Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 247

Al-Baqara 2:247

البقرة

وَقَالَ لَهُمْ نَبِيُّهُمْ إِنَّ ٱللَّهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكًا ۚ قَالُوٓا۟ أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ ٱلْمُلْكُ عَلَيْنَا وَنَحْنُ أَحَقُّ بِٱلْمُلْكِ مِنْهُ وَلَمْ يُؤْتَ سَعَةً مِّنَ ٱلْمَالِ ۚ قَالَ إِنَّ ٱللَّهَ ٱصْطَفَىٰهُ عَلَيْكُمْ وَزَادَهُۥ بَسْطَةً فِى ٱلْعِلْمِ وَٱلْجِسْمِ ۖ وَٱللَّهُ يُؤْتِى مُلْكَهُۥ مَن يَشَآءُ ۚ وَٱللَّهُ وَٰسِعٌ عَلِيمٌ

Maana

Na Nabii wao akawaambia: Hakika, Mwenyezi Mungu ameshawateulia Taluti (Sauli) kuwa ndiye mfalme. Wakasema: Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, ilhali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Hakika, Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa elimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na Nabii wao akawaambia: Mwenyezi Mungu amekuteulieni Twaluti (Sauli) kuwa ni mfalme. Wakasema: vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa ilimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi. [247]

[247] Nabii wao akawaambia: "Hakika Mwenyezi Mungu amekuitikieni, basi amemkhiari Twaluti awe ndiye mtawala wenu." Wakuu wao wakapinga huo uteuzi wa Mwenyezi Mungu, wakisema: "Kwa nini awe yeye ni wa kututawala na hali sisi ni bora kuliko yeye. Yeye si mtu wa ukoo bora wala hana mali." Nabii wao akawarudi kwa kusema: "Mwenyezi Mungu amemkhiari yeye kuwa ni mtawala wenu kwa sababu ana sifa nyingi za uwongozi, kama mazoezi makubwa katika mambo ya vita, na siyasa ya kutawala, pamoja na nguvu za mwili. Na utawala uko katika mkono wa Mwenyezi Mungu humpa amtakaye katika waja wake, wala yeye hatagemei urithi wala mali." Na fadhila za Mwenyezi Mungu na ujuzi wake umeenea. Yeye huchagua lilio na maslaha yenu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na Mtume wao aliwaambia, «Hakika Allah Mtukufu amewaletea Ṭālūt kuwa ni mfalme, ikiwa ni kuyaitikia maombi yenu, ili awaongoze katika kupigana na adui yenu kama mlivyoomba.» Wakasema wakuu wa Wana wa Isrãîl, «Vipi Ṭālūt atakuwa mfalme kwetu, hali yeye hastahiki hilo? Yeye si katika wajukuu wa wafalme, wala hatoki kwenye nyumba ya utume na wala hakupewa ukunjufu wa mali ya kujisaidia nayo katika ufalme wake. Sisi tuna haki zaidi ya huu ufalme kuliko yeye. Kwani sisi ni wajukuu wa wafalme na tunatoka kwenye nyumba ya utume.» Mtume wao akawaambia, «Hakika Allah Mtukufu Amewachagulia, na Yeye, Aliyetakasika na kila sifa mbaya, Anayajua zaidi mambo ya waja Wake, na amemuongezea ukunjufu wa elimu na nguvu ya mwili ya kupigana na adui. Na Allah Mtukufu ni Mmiliki wa ufalme. Anampa ufalme wake Anayemtaka katika waja wake. Na Allah Mtukufu ni Mwingi wa fadhila na utoaji, ni Mjuzi kabisa wa ukweli wa mambo, hapana chenye kufichika Kwake».

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net