Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 9 · Aya ya 40

At-Tawba 9:40

التوبة

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ ٱللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ثَانِىَ ٱثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِى ٱلْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَـٰحِبِهِۦ لَا تَحْزَنْ إِنَّ ٱللَّهَ مَعَنَا ۖ فَأَنزَلَ ٱللَّهُ سَكِينَتَهُۥ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُۥ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ٱلسُّفْلَىٰ ۗ وَكَلِمَةُ ٱللَّهِ هِىَ ٱلْعُلْيَا ۗ وَٱللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

Maana

Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwishamnusuru walipomtoa wale waliokufuru, akiwa ni wa pili wa wawili walipokuwa katika pango, alipomwambia sahibu yake: 'Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi.' Basi Mwenyezi Mungu akauteremsha utulivu wake juu yake, na akamuunga mkono kwa majeshi ambayo hamkuyaona, na akalifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini zaidi, na Neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu zaidi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipo mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyo yaona, na akalifanya neno la walio kufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima. [40]

[40] Enyi Waumini! Ikiwa nyinyi hamtasaidia kumnusuru Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi. Kwani Mwenyezi Mungu anatosha Yeye kumnusuru. Kama pale alipo msaidia na akamnusuru alipo tolewa Makka kwa kahari na makafiri, naye hana mwenziwe ila Abu Bakar peke yake. Wakawa wao wawili pangoni wanajificha wasionekane na washirikina walio kuwa wanawasaka wawaadhibu na kuwauwa. Abu Bakar akawa anamkhofia Mtume maisha yake. Mtume akamwambia kumpoza: Usihuzunike! Kwani hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi, kwa kutunusuru na kutusaidia. Hapo Mwenyezi Mungu akamteremshia Abu Bakar utulivu, na akamuunga mkono Mtume kwa askari walio toka kwake, na ambao hawawajui ila Yeye Subhanahu. Na mambo yakamalizikia kuwa shari ya washirikina ikavia na Dini ya Mwenyezi Mungu ikashinda. Na Mwenyezi Mungu anasifika kuwa ni Mwenye nguvu, hashindiki, ni Mwenye hikima hapotei katika mipango yake. Hilo pango alilo jificha Nabii s.a.w. na rafiki yake Abu Bakar r.a. lilikuwa katika mlima wa Thor, karibu na Makka. Wakakaa humo siku tatu, baadae wakatoka usiku walipoona msako umetulia. Walifika Madina taarikh 8 katika Mwezi Rabii'ul awwal (Mfungo Sita) mwaka wa kwanza wa Hijra. (20 Septemba, 630 kwa taarikh za Kizungu.)

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi mkusanyiko wa Maswahaba wa Mtume wa Allah Mtukufu (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukiye), msipotoka pamoja na yeye anapowataka mtoke, na msipomtetea, basi Allah Mtukufu Alimsaidia na kumtetea siku ile Makafiri wa Kikureshi walipomtoa kwenye mji wake wa Makka, na yeye ni wapili kati ya wawili (yeye na Abû Bakr al-Ṣiddîq, radhi za Allah Mtukufu zimshukie) wakawafanya ibidi waingie pangoni katika jabali la Thawr, wakakaa humo siku tatu, pindi alipomwambia rafiki Yake Abû Bakr, alipomuona ameingiwa na hofu juu yake, «Usihuzunike, Mungu Yupo pamoja na sisi» kwa kutunusuru na kutupa nguvu. Hapo Allah Mtukufu Aliteremsha utulivu kwenye moyo wa Mtume wa Allah Mtukufu (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukiye), na akamsaidia kwa askari ambao hakuna aliowaona kati ya wanadamu, nao ni Malaika. Hapo Allah Mtukufu Alimuokoa na adui yake, Akawafanya wanyonge maadui wake, Akalifanya neno la waliokanusha ndilo la chini na neno la Allah Mtukufu ndilo la juu. Na hilo ni kwa kuliinua juu jambo la Uislamu. Na Allah Mtukufu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika kuyaendesha mambo ya waja Wake. Katika ayah hii pana kitambulisho cha cheo cha Abû Bakr (radhi za Allah Mtukufu zimshukie).

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

At-Tawba

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net