وَأَيَّدْنَـٰهُ بِرُوحِ ٱلْقُدُسِ ۗ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ مَا ٱقْتَتَلَ ٱلَّذِينَ مِنۢ بَعْدِهِم مِّنۢ بَعْدِ مَا جَآءَتْهُمُ ٱلْبَيِّنَـٰتُ وَلَـٰكِنِ ٱخْتَلَفُوا۟ فَمِنْهُم مَّنْ ءَامَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ مَا ٱقْتَتَلُوا۟ وَلَـٰكِنَّ ٱللَّهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

Maana

Mitume hao tumewaboresha baadhi yao juu ya wengineo. Miongoni mwao kuna wale ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na akawapandisha vyeo baadhi yao. Na tukampa Isa mwana wa Maryam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Mtakatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelipigana wale waliokuwa baada yao, baada ya kujiwa na hoja zilizo wazi. Lakini walihitilafiana. Basi miongoni mwao kuna wale walioamini, na miongoni mwao kuna wale waliokufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelitaka, wasingelipigana. Lakini Mwenyezi Mungu hufanya kile akitakacho.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo. [253]

[253] Hao ni Mitume ambao baadhi yao tumewataja, wengine tumewatukuza kuliko wenginewe. Wamo kati yao walio semezwa na Mwenyezi Mungu ana kwa ana, kama Musa. Na wengine kati yao Mwenyezi Mungu amewanyanyua kushinda vyeo vya wote, kama Muhammad ambaye akamkhusisha kumpa Ujumbe kwa ulimwengu wote, na kukamilisha Sharia, na kuwa ni Mtume wa mwisho. Na miongoni mwao ni Isa bin Maryam, ambaye Mwenyezi Mungu alimtia nguvu kwa kumpa miujiza kama kufufua wafu, na kuponyesha upofu na ukoma, na akamletea Jibril, Roho Mtakatifu, ili kumtia nguvu. Na Mitume hawa wameleta Uwongofu, na Dini ya Haki, na Ushahidi ulio wazi wenye kuongoa. Kwa haya imewajibikia watu wote wawaamini, wala wasikhitalifiane, wala wasipigane. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasipigane hao watu baada ya kuletewa Mitume na ishara zilizo wazi zenye kuonyesha Haki, pasingetokea kupigana wala kukhitalifiana. Lakini Mwenyezi Mungu hakutaka hayo. Kwa hivyo wakakhitalifiana. Basi kati yao wakawapo walio amini, na wengine walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli uwana wala wasingeli khitalifiana. Bali wangeli kuwa wote katika Haki. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda apendalo.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Mitume hawa watukufu, Allah Mtukufu Amewatukuza baadhi yao juu ya wengine, kulingana na neema za Allah Mtukufu juu yao. Miongoni mwao kuna ambao Allah Mtukufu Amesema nao, kama Mûsã na Muhammad, rehema na amani ziwashukie. Katika hili pana kuthibitisha sifa ya kusema kwa Allah Mtukufu, Aliyeshinda na kutukuka, kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake. Na miongoni mwao kuna ambao Allah Mtukufu Aliwainua daraja nyingi za juu, kama Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie, kwa kuenea ujumbe wake, kutia kikomo cha unabii kwake, kwa kuwatukuza ummah wake juu ya ummah wengine na yasiyokuwa hayo. Na Allah Mtukufu Alimpa ‘Ǐsâ mwana wa Maryam, amani imshukie, hoja zilizo wazi, ambazo ni miujiza yenye kushinda, kama kumponya aliyezaliwa kipofu, kwa idhini ya Allah Mtukufu, na kumponya mwenye barasi, kwa idhini ya Allah Mtukufu, na kama kuhuisha kwake waliokufa kwa idhini ya Allah Mtukufu. Na Allah Mtukufu Alimpa nguvu kwa Jibrili, amani imshukie. Na lau Allah Mtukufu angetaka wasipigane hao waliokuja baada ya hawa Mitume, baada ya kuwafunukia wao hoja zilizo wazi, hawangalipigana. Lakini ilitokea tafauti baina yao: katika wao kuna aliyejikita kwenye Imani yake, na katika wao kuna aliyeshikilia kukanusha. Na lau Allah Mtukufu angetaka, baada ya hizo tafauti zilizotokea zilizopelekea kupigana, hawangalipigana, lakini Allah Mtukufu Anampa taufik ya kumtii Yeye na kumuamini Anayemtaka, na Anamuondolea taufiki Yake Anayemtaka akamuasi na kumkanusha, Kwani Yeye Anafanya na kuchagua Analolitaka.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net