Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 6 · Aya ya 157

Al-An'aam 6:157

الأنعام

أَوْ تَقُولُوا۟ لَوْ أَنَّآ أُنزِلَ عَلَيْنَا ٱلْكِتَـٰبُ لَكُنَّآ أَهْدَىٰ مِنْهُمْ ۚ فَقَدْ جَآءَكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ ۚ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَّبَ بِـَٔايَـٰتِ ٱللَّهِ وَصَدَفَ عَنْهَا ۗ سَنَجْزِى ٱلَّذِينَ يَصْدِفُونَ عَنْ ءَايَـٰتِنَا سُوٓءَ ٱلْعَذَابِ بِمَا كَانُوا۟ يَصْدِفُونَ

Maana

Au mkasema: "Lau hakika sisi tungeteremshiwa Kitabu hicho, basi tungelikuwa waongofu zaidi kuwaliko wao." Basi hakika imekwishawajia hoja iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uongofu, na rehema. Kwa hivyo, ni nani aliye dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule anayekadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa wale wanaojitenga na Ishara zetu adhabu mbaya kabisa kwa sababu ya walivyokuwa wakijitenga.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Au mkasema: Lau kuwa tumeteremshiwa sisi Kitabu tungeli kuwa waongofu zaidi kuliko wao. Basi imekufikieni bayana kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu, na rehema. Basi nani aliye dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa wanao jitenga na Ishara zetu adhabu kali kabisa kwa sababu ya kujitenga kwao. [157]

[157] Na Sisi tumeiteremsha Qur'ani ili wasiseme pia: Lau kuwa sisi tumeteremshiwa ufunuo kama walivyo teremshiwa wao, tungeli washinda kwa uwongofu, na hali yetu ingeli kuwa bora zaidi, kwa sababu ya akili zetu ni pana zaidi na sisi tumetengenea vizuri! Baada ya hii leo hamna hoja ya kuasi kwenu. Wala hapana udhuru wa kauli yenu hii. Kwani Qur'ani imekujieni kutoka kwa Mola Mlezi wenu, nayo ni alama iliyo wazi ya ukweli wa Muhammad. Inabainisha yote mnayo yahitajia katika Dini yenu na dunia yenu. Inakuongoeni kwenye Njia iliyo sawa, na rehema kwenu kuifuata. Na hapana mwenye kudhulumu zaidi kuliko huyo anaye zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu alizo ziteremsha katika Vitabu vyake, na Ishara zake alizo ziumba katika ulimwengu, naye akazipuuza na asiziamini, na wala asizitende! Na Sisi tutawaadhibu hao wanao zikataa Ishara zetu, wala hawazingatii adhabu yenye mwisho wa uchungu, kwa sababu ya kukataa kwao na kuacha kuzingatia kwao.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na ili msije mkasema, enyi washirikina, «Lau kama sisi tungetereshiwa kitabu kutoka mbinguni, kama walivyoteremshiwa Mayahudi na Wanaswara, tungalikuwa na muelekeo madhubuti sana kwenye njia ya haki kuliko wao.» Hakika kimewajia Kitabu kwa lugha ya Kiarabu chenye ufafanuzi. Na hiyo ni hoja iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu, ni muongozo wa njia ya haki na ni rehema kwa umma huu. Na hapana yoyote mbaya wa dhuluma na uadui kuliko yule aliyezikanusha hoja za Allah Mtukufu, Aliyetukuka, na akazipa mgongo. Basi hawa wenye kupa mgongo tutawatesa mateso makubwa kwenye Moto wa Jahanamu, kwa sababu ya kuzipa mgongo kwao aya zetu na kuzuia kwao njia zetu.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-An'aam

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net