Al-An'aam 6:19
الأنعامقُلْ أَىُّ شَىْءٍ أَكْبَرُ شَهَـٰدَةً ۖ قُلِ ٱللَّهُ ۖ شَهِيدٌۢ بَيْنِى وَبَيْنَكُمْ ۚ وَأُوحِىَ إِلَىَّ هَـٰذَا ٱلْقُرْءَانُ لِأُنذِرَكُم بِهِۦ وَمَنۢ بَلَغَ ۚ أَئِنَّكُمْ لَتَشْهَدُونَ أَنَّ مَعَ ٱللَّهِ ءَالِهَةً أُخْرَىٰ ۚ قُل لَّآ أَشْهَدُ ۚ قُلْ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَٰحِدٌ وَإِنَّنِى بَرِىٓءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ
Sema: Ni kitu gani ushahidi wake ndio mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na imefunuliwa kwangu Qur-ani hii ili kwayo niwaonye nyinyi na kila inayemfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami hakika niko mbali na mnaowashirikisha.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha. [19]
[19] Ewe Nabii! Waambie hao wanao kukanusha na wanao taka ushahidi wa Utume wako: Kitu gani chenye ushahidi mkubwa, na chenye kustahiki kusadikiwa kuliko vyote? Kisha uwambie: Hakika Mwenyezi Mungu ndiye shahidi mkubwa kushinda wote wa kushuhudia baina yangu na nyinyi katika ukweli wa haya ninayo kuleteeni. Na Yeye ndiye aliye iteremsha hii Qur'ani ili iwe ni hoja ya ukweli wangu, nipate kukuhadharisheni nyinyi na kila itakayo mfikia khabari yake. Nayo ni hoja ya kukata, inayo shuhudia ukweli wangu. Kwani nyinyi hamwezi kuleta mfano wake! Waulize: Hivyo nyinyi mnaitakidi kuwa Mwenyezi Mungu ana miungu wenziwe? Kisha uwambie: Mimi sishuhudii hayo, wala sisemi hivyo, wala sikukubalieni kwa hayo. Hapana shaka wa kuabudiwa kwa haki ni Mungu Mmoja. Na mimi ni mbali kabisa na hayo masanamu mnayo mshirikisha Naye.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Ni kitu gani chenye ushahidi zaidi katika kuthibitisha ukweli wangu katika haya ninayowaambia kwamba mimi ni Mtume wa Allah Mtukufu?» Sema, «Allah Mtukufu ni shahidi baina yangu mimi na nyinyi.» Yaani: yeye Ndiye Mjuzi wa niliyokuja nayo kwenu na yale mtakayoniambia. «Na Allah Mtukufu Ameniletea mimi Qur’ani hii kwa njia ya wahyi ili ni waonye nayo adhabu ya Allah Mtukufu isiwashukie, na niwaonye nayo ummah wengine ambao itawafikia.» Nyinyi mnakubali kwamba, pamoja na Allah Mtukufu, pana waabudiwa wengine mnaowashirikisha Naye. Waambie, ewe Mtume, «Mimi sitoi ushahidi juu ya lile mlilolikubali. Hakika Allah Mtukufu ni Mola mmoja Asiye na mshirika. Na mimi nimejiepusha na kila mshirika mnayemuabudu pamoja na Yeye».
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net