Al-An'aam 6:152
الأنعاموَلَا تَقْرَبُوا۟ مَالَ ٱلْيَتِيمِ إِلَّا بِٱلَّتِى هِىَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُۥ ۖ وَأَوْفُوا۟ ٱلْكَيْلَ وَٱلْمِيزَانَ بِٱلْقِسْطِ ۖ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَإِذَا قُلْتُمْ فَٱعْدِلُوا۟ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ ٱللَّهِ أَوْفُوا۟ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّىٰكُم بِهِۦ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ
Wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa kile kilicho kizuri kabisa mpaka afike utu uzima wake. Na timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu. Hatuibebeshi nafsi isipokuwa kwa uwezo wake. Na mnaposema, basi fanyeni uadilifu hata kama ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu, itimizeni. Hayo amewausia ili mkumbuke.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Wala msiyakaribie mali ya yatima ila kwa njia ya wema kabisa, mpaka afikilie utu-uzima. Na timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu. Sisi hatumkalifishi mtu ila kwa kadiri ya uwezo wake. Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu itekelezeni. Hayo amekuusieni ili mpate kukumbuka. [152]
[152] Wala msiyatumie mali ya yatima ila kwa njia iliyo bora kabisa ya kuyahifadhi na kuyakuza. Na endeleeni hivyo mpaka huyo yatima afike umri wa uwongofu, atapo weza mwenyewe kuendesha mambo yake baraabara. Hapo tena ndio mpeni mali yake. Wala msipunje vipimo na mizani kwa kupunguza mnapo toa, au kuongeza mnapo chukua. Bali pimeni kwa uadilifu kama muwezavyo. Na Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi ila kwa kadiri iwezavyo bila ya karaha. Na mkisema neno katika kuhukumu, au ushahidi, au khabari, au mfano wa hayo, basi msikengeuke mkaacha uadilifu na ukweli. Bali hakikisheni kusema sawa, bila ya kuzingatia makhusiano ya jinsi, yaani uke na ume, au rangi, au ujamaa au ushemeji. Wala msitengue ahadi za Mwenyezi Mungu alizo chukua kwenu kwa taklifu, wala ahadi zilio baina yenu wenyewe kwa wenyewe, katika mambo yaliyo fungamana na maslaha yaliyo ruhusiwa kisharia. Bali timizeni ahadi hizi zote. Mwenyezi Mungu amekuamrisheni kwa kutilia mkazo mjitenge na yaliyo katazwa, na mkumbuke kuwa Sharia ni kwa ajili ya maslaha yenu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Wala msiyasogelee, enyi wasimamizi, mali ya yatima isipokuwa kwa namna ya kuyatengeneza na kuyafanya yenye faida, mpaka atakapofikia miaka ya kubaleghe na awe mwangalifu. Na pindi afikiapo umri huo, mpeni mali yake. Na tekelezeni vipimo na mizani kwa usawa kwa namna ambayo utekelezaji utakuwa umefanyika kwa ukamilifu. Na mtakapojibidiisha uwezo wenu, hapana ubaya kwenu katika yale ambayo huenda yakawa na upungufu upande wenu. Kwani hatumlazimishi mtu isipokuwa uwezo wake. Na msemapo, basi jitahidini katika maneno yenu kuchunga usawa pasi na kupotoka kwenye haki kwenye utoaji habari au ushahidi au hukumu au kwenye uombezi, hata kama yule ambaye neno hilo linamuhusu yeye ana ujamaa na nyinyi, msilemee upande wake bila ya haki. Na tekelezeni yale aliyowaagiza mfanye ya kujilazimisha na sheria Yake. Hukumu hizo mlizosomewa, Mola wenu Amewausia mzifuate kwa matarajio kwamba mkumbuke mwisho wa mambo yenu.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net