Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 7 · Aya ya 150

Al-A'raaf 7:150

الأعراف

وَلَمَّا رَجَعَ مُوسَىٰٓ إِلَىٰ قَوْمِهِۦ غَضْبَـٰنَ أَسِفًا قَالَ بِئْسَمَا خَلَفْتُمُونِى مِنۢ بَعْدِىٓ ۖ أَعَجِلْتُمْ أَمْرَ رَبِّكُمْ ۖ وَأَلْقَى ٱلْأَلْوَاحَ وَأَخَذَ بِرَأْسِ أَخِيهِ يَجُرُّهُۥٓ إِلَيْهِ ۚ قَالَ ٱبْنَ أُمَّ إِنَّ ٱلْقَوْمَ ٱسْتَضْعَفُونِى وَكَادُوا۟ يَقْتُلُونَنِى فَلَا تُشْمِتْ بِىَ ٱلْأَعْدَآءَ وَلَا تَجْعَلْنِى مَعَ ٱلْقَوْمِ ٱلظَّـٰلِمِينَ

Maana

Na wakati aliporudi Musa kwa kaumu yake hali ya kuwa ameghadhibika na kuhuzunika, akasema: Ni mabaya mno mliyonifanyia nyuma yangu! Je, mmeiharakisha amri ya Mola wenu Mlezi? Na akazitupa chini mbao zile, na akamkamata kaka yake kichwa akimvuta kwake. (Harun) akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika kaumu hawa waliniona kuwa mimi ni dhaifu, na walikaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui zangu, wala usiniweke pamoja na kaumu madhalimu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na alipo rudi Musa kwa watu wake, naye amekasirika na kuhuzunika, alisema: Ni maovu yalioje mlio nifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu Mlezi? Na akaziweka chini zile mbao, na akamkamata kichwa ndugu yake akimvutia kwake. (Haarun) akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu, wala usinifanye pamoja na watu madhaalimu. [150]

[150] Na Musa alipo rejea kutoka kuzungumza na Mola Mlezi wake kuja kwa watu wake, naye kakasirika nao kwa vile walivyo muabudu ndama, na amehuzunika kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewatia mtihanini - kwani Mwenyezi Mungu alikwisha mpa khabari ya yale kabla hajarejea - aliwaambia: Kitendo gani kiovu hichi mlicho kitenda baada ya kuondoka kwangu! Mmetangulia kwa kumuabudu ndama msifuate amri ya Mola wenu Mlezi kuwa mningojee, na mkawa hamkuishika ahadi yangu mpaka nikakuleteeni Taurati? Akaziweka zile mbao, na akamuelekea nduguye kwa huzuni kubwa kwa yale aliyo yaona kwa kaumu yake. Akaingia kumvuta ndugu yake kwa kichwa akimbururia kwake kwa wingi wa ghadhabu. Haya ni kuwa alidhani kuwa amefanya taksiri hakuwazuia kufanya walio yafanya! Haarun akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu walipo fanya waliyo yafanya walinidharau na wakanishinda nguvu. Na wakakaribia kuniuwa kwa kuwa niliwakataza wasimuabudu ndama. Basi usiwafurahishe maadui kwa kunitesa mimi, wala usiitakidi kuwa mimi ni mmoja wa wenye kudhulumu, kwani mimi ni mbali nao na dhulma yao. Haarun amemwita Musa kwa kumnasibisha na mama yao, ijapo kuwa hao walikuwa ndugu khalisa, wa baba na mama, kwa sababu huyo mama alikuwa Muumini. Kumtaja yeye ni kuzidi kukumbusha mapenzi.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Aliporejea Mûsã kwa watu wake akiwa na hasira na huzuni, kwa kuwa Allah Mtukufu Alimpa habari kwamba watu wake wamepatikana na mtihani na kwamba Sãmirîy amewapoteza. Mûsã alisema, «Ni ubaya ulioje mlioufanya nyuma yangu baada ya mimi kuondoka! Je mmeitangulia amri ya Mola wenu?» Yaani, mlikufanyia haraka kuja kwangu kwenu, na hali ni jambo lililopangwa na Allah Mtukufu? Mûsã alizitupa mbao za Taurati kwa kuwakasirikia watu wake walioabudu ndama na kwa kumkasirikia ndugu yake Hãrûn. Akakishika kichwa cha Hãrûn na akakivuta upande wake. Hãrûn alisema kwa kubembeleza, Ewe mwana wa mamangu, ‘Hakika hawa watu walinidharau, waliniona ni mnyonge na walikaribia kuniua, kwa hivyo usiwafurahishe maadui kwa unayonifanya na usiniingize katika hasira zako ukanifanya ni pamoja na wale walioenda kinyume na amri yako na wakaabudu ndama».

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-A'raaf

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net