Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 9 · Aya ya 60

At-Tawba 9:60

التوبة

إِنَّمَا ٱلصَّدَقَـٰتُ لِلْفُقَرَآءِ وَٱلْمَسَـٰكِينِ وَٱلْعَـٰمِلِينَ عَلَيْهَا وَٱلْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِى ٱلرِّقَابِ وَٱلْغَـٰرِمِينَ وَفِى سَبِيلِ ٱللَّهِ وَٱبْنِ ٱلسَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ ٱللَّهِ ۗ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Maana

Hakika sadaka ni za mafakiri tu, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na waliogharamika, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu uliofaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima. [60]

[60] Zaka iliyo faridhiwa haitumiwi ila kwa mafakiri wasio pata cha kuwatosha, na masikini wagonjwa ambao hawawezi kazi wala hawana mali, na wale wanao itumikia kwa kuikusanya, na wanao tiwa moyo kwa sababu wanatarajiwa kusilimu na kupatikana kwao manufaa kwa utumishi wao na kuunusuru Uislamu, na wale wanao eneza Uislamu na kufanya tabshiri (Da'awa), na katika kuwakomboa waliomo utumwani na walio tekwa, na kuwatoa waliomo katika unyonge na utawala wa madhila, na katika kuwalipia wenye madeni walio shindwa kuyalipa ikiwa hayo madeni hayakutokana na madhambi au dhulma au upumbavu, na katika kuzatiti Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na katika mambo kama hayo yaliyomo katika njia za kheri na wema, na katika kusaidia wasafiri walio katikiwa kupata msaada wa mali yao na watu wao. Mwenyezi Mungu ameyatungia sharia hayo kuwa ni waajibu kwa ajili ya maslaha ya waja wake. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye kujua vyema maslaha ya viumbe vyake, na Mwenye hikima kwa anayo yafanyia sharia. Zaka ni mpango ulio wekwa wa kukusanya mali kutokana na matajiri na kurudishiwa mafakiri. Kwa hivyo ni haki ya mafakiri katika mali ya matajiri. Na huyakusanya mtawala na huyatumilia kwa njia zake ambazo zinahisabiwa kuwa ndio muhimu kabisa na bora hizo ni kupiga vita athari za ufakiri kwa mafakiri. Hupewa mafakiri, masikini, wasafiri, kusaidiwa mwenye deni aliye kopa kwa jambo la halali si kwa uharibifu, na katika hayo ipo njia ya kupewa mkopo "kardhan hasanan" (mkopo kwa Lillahi). Katika mwanzo wa Uislamu ilivyo kuwa Zaka inatozwa na kutumiwa vilivyo hapakuwapo katika umma mtu anaye lala na njaa, wala mwombaji aliye dhalilika kwa haja. Ilifika hadi hata wenye kutumikia Zaka wakashitaki kuwa jinsi ya kuenea neema hapana wa kustahiki kupewa. Alishitaki mmoja wapo katika Afrika kumshitakia Khalifa Umar bin Abdulaziz kuwa hakumpata fakiri wa kumpa Zaka. Umar akamwambia walipie wenye madeni. Akawalipia. Bado akashitaki tena. Akamwambia wanunue watumwa uwape uhuru wao. Huo basi ndio utumiwaji wa Zaka. Na ukitaka kweli, ni kuwa lau kuwa Zaka zikikusanywa kwa inavyo faa, na zikatumiliwa zinavyo stahiki basi huo bila ya shaka ungeli kuwa ni mpango bora kabisa wa kudhamini maisha ya umma yasipate shida ya umasikini.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Zaka za lazima zinapewa wahitaji wasiomiliki kitu, masikini wasiomiliki kiwango kinachowatosha kwa mahitaji yao, wenye kuzishughulikia kwa kuzikusanya,wale ambao mwazizoeza nyoyo zao, miongoni mwa wale mnaotarajia wasilimu au ipate nguvu Imani yao au wawe na manufaa kwa Waislamu au mzuie kwazo madhara ya mtu yoyote yasiwafikie Waislamu. Pia zinatolewa katika kuacha huru watumwa na wale wenye mikataba ya uhuru. Na zinatolewa kupewa wenye kuingia kwenye madeni kwa sababu ya kuleta maelewano baina ya watu na wenye kulemewa na madeni waliyokopa kwa lengo lisiliokuwa la uharibifu au utumiaji wa kupita kiasi kisha wakashindwa kulipa. Na zinapewa wapiganaji katika njia ya Allah Mtukufu. Na zinapewa msafiri aliyeishiwa na matumizi. Ugawaji huu ni lazima Aliyoifaradhia Allah Mtukufu na Akaikadiria. Na Allah Mtukufu ni Mjuzi mno wa mambo yanayowafaa waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na sheria Zake.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

At-Tawba

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net