Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 7 · Aya ya 89

Al-A'raaf 7:89

الأعراف

قَدِ ٱفْتَرَيْنَا عَلَى ٱللَّهِ كَذِبًا إِنْ عُدْنَا فِى مِلَّتِكُم بَعْدَ إِذْ نَجَّىٰنَا ٱللَّهُ مِنْهَا ۚ وَمَا يَكُونُ لَنَآ أَن نَّعُودَ فِيهَآ إِلَّآ أَن يَشَآءَ ٱللَّهُ رَبُّنَا ۚ وَسِعَ رَبُّنَا كُلَّ شَىْءٍ عِلْمًا ۚ عَلَى ٱللَّهِ تَوَكَّلْنَا ۚ رَبَّنَا ٱفْتَحْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ قَوْمِنَا بِٱلْحَقِّ وَأَنتَ خَيْرُ ٱلْفَـٰتِحِينَ

Maana

"Bila ya shaka tutakuwa tumemzulia uongo Mwenyezi Mungu ikiwa tutarudi katika mila yenu baada ya Mwenyezi Mungu kwishatuokoa kutokana nayo. Wala haiwi kwetu sisi kuirejea mila hiyo, isipokuwa akitaka Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi. Mola wetu Mlezi umekienea kila kitu kwa elimu. Kwa Mwenyezi Mungu tumetegemea. Mola wetu Mlezi, hukumu baina yetu na kaumu yetu kwa haki, nawe ndiwe Mbora zaidi wa wanaohukumu."

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Bila ya shaka itakuwa tumemzulia uwongo Mwenyezi Mungu tukirudi katika mila yenu baada ya kwisha tuokoa nayo Mwenyezi Mungu. Wala haiwi kwetu sisi kuirejea mila hiyo, ila akitaka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu. Ujuzi wa Mola Mlezi wetu umeenea katika kila kitu. Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea. Ewe Mola Mlezi wetu! Tuhukumie baina yetu na kaumu yetu kwa haki, nawe ndiye mbora wa wanao hukumu. [89]

[89] Akaendelea zaidi kuwavunja tamaa yao ya kuwarejeza kwenye mila yao kama walivyo taka. Akasema: Tutakuwa tunamzulia uwongo Mwenyezi Mungu tukiwa katika mila yenu baada ya Mwenyezi Mungu kesha tuhidi kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na haifai sisi kuwa katika mila yenu kwa khiari yetu na kutaka kwetu, ila akipenda Mwenyezi Mungu turejee katika mila yenu. Na hayo hayawi! Kwa sababu Mola Mlezi wetu anatujua vyema, na Yeye hataki turejee kwenye upotovu wenu. Yeye aliye tukuka shani yake amekienea kila kitu kwa ujuzi wake. Anatuongoa kwa upole wake na hikima yake kwenye jambo litalo tuhifadhia Imani yetu. Kwa Yeye peke yake ndio tumesalimisha mambo yetu, na huku tunashikilia yale aliyo tuwajibisha tuyashike. Ewe Mola Mlezi wetu! Tutenge sisi na hao kaumu yetu kwa Haki, kama ilivyo kuwa mwendo wako unavyo amua baina ya wenye kufuata Haki na wakatenda mema, na wale wapotovu waharibifu. Na Wewe kwa kuwa ujuzi wako na uwezo ulivyo enea ndiye Muadilifu na Muweza kuliko mahakimu wote.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Akasema Shu‛ayb kuwaambia watu wake, kwa kuongezea, Tutakuwa tumemzulia Allah Mtukufu urongo tukirudi kwenye dini yenu baada ya Allah Mtukufu kutuokoa nayo. Haiwezekani kwetu kugeuka kuifuata dini isiyokuwa ya Mola wetu, isipokuwa iwapo Allah Mtukufu, Mola wetu, Ametaka. Hakika Mola wetu Amekienea kila kitu kwa ujuzi, kwa hivyo Anakijua kinachowafaa waja. Ni kwa Allah Mtukufu, Peke Yake, mategemeo yetu ya kupata uongofu na ushindi. Ewe Mola wetu, toa uamuzi wa haki kati yetu na watu wetu, na wewe ndiye bora wa wenye kutoa uamuzi.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-A'raaf

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net