Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 13 · Aya ya 4

Ar-Ra'd 13:4

الرعد

وَفِى ٱلْأَرْضِ قِطَعٌ مُّتَجَـٰوِرَٰتٌ وَجَنَّـٰتٌ مِّنْ أَعْنَـٰبٍ وَزَرْعٌ وَنَخِيلٌ صِنْوَانٌ وَغَيْرُ صِنْوَانٍ يُسْقَىٰ بِمَآءٍ وَٰحِدٍ وَنُفَضِّلُ بَعْضَهَا عَلَىٰ بَعْضٍ فِى ٱلْأُكُلِ ۚ إِنَّ فِى ذَٰلِكَ لَـَٔايَـٰتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ

Maana

Na katika ardhi vimo vipande vilivyokaribiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isiyochipua kwenye shina moja, nayo inanyweshwa katika maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yake kuwa bora kuliko mingine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa kaumu wanaotia mambo akilini.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isio chipua kwenye shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanao tia mambo akilini. [4]

[4] Na hakika hiyo ardhi nafsi yake ina maajabu. Ndani yake vipo vipande vilivyo karibiana, navyo juu ya hivyo vina udongo mbali mbali. Vingine ardhi yaabisi, na vingine vya rutba, ijapo kuwa ni udongo ule ule. Ndani yake yapo mabustani yaliyo jaa miti ya mizabibu, na ndani yake mazao mengine yanavunwa, na mitende yenye kuzaa, nayo ama iliyo kusanyika au iko mbali mbali. Na yote hayo ijapo kuwa inanyweshwa maji yale yale yanakhitalifiana kwa utamu wao. Na hakika katika ajabu hizi zipo dalili wazi za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye akili ya kufikiria. Aya hii tukufu inaonyesha ilimu ya ardhi (Geology) na ilimu ya mazingira (Ecology) na athari yao juu ya sifa za mimea. Inajuulikana katika ilimu kuwa rutuba ya ardhi inategemea juu ya chembe chembe za maadeni zinazo khitalifiana kwa namna na ukubwa, na maji yanayo toka kwenye mvua, na hewa, na vitu vyenye asili ya uhai, kama mimea na vyenginevyo, ambavyo hupatikana juu ya udongo au ndani yake. Huwapo hivyo kwa mamilioni vidogo vidogo hata havionekani kwa jicho tu. Kwa jumla ukizingatia haya utaona yanaonyesha uwezo wa Muumba na busara ya uumbaji, kwani ardhi kama wasemavyo wakulimu inakhitalifiana kila shubiri. Na inajuulikana kwa wanazuoni wa sayansi kuwa ukipatikana upungufu katika hivyo vitu vya msingi katika udongo basi hudhihirisha upungufu wake katika mimea, na kwa hivyo wakulima hujalizia upungufu huo kwa kutia mbolea mbali mbali na hutengeneza hali ya mazingira. Na hayo yana athari zake juu ya mazao ikiwa kwa mmea wa namna moja au namna mbali. Ametakasika Mwenyezi Mungu ambaye katika mikono yake upo ufalme wa kila kitu, naye ni Muweza wa kila kitu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na kwenye ardhi kuna sehemu zinazo pakana, kati ya hizo kuna zilizo nzuri zenye kuota mimea inayowafaa watu na kati ya hizo kuna kavu zenye chumvi zisizootesha chochote. Na katika ardhi nzuri kuna mashamba ya zabibu, na Amejaalia humo aina tafauti za mazao na mitende iliyokusanyika mahali pamoja na isiyokusanyika hapo, vyote hivyo viko katika mchanga mmoja na vinakunywa maji mamoja, isipokuwa vinatafautiana katika matunda, ukubwa, utamu na mengineyo: hili ni tamu na hili ni kali, na mengine ni bora kuliko mengine katika kula. Katika hilo kuna dalili kwa mwenye moyo unaoyaelewa maamrisho ya Allah Mtukufu na makatazo Yake.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Ar-Ra'd

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net