Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 7 · Aya ya 155

Al-A'raaf 7:155

الأعراف

وَٱخْتَارَ مُوسَىٰ قَوْمَهُۥ سَبْعِينَ رَجُلًا لِّمِيقَـٰتِنَا ۖ فَلَمَّآ أَخَذَتْهُمُ ٱلرَّجْفَةُ قَالَ رَبِّ لَوْ شِئْتَ أَهْلَكْتَهُم مِّن قَبْلُ وَإِيَّـٰىَ ۖ أَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ ٱلسُّفَهَآءُ مِنَّآ ۖ إِنْ هِىَ إِلَّا فِتْنَتُكَ تُضِلُّ بِهَا مَن تَشَآءُ وَتَهْدِى مَن تَشَآءُ ۖ أَنتَ وَلِيُّنَا فَٱغْفِرْ لَنَا وَٱرْحَمْنَا ۖ وَأَنتَ خَيْرُ ٱلْغَـٰفِرِينَ

Maana

Na Musa akawateua kaumu wake wanaume sabini kwa ajili ya miadi yetu. Na ulipowachukua mtetemeko mkubwa, akasema: Mola wangu Mlezi! Ungelitaka, ungeliwaangamiza wao hapo kabla na hata mimi. Unatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wapumbavu katika sisi? Haya si chochote isipokuwa ni majaribio yako, unampoteza kwayo umtakaye, na unamuongoa umtakaye. Wewe ndiye rafiki mlinzi wetu. Basi tusitiri dhambi na uturehemu. Na Wewe ndiwe Mbora zaidi wa wasitirio dhambi.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na Musa akawateuwa watu sabiini katika kaumu yake kwa miadi yetu. Na ulipo fika mtetemeko mkubwa alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ungeli taka ungeli wahiliki wao na mimi zamani! Unatuhiliki kwa waliyo yafanya wajinga katika sisi? Haya si chochote ila ni mtihani wako, umpoteze umtakaye na umhidi umtakaye. Wewe ndiye Rafiki Mlinzi wetu. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe ndiye mbora wa kughufiria. [155]

[155] Kisha Mwenyezi Mungu alimuamrisha awalete baadhi ya jamaa katika kaumu yake wawatakie radhi walio muabudu ndama, na akawapa miadi. Musa akawateuwa katika kaumu yake watu sabiini katika wasio muabudu ndama, nao wakawa wanawawakilisha kaumu yao. Akenda nao mpaka kwenye mlima. Na huko wakamwomba Mwenyezi Mungu awaondolee balaa, na akubali toba ya walio muabudu ndama kati yao. Ikawachukua zilzala (tetemeko) kubwa pahala hapo, wakazimia kwa sababu yake. Na hayo kwa kuwa hawakuwaacha kaumu yao walipo abudu ndama, wala hawakuamrisha mema, wala hawakuwakanya maovu! Musa alipoona yale alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Lau ungeli penda kuwaangamiza ungeli waangamiza kabla hawajaja hapa kwenye miadi, na ukaniangamiza na mimi pia, ili waone hayo Wana wa Israili wasinituhumu kuwa mimi nimewauwa. Basi ewe Mola Mlezi wangu! Usituhiliki kwa walio yafanya wajinga kati yetu. Kwani hii balaa ya kuabudu ndama haikuwa ila ni majaribio yaliyo toka kwako. Wewe unampoteza unaye taka apotee katika hao wanao ishika njia ya shari, na unawahidi (unawaonoza) unaye taka ahidike. Wewe ndiye mwenye kusema: Nitawaandikia wenye kujikinga na ukafiri na maasi katika kaumu yako, na akatoa Zaka iliyo faridhiwa, na Mwenye kusamehe madhambi.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na Mûsã alichagua miongoni mwa watu wake wanaume sabiini walio bora kati yao, akatoka nao akaenda hadi Tûr Sînã’ kwa wakati na muda ambao Allah Mtukufu Alimuagizia akutane na Yeye pamoja nao ili watubie kwa yale yaliyokuwa kwa wahuni wa Wana wa Isrãîl ya kuabudu kigombe. Walipokuja mahali hapo walisema, «Hatutakuamini, ewe Mûsã mpaka tumuone Allah Mtukufu waziwazi, basi utakaposema na Yeye tuoneshe.» Papo hapo walishikwa na mtetemeko mkali wakafa. Akasimama Mûsã akimnyenyekea Allah Mtukufu na akasema, Ewe Mola wangu, niwaambie nini Wana wa Isrãîl nikiwajia na hali wewe umewaangamiza wabora wao? Lau ungetaka ungaliwaangamiza wote kabla ya hali hii ya kuwa mimi niko na wao. Hilo lingalikuwa sahali zaidi kwangu. Unatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wachache wa akili miongoni mwetu? Kitendo hiki ambacho watu wangu wamekifanya cha kuabudu kigombe, hakikuwa isipokuwa ni majaribu na mtihani, unampoteza kwayo unayemtaka miongoni mwa viumbe wako na unamuongoza kwayo unayemtaka kumuongoza. Ni wewe mtegemewa wetu na mwenye kutunusuru, tusamehe dhambi zetu na uturehemu kwa rehema zako; na wewe ndiye bora wa wenye kusamehe makosa na kusitiri dhambi.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-A'raaf

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net