Al-An'aam 6:34
الأنعاموَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُوا۟ عَلَىٰ مَا كُذِّبُوا۟ وَأُوذُوا۟ حَتَّىٰٓ أَتَىٰهُمْ نَصْرُنَا ۚ وَلَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَـٰتِ ٱللَّهِ ۚ وَلَقَدْ جَآءَكَ مِن نَّبَإِى۟ ٱلْمُرْسَلِينَ
Na hakika walikadhibiwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia kule kukanushwa, na kuudhiwa, mpaka ilipowafikia nusura yetu. Na hakuna wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu. Na hakika imekwishakujia katika habari za Mitume hao.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na hakika walikanushwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia kule kukanushwa, na kuudhiwa, mpaka ilipo wafikia nusura yetu. Na hapana wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka zimekujia baadhi ya khabari za Mitume hao. [34]
[34] Na hakika Mitume wa kabla yako walikabiliwa na ukanushi na maudhi kutokana na kaumu zao, kama walivyo kufanyia wewe kaumu yako. Nao wakasubiri juu ya kukanushwa na kuudhiwa, mpaka tulipo wanusuru. Basi nawe subiri kama walivyo subiri wao, mpaka ikujie nusura yetu. Wala hapana la kugeuza ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwa atawanusuru wenye kusubiri. Lazima hayo yatimie. Na Sisi tumekusimulia kutokana na khabari za hao Mitume, na tulivyo waunga mkono. Ndani ya hayo mna maliwaza yako, na maelezo kuwa yeyote mwenye kuchukua Ujumbe lazima ahimili kila namna ya shida.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Hakika makafiri waliwakanusha Mitume kabla yako Aliowatuma Allah Mtukufu, Aliyetukuka, kwa umma wao. Wao waliudhiwa katika kufuata njia Yake na wakasubiri juu ya hilo na wakaendelea katika ulinganizi wao na bidii yao mpaka ikawajia nusura ya Allah Mtukufu. Na hakuna mwenye kuyageuza maneno ya Allah Mtukufu, nayo ni yale Aliyoyateremsha kwa Nabii Wake Muhammad, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie,) yenye ahadi Yake kwamba Atampa ushindi juu ya wanaomfanyia uadui. Na hakika imekujia wewe, ewe Mtume, habari ya Mitume waliokuwa kabla yako na nusura ya Allah Mtukufu iliyohakikishika kwao na mateso ya Allah Mtukufu na ghadhabu Zake zilizowafikia wenye kuwakanusha. Basi wewe una kielezo chema na mfano wa kuigwa kutoka kwa Mitume waliotangulia. Katika hili pana kumliwaza Mtume, (rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie).
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net