At-Tawba 9:37
التوبةإِنَّمَا ٱلنَّسِىٓءُ زِيَادَةٌ فِى ٱلْكُفْرِ ۖ يُضَلُّ بِهِ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ يُحِلُّونَهُۥ عَامًا وَيُحَرِّمُونَهُۥ عَامًا لِّيُوَاطِـُٔوا۟ عِدَّةَ مَا حَرَّمَ ٱللَّهُ فَيُحِلُّوا۟ مَا حَرَّمَ ٱللَّهُ ۚ زُيِّنَ لَهُمْ سُوٓءُ أَعْمَـٰلِهِمْ ۗ وَٱللَّهُ لَا يَهْدِى ٱلْقَوْمَ ٱلْكَـٰفِرِينَ
Hakika kuahirisha (miezi) ni kuzidi tu katika kukufuru; wanapotezwa kwa hilo wale waliokufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyoitukuza Mwenyezi Mungu, ndiyo wahalalishe yale aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu makafiri.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni kuzidi katika kukufuru; kwa hayo hupotezwa walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo huhalalisha alivyo viharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri. [37]
[37] Na hakukuwa kuichelewesha miezi mitakatifu, au baadhi yake, kuliko alivyo iweka Mwenyezi Mungu, ila ni kuzidi ukafiri, kama walivyo kuwa wakifanya watu wa kijahiliya. Hao makafiri wakizidisha hivyo kuongeza upotovu juu ya upotovu! Waarabu wakati wa ujuhali walikuwa hufanya mwezi uliyo harimishwa kupigana vita kuwa ni wa halali, pindi wakihitajia kupigana. Na hufanya mwezi ulio halalishwa ndio ulio harimishwa. Na wakisema: Mwezi kwa mwezi. Yaani kulipizia ipate kutimia idadi ile aliyo harimisha Mwenyezi Mungu. Matamanio yao yamewapendezeshea kitendo chao hicho kiovu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu walio shikilia kukataa kuifuata Njia ya kwendea Kheri.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Hakika yale Waarabu walikuwa wakiyafanya katika kipindi cha ujinga kwa kuiharamisha miezi minne kila mwaka, kwa idadi na sio kwa kuyataja majina ya miezi iliyoharamishwa na Allah Mtukufu, wakawa waichelewesha baadhi yake au waitanguliza, na wakaiweka badala yake miezi ya uhalali kama wanavyotaka, kulingana na mahitaji yao ya kupigana. Hakika hayo ni katika kuzidisha ukafiri. Shetani anawapoteza kwa hayo wale waliokufuru: wanauhalalisha ule waliouchelewesha kuuharamisha kati ya miezi minne mwaka huu, na wanauhalalisha mwaka mwingine, ili walinganishe kiwango cha miezi minne, wapate kuihalalisha Aliyoiharamisha Allah Mtukufu kati ya hiyo. Shetani amewapambia vitendo viovu. Na Allah Mtukufu hawapi taufiq watu Makafiri kufuata haki na usawa.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net