At-Tawba 9:74
التوبةيَحْلِفُونَ بِٱللَّهِ مَا قَالُوا۟ وَلَقَدْ قَالُوا۟ كَلِمَةَ ٱلْكُفْرِ وَكَفَرُوا۟ بَعْدَ إِسْلَـٰمِهِمْ وَهَمُّوا۟ بِمَا لَمْ يَنَالُوا۟ ۚ وَمَا نَقَمُوٓا۟ إِلَّآ أَنْ أَغْنَىٰهُمُ ٱللَّهُ وَرَسُولُهُۥ مِن فَضْلِهِۦ ۚ فَإِن يَتُوبُوا۟ يَكُ خَيْرًا لَّهُمْ ۖ وَإِن يَتَوَلَّوْا۟ يُعَذِّبْهُمُ ٱللَّهُ عَذَابًا أَلِيمًا فِى ٱلدُّنْيَا وَٱلْـَٔاخِرَةِ ۚ وَمَا لَهُمْ فِى ٱلْأَرْضِ مِن وَلِىٍّ وَلَا نَصِيرٍ
Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao hakika wamekwishasema neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakawa na utashi mkubwa juu ya yale ambayo hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwatajirisha, na Mtume wake pia kutokana na fadhila zake. Basi wakitubu, itakuwa heri kwao. Na wakigeuka, Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na wala hawana katika ardhi mlinzi yeyote wala wa kuwanusuru.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao wamekwisha sema neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakajihimu kufanya ambayo hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kutokana na fadhila zake. Wakitubu itakuwa kheri kwao, na wakigeuka Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu chungu duniani na Akhera. Na wala hawana katika ardhi mlinzi wala wa kuwanusuru. [74]
[74] Hao wanaafiki wanaapa mbele yako, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwamba hawakusema jambo baya katika hayo uliyo ambiwa. Nao ni waongo katika kukataa kwao, wanaapa kiapo cha uwongo! Na wao hakika wamesema neno la kufuru. Na ukafiri wao sasa umebainika, baada ya kuwa kwanza umefichika. Na hapana sababu yoyote ya kukuchukia ila ni kiburi kwa neema walizo pewa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa kule kupewa ngawira walizo shirikiana na Waislamu! Wakirejea kwa Mwenyezi Mungu, wakaacha unaafiki wao, na wakajuta kwa waliyo yatenda, toba yao itakubaliwa. Na hivyo itakuwa kheri kwao. Wakiitupa Imani, basi Mwenyezi Mungu atawaadhibu duniani kwa namna mbali mbali za balaa, na kesho Akhera atawatia katika Moto wa Jahannamu. Wala hawatapata katika ardhi wa kuwapigania, au wa kuwaombea, au wa kuwanusuru.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Wanafiki wanaapa kwa Allah Mtukufu kwamba wao hawakusema kitu cha kumkosea Mtume na Waislamu. Wao ni warongo. Hakika wamesema neno la ukafiri na wametoka kwa hilo kwenye Uislamu, na wamejaribu kumdhuru Mtume wa Allah Mtukufu (sala na salamu zimuendee), Allah Mtukufu hakuwawezesha kulifanya hilo. Na wanafiki hawakupata kitu chochote cha kumtia dowa na kumkosoa, isipokuwa ni kwamba Allah Mtukufu Aliwaneemesha akawapa utajiri kwa milango ya heri na baraka Aliyomfungulia Nabii Wake, (sala na salamu zimuendee). Basi wakirudi makafiri hawa kwenye Imani na kutubia, hilo ni bora kwao, na wakigeuka nyuma au wakasalia hali ile walivyo, Allah Mtukufu Atawaadhibu adhabu iumizayo hapa duniani, kupitia mikono ya Waislamu, na kesho Akhera kwa Moto wa Jahanamu, na hapatakuwa na mwokoaji wa kuwaokoa wala msaidizi wa kuwakinga na janga la adhabu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net