Al-Anfaal 8:60
الأنفالوَأَعِدُّوا۟ لَهُم مَّا ٱسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ ٱلْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِۦ عَدُوَّ ٱللَّهِ وَعَدُوَّكُمْ وَءَاخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ ٱللَّهُ يَعْلَمُهُمْ ۚ وَمَا تُنفِقُوا۟ مِن شَىْءٍ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ
Na waandalieni muwezavyo katika nguvu, na kwa farasi waliofungwa tayari tayari, ili muwatie hofu kwavyo maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo kando na hao ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na chochote mnachotoa kwenda katika Njia ya Mwenyezi Mungu, mtarudishiwa kikamilifu, nanyi hamtadhulumiwa.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa. [60]
[60] Enyi Umma wa Kiislamu! Tayarisheni kila muwezavyo nguvu za vita za namna zote kwa ajili ya kujizatiti kwa ajili ya kupigana, na wekeni askari walinzi na farasi wao mipakani na kando kando ya nchi, ili kwa hivi mjitayarishe na ulinzi mwatie kiwewe adui za Mwenyezi Mungu na adui zenu miongoni mwa hao makafiri ambao wamo kungojea likupateni jambo. Na pia mpate kuwatishia wenginewe ambao nyinyi hamwajui hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu anawajua, kwani hapana jambo linalo jificha kwake. Na kila mnacho kitoa kwa kuzitayarisha nguvu zenu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Yeye atakulipeni malipo ya kutosha, bila ya kupunguka hata chembe katika mnayo stahiki katika fadhila ya Mola wenu Mlezi Katika Aya hii tukufu pana kuhimizwa na kuamrishwa kujitayarisha kwa ajili ya kupambana na adui. Kwani vita, zamani na sasa, ni jambo la khatari na muhimu kabisa. Juu yake inategemea kheri na shari, kufa kupona kwa umati na umati. Basi yapasa kujitayarisha, kujizatiti, na kujitengeneza kwa jiha mbali mbali za vifaa na silaha na zana. Kuingia vitani bila ya kujipatia zana zote na kujitayarisha ni kutafuta kushindwa. Na tunaona hivi sasa madola yanavyo jiandaa wakati wa amani na vita, na yanavyo jenga siasa zao na mipango yao na wanavyo kusanya uwezekano wao wote ili wapate ushindi katika vita. Na vita sasa havimsazi mtu. Wanashiriki katika vita wanajeshi na raia. Kwa hivyo ndio inapasa zaidi kujitengeneza kila mmoja wao kwa matengenezo ya kuwakusanya na kuwaweka tayari wote ili upatikane ushindi.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na Tayarisheni, enyi makundi ya Waislamu,ili kukabiliana na maadui wenu, chochote mkiwezacho cha wingi wa watu na zana, ili muingize, kwa hio, hofu katika nyoyo za maadui wa Allah Mtukufu na maadui wenu wanaowavizia; na muwatishe wengine ambao uadui wao bado haujajitokeza kwenu hivi sasa, lakini Allah Mtukufu Anawajua na Anayajua yale ambayo wanayadhamiria. Na mali yoyote na vinginevyo mnavyovitoa katika njia ya Allah Mtukufu, vingi au vichache, Allah Mtukufu Atawapa badala yake duniani na Atawaekea thawabu zake mpaka Siku ya Kiyama; na nyinyi hamtapunguziwa malipo ya hayo chochote.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net