Al-Baqara 2:246
البقرةأَلَمْ تَرَ إِلَى ٱلْمَلَإِ مِنۢ بَنِىٓ إِسْرَٰٓءِيلَ مِنۢ بَعْدِ مُوسَىٰٓ إِذْ قَالُوا۟ لِنَبِىٍّ لَّهُمُ ٱبْعَثْ لَنَا مَلِكًا نُّقَـٰتِلْ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ ۖ قَالَ هَلْ عَسَيْتُمْ إِن كُتِبَ عَلَيْكُمُ ٱلْقِتَالُ أَلَّا تُقَـٰتِلُوا۟ ۖ قَالُوا۟ وَمَا لَنَآ أَلَّا نُقَـٰتِلَ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ وَقَدْ أُخْرِجْنَا مِن دِيَـٰرِنَا وَأَبْنَآئِنَا ۖ فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ ٱلْقِتَالُ تَوَلَّوْا۟ إِلَّا قَلِيلًا مِّنْهُمْ ۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌۢ بِٱلظَّـٰلِمِينَ
Je, hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipomwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, ilhali tumeshatolewa katika maboma yetu na watoto wetu? Lakini walipoandikiwa kupigana vita, wakageuka, isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema madhalimu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipo mwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali tumetolewa majumbani kwetu na watoto wetu? Lakini walipo andikiwa kupigana waligeuka, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu. [246]
[246] Zingatia khabari hii ya ajabu ya baadhi ya Wana wa Israili baada ya zama za Musa. Walimtaka Nabii wao wa wakati ule awawekee mtawala ataye weza kuwakusanya baada ya mfarakano walio kuwa nao, awaongoze chini ya bendera ya kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu na kurejeza utukufu wao. Yule Nabii akawauliza kuhakikisha kama wana ukweli katika jambo hilo: "Je haiwezi kuwa nyinyi mtaingia woga mkatae kupigana pindi mkifaridhiwa mpigane?" Wakakataa hayo wakisema: "Itakuwaje tusipigane kurejeza haki zetu, na hali sisi tumefukuzwa makwetu na adui?" Mwenyezi Mungu alipo waitikia yale wayatakayo na akaandikia vita wakakataa ila kikundi cha wachache tu miongoni mwao. Na kule kukataa kwao ni dhulma kujidhulumu nafsi zao, na Nabii wao na Dini yao. Na Mwenyezi Mungu anayajua hayo kwao, na atawalipa malipo ya madhaalimu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Kwani hukukijua, ewe Mtume, kisa cha watukufu na mabwana, miongoni mwa Wana wa Isrãîl, baada ya zama za Mûsã kupita? Walipomtaka Mtume wao amtawalishe kwao mfalme, wapate kukusanyika chini ya uongozi wake na wapate kupigana na maadui zao katika njia ya Allah Mtukufu. Nabii wao akawaambia, «Je, mambo ni kama vile ninavyoyatarajia kwamba lau mtafaradhiwa kupigana katika njia ya Allah Mtukufu kuwa hamtapigana? Kwani mimi nachelea mtaogopa na mtakimbia vitani.» Wakasema wakikanusha matarajio ya Nabii wao, «Ni kizuizi kipi kitakacho kutuzuia tusipigane katika njia ya Allah Mtukufu, ambapo adui yetu ametutoa kwenye Makao yetu na akatutenganisha na na watoto wetu kwa kutuua na kututeka?» Basi Allah Mtukufu Alipowafaradhia kupigana wakiwa na mfalme Aliyewachagulia walikuwa waoga na wakakimbia vitani, isipokuwa wachache kati yao waliojikita imara kwa fadhila za Allah Mtukufu. Allah Mtukufu Anawajua mno madhalimu, wenye kuzivunja ahadi zao.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net