Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 6 · Aya ya 99

Al-An'aam 6:99

الأنعام

وَهُوَ ٱلَّذِىٓ أَنزَلَ مِنَ ٱلسَّمَآءِ مَآءً فَأَخْرَجْنَا بِهِۦ نَبَاتَ كُلِّ شَىْءٍ فَأَخْرَجْنَا مِنْهُ خَضِرًا نُّخْرِجُ مِنْهُ حَبًّا مُّتَرَاكِبًا وَمِنَ ٱلنَّخْلِ مِن طَلْعِهَا قِنْوَانٌ دَانِيَةٌ وَجَنَّـٰتٍ مِّنْ أَعْنَابٍ وَٱلزَّيْتُونَ وَٱلرُّمَّانَ مُشْتَبِهًا وَغَيْرَ مُتَشَـٰبِهٍ ۗ ٱنظُرُوٓا۟ إِلَىٰ ثَمَرِهِۦٓ إِذَآ أَثْمَرَ وَيَنْعِهِۦٓ ۚ إِنَّ فِى ذَٰلِكُمْ لَـَٔايَـٰتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

Maana

Na Yeye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni; na kwayo tukatoa mimea ya kila kitu. Na kutokana na baadhi yake tukatoa mimea ya kijani, tukatoa ndani yake punje zilizopandana; na kutokana na mitende katika makole yake yakatoka mashada yaliyo karibu; na mabustani ya mizabibu na mizaituni, na makomamanga, yanayofanana na yasiyofanana. Angalieni matunda yake yanapozaa na yakaiva. Hakika katika hayo kuna Ishara kwa kaumu wanaoamini.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na Yeye ndiye anaye teremsha maji kutoka mbinguni; na kwayo tunatoa mimea ya kila kitu. Kutokana na baadhi yao tukatoa mimea ya majani, tukatoa ndani yake punje zilizo pandana; na kutokana na mitende yakatoka kwenye makole yake mashada yaliyo inama; na bustani za mizabibu na mizaituni, na makomamanga, yaliyo fanana na yasiyo fanana. Angalieni matunda yake yanapo zaa na yakawiva. Hakika katika hayo pana Ishara kwa watu wanao amini. [99]

[99] Naye ndiye anaye teremsha kutoka mawinguni maji, ambayo kwayo akatoa kila namna ya mimea. Kuna mimea inayo toa majani laini kuwa ni mboga, na tunatoa pia mimea ya kuzaa punje nyingi zimepandana wenyewe kwa wenyewe. Na kutokana na makole ya mitende mna mashada yamebeba tende, wepesi kuzipata. Na pia tumetoa kutokana na maji mizabibu, na zaituni, na makomamanga. Katika hiyo yapo matunda yalio fanana kwa sura, na yasiyo fanana kwa utamu, na harufu, na namna ya faida yake. Hebu yaangalieni kwa kupima na kuzingatia matunda yake inapo zaa hiyo miti, na matunda yanapo wiva, vipi yanapo komaa baada ya kupitia hali mbali mbali! Hakika katika haya zipo ishara kwa wanao itafuta Haki na wanaamini na kunyenyekea. Aya hii inafahamisha maana kwa ilimu ya sayansi, nayo ni kuwa maji husaidia mimea kuchipua. Mbegu iliyo kaa tu haitaharaki husisimka kwa kupata maji ikaanza kumea, ikafanya kazi yake ya uhai. Mimea tena hukua na kutoa majani yenye rangi ya kijani, nayo ni madda inayo itwa "Chlorophyl". Hiyo Klorofil ni lazima kuwepo kwa ajili ya kujenga chakula kwa msaada wa mwangaza wa jua, na kuweza kuukuza mmea na kutoa matunda na mbegu nyengine.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na Allah Mtukufu, kutakasika na sifa za pungufu ni Kwake, Ndiye Aliyeteremsha mvua kutoka kwenye mawingu, Akatoa kwayo mimea ya kila kitu, Akatoa, kutokana na mimea, nafaka na miti mibichi, kisha akatoa kwenye mimea ya nafaka mbegu zilizoshikana, kama masuke ya mahindi, ngano na mpunga. Na Akatoa kutoka kwenye kizao cha mtende, nacho ni kile ambacho karara la tende linachomoza hapo, mitungo ambayo kuichuma ni karibu. Na Akatoa, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, mashamba ya mizabibu. Na Akatoa mizaituni na mikomamanga ambayo majani yake yanafanana na matunda yake yanatafautiana kimaumbile, utamu na kitabia. Angalieni, enyi watu, matunda ya mimea hii inapotoa mazao na kuiva kwake na kustawi kwake yanapostawi. Hakika katika hayo, enyi watu, kuna dalili ya ukamilifu wa uwezo wa muumba vitu hivi, hekima Yake na rehema Yake kwa watu wenye kumuamini Yeye, Aliyetukuka, na kuzifuata sheria Yake kivitendo.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-An'aam

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net