Al-Baqara 2:231
البقرةوَإِذَا طَلَّقْتُمُ ٱلنِّسَآءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ سَرِّحُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ ۚ وَلَا تُمْسِكُوهُنَّ ضِرَارًا لِّتَعْتَدُوا۟ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُۥ ۚ وَلَا تَتَّخِذُوٓا۟ ءَايَـٰتِ ٱللَّهِ هُزُوًا ۚ وَٱذْكُرُوا۟ نِعْمَتَ ٱللَّهِ عَلَيْكُمْ وَمَآ أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّنَ ٱلْكِتَـٰبِ وَٱلْحِكْمَةِ يَعِظُكُم بِهِۦ ۚ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ وَٱعْلَمُوٓا۟ أَنَّ ٱللَّهَ بِكُلِّ شَىْءٍ عَلِيمٌ
Na mtakapowataliki wanawake talaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo, ameidhulumu nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa masikhara. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyowateremshia katika Kitabu na hekima anachowaonya kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mno kila kitu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na mtakapo wapa wanawake t'alaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa maskhara. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyo kuteremshieni katika Kitabu na hikima anacho kuonyeni kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. [231]
[231] Mnapo wawacha wake wakakaribia kumaliza eda zao mnaweza kuwarejea kwa makusudio ya uadilifu na kukaa nao kwa wema bila ya kuwadhuru, na pia mnaweza kuwaacha watimize eda zao kwa kuzingatia muamala mwema ulio laiki wakati wa kufarikiana bila ya kuwatendea mabaya. Wala haijuzu katika kuwarejea ikawa makusudio yake ni madhara na kuirefusha eda. Mwenye kutenda hayo basi mwenyewe amejinyima starehe ya maisha ya mke na mume, na imani ya watu kwake, na anastahiki kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu. Wala msizifanyie maskhara na mchezo na kuwa ni upuuzi hukumu za Mwenyezi Mungu zilizo kuja katika Aya hizi kwa ajili ya kutengeza maisha ya kinyumba, na zikaweka khatamu za ukoo katika mikono ya wakili, naye ni mume, mkawa mnatoa T'alaka bila ya sababu, na mkawapatisha wake zenu madhara na maudhi. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu kwa kukupangieni mpango bora kabisa katika maisha ya ndoa, na pia kwa aliyo kuteremshieni katika Kitabu kilicho bainisha wazi ujumbe wa Muhammad, na ilimu mbali mbali zenye manufaa, na mifano na hadithi za kukuwaidhini na kukuongoeni. Na jikingeni na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa Mwenyezi Mungu anajua siri zenu na mnayo dhihirisha na niya zenu na vitendo vyenu. Naye ni Mwenye kukulipeni kwa myatendayo.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Pindi mtakapowataliki wanawake wakakaribia siku za kumaliza eda lao, basi warejeeni hali ya kuwa nia zenu ni kuwatekelezea haki zao kwa njia nzuri, kisheria na kidesturi, au waacheni mpaka eda lao limalizike. Na kueni na hadhari, isije ikawa kuwarejea ni kwa lengo la kuwadhuru kwa kuwafanyia uadui katika haki zao. Na yoyote atakayelifanya hilo, ameshaidhulumu nafsi yake kwa kustahiki mateso. Na wala msizifanye aya za Allah Mtukufu na hukumu Zake kuwa ni mchezo na upuzi. Nakumbukeni neema ya Allah Mtukufu kwenu, kwa kuwafanya Waislamu na kuwafafanulia hukumu Zake. Na yakumbukeni yale Aliyoyateremsha Allah Mtukufu, ya Qur’ani na mafundisho ya Mtume Wake. Na mshukuruni Allah Mtukufu kwa neema hizi zilizo kubwa. Allah Mtukufu Anawakumbusha hayo msiende kinyume nayo. Basi, mcheni Allah Mtukufu Na mjue kwamba Allah Mtukufu ni Mjuzi wa kila kitu, hapana kitu chenye kufichika Kwake, na Atamlipa kila mmoja kwa anayostahiki alipwe.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net