Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 9 · Aya ya 29

At-Tawba 9:29

التوبة

قَـٰتِلُوا۟ ٱلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِٱللَّهِ وَلَا بِٱلْيَوْمِ ٱلْـَٔاخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ ٱللَّهُ وَرَسُولُهُۥ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ ٱلْحَقِّ مِنَ ٱلَّذِينَ أُوتُوا۟ ٱلْكِتَـٰبَ حَتَّىٰ يُعْطُوا۟ ٱلْجِزْيَةَ عَن يَدٍ وَهُمْ صَـٰغِرُونَ

Maana

Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho, wala hawaharamishi yale aliyoharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki Dini ya haki, miongoni mwa wale waliopewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa hiari yao, hali wametii.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho, wala hawaharimishi alivyo harimisha Mwenyezi Mungu na Mtume, wala hawashiki Dini ya Haki, miongoni mwa walio pewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa khiari yao, hali wamet'ii. [29]

[29] Enyi mlio amini! Wapigeni vita makafiri katika Watu wa Kitabu wasio muamini Mwenyezi Mungu kwa Imani iliyo sawa, wala hawakiri kuwa kuna kufufuliwa na kulipwa, wala hawayashiki aliyo yakataza Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaishiki Dini ya Haki, nayo ni Uislamu. Wapigeni vita mpaka waamini, au watoe Jizya, nao wamenyenyekea na wat'iifu, si wenye kuasi, wasaidie katika kujenga mfuko wa Kiislamu. "Jizya" ni katika kipato muhimu katika madukhuli ya serikali ya Kiislamu. Kodi hii ilikuwa baina ya Dirham 8 na 40. Kila mtu mmoja katika Mayahudi na Wakristo na walio kuwa kama wao akitozwa Dirham 12. Akilazimishwa kulipa mwanamume aliye kwisha baalighi, na mzima wa mwili na akili, na kwa sharti awe na mali ya kuweza kutoa. Wanawake na watoto walisamehewa, na vile vile vizee. Kwa sababu hao hawapigwi vita. Wala hawatozwi vipofu na wasio jiweza, ila wakiwa matajiri. Kadhaalika hawatozwi mafakiri na masikini na watumwa. Wala hawakutakiwa kutoa mamonaki, yaani mapadri wanao jitenga na watu. Na asli ya kutozwa Jizya ni ulinzi wa wasio kuwa Waislamu. Kwa sababu Ahli Lkitaab, Watu wa Biblia, na walio kama wao, hawakulazimishwa kuingia vitani kulinda nchi wala kujilinda nafsi zao. Kwa hivyo ilikuwa ni haki wao watoe kodi kuwa ni badala ya ulinzi na manufaa mengine ya dola wanayo yapata na wanastarehea nayo. Pia ni badala ya wanacho kitoa Waislamu. Kwani Muislamu anatozwa ile khumsi (moja katika tano) ya ngawira, anatozwa Zaka ya mali, na Zaka ya Fitri, na kafara mbali mbali kwa kulipia makosa. Kwa hivyo ikawa hapana budi kuchukuliwa kodi kutokana kwa asiye kuwa Muislamu badala ya yote anayo yatoa Muislamu kwa maslaha ya wote na kwa ajili ya mafakiri wa wasio kuwa Waislamu. Wala haikukusudiwa kutozwa kodi kuwatia unyonge au kuwatia adabu. Kwani hayo hayaambatani na uadilifu wa Uislamu, wala hayakubaliani na makusudio yake mazuri.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi Waislamu, wapigeni vita Makafiri ambao hawamuamini Allah Mtukufu, wala hawaamini Kufufuliwa na Kulipwa, wala hawajiepushi na yale ambayo Allah Mtukufu na Mtume Wake wameyakataza, wala hawajilazimishi na hukumu za sheria ya Uislamu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, mpaka watoe jizia, ambayo nyinyi mnawalazimisha nayo, kwa mikono yao wakiwa wanyenyekevu na wanyonge.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

At-Tawba

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net