Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 2 · Aya ya 219

Al-Baqara 2:219

البقرة

يَسْـَٔلُونَكَ عَنِ ٱلْخَمْرِ وَٱلْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَآ إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَـٰفِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَآ أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ وَيَسْـَٔلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلِ ٱلْعَفْوَ ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ ٱللَّهُ لَكُمُ ٱلْـَٔايَـٰتِ لَعَلَّكُمْ تَتَفَكَّرُونَ

Maana

Wanakuuliza juu ya mvinyo na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilichozidi mahitaji. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kutafakari.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri-- [219]

[219] Ewe Muhammad! Wanakuuliza juu ya hukumu ya ulevi na kamari. Waambie kwamba katika yote mawili hayo pana madhara makubwa, kwa kuharibu siha na kupoteza akili na mali, na kuleta chuki na uadui baina ya watu. Pia ndani ya hayo yapo manufaa, kama kujipumbaza na kupata faida ya sahali. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake, basi epukaneni nayo. Na wanakuuliza watoe nini? Wajibu watoe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kilicho chepesi na hakina uzito kukitoa. Hivyo ndio Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri yale yatakayo kurejeeni katika maslaha ya dunia na Akhera. Kifungu hichi cha Qur'ani kinatuwekea wazi makusudio ya sharia ya Kiislamu. Kinatueleza kuwa sharia inataka manufaa ya waja. Chenye kuzidi nafuu yake kuliko madhara kinafaa. Chenye nafuu chache kuliko madhara kinakatazwa. Pia kifungu kinatuonyesha kuwa vitu ulimwenguni vimechanganya mema na mabaya. Hapana ovu lisio kuwa na wema, wala wema usio na uovu. Ulevi, mama wa maovu, unao haribu akili na kumfanya mtu kuwa mnyama, nao una faida pamoja na uovu wake usio na mpaka. Na kamari inayo shughulisha nafsi na akili, ikaleta mpapatiko usio sita, nayo ina nafuu yake pamoja na kuwa na madhambi yanayo fisidi maisha na nyumba za watu, na kila makhusiano bora ya binaadamu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Wanakuuliza Waislamu, ewe Nabii, hukumu ya kutumia khamr kwa kunywa, kuuza na kununua. Khamr ni kila chenye kulewesha kinachofinika akili na kuziba, kiwe ni chenye kunywewa au kuliwa. Na wanakuuliza kuhusu hukumu ya kamari. Kamari ni kupokea au kutoa mali kwa bahati nasibu, nayo ni mashindano ambayo yana kupeana badali kutoka pande mbili za ushindani. Waambie, «Katika hayo pana madhara mengi na uharibifu mwingi katika dini na dunia, na akili na mali. Na yamo, katika mambo mawili hayo, manufaa kwa watu, kwa upande wa kuchuma mali na mengineyo. Na madhambi yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake, kwani huzuia kumtaja Allah Mtukufu na kusali, na yote mawili yanaleta uadui na kuchukiana kati ya watu na yanaharibu mali». Huu ulikuwa ni utayarishaji wa kuyaharamisha mambo mawili hayo. Na wanakuuliza kuhusu kiwango ambacho wao wakitoe katika mali yao kwa njia ya sadaka na kujitolea.Waambie, «Toeni kiwango kinachozidi baada ya mahitaji yenu.» Mfano wa haya maelezo yaliyo wazi, Allah Mtukufu Anawabainishia aya na hukumu za Sheria, ili mpate kuyafikiria yenye manufaa kwenu

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Baqara

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net