Al-An'aam 6:151
الأنعامقُلْ تَعَالَوْا۟ أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا۟ بِهِۦ شَيْـًٔا ۖ وَبِٱلْوَٰلِدَيْنِ إِحْسَـٰنًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوٓا۟ أَوْلَـٰدَكُم مِّنْ إِمْلَـٰقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا۟ ٱلْفَوَٰحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا۟ ٱلنَّفْسَ ٱلَّتِى حَرَّمَ ٱللَّهُ إِلَّا بِٱلْحَقِّ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّىٰكُم بِهِۦ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ
Sema: Njooni niwasomee yale aliyowaharamishia Mola wenu Mlezi: Kwamba msimshirikishe Yeye na chochote, na wazazi wawili wafanyieni uzuri, wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunawaruzuku nyinyi na wao. Wala msikaribie machafu, yaliyo dhahiri yake, na yaliyofichikana yake. Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu aliiharamisha isipokuwa kwa haki. Hayo aliwausia ili myatie akilini.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola wenu Mlezi. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayo onekana, na yanayo fichikana. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini. [151]
[151] Ewe Nabii! Waambie: Njooni nikubainishieni yaliyo haramu ambayo inatakikana mshughulike nayo, na mjitenge nayo. Msimfanye yeyote kuwa ni mshirika na Mwenyezi Mungu, kwa shirki ya namna yoyote. Wala msiwafanye uovu wazazi wenu, bali wafanyieni wema mwisho wa wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya kukufikieni ufakiri, au mnao ogopa usikufikieni siku za usoni. Kwani nyinyi sio mnao toa riziki. Bali Sisi ndio tunakuruzukuni nyinyi na tunawaruzuku wao. Wala msikaribie uchafu wa uzinzi, kwani huo ni katika mambo mabaya yanayo katazwa, sawa sawa ikiwa jahara au kwa siri asiyo iona ila Mwenyezi Mungu. Wala msiuwe nafsi yoyote aliyo kataza Mwenyezi Mungu kuiuwa kwa kutokuwapo kupasa kwake, ila ikiwa kuuwa huko ni kwa haki ya kutekeleza hukumu ya mahkama. Mwenyezi Mungu amekuamrisheni kwa amri ya nguvu muepuke haya yaliyo katazwa ambayo akili ya maumbile inakwambieni muepukane nayo, ili nanyi myatie akilini hayo.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Waambie, ewe Mtume, Njooni niwasomee Yale Aliyoyaharamishia Allah Mtukufu: Msishirikishe pamoja na Allah Mtukufu kitu chochote, miongoni mwa viumbe Vyake katika kumuabudu Yeye; bali zielekezeni aina zote za ibada Kwake Yeye Peke Yake, kama kuogopa, kutaraji, kuomba na megineyo. Muwafanyie wema wazazi wawili kwa kuwasaidia, kuwaombea Mungu na mengineyo ya wema kama hayo Msiwaue watoto wenu kwa sababu ya ufukara uliowashukia, kwani Allah Mtukufu Anawaruzuku nyinyi na wao. Wala msiyasongelee madhambi makubwa yaliyo wazi na yaliyofichika. Na msiiue nafsi ambayo Allah Mtukufu Ameharamisha kuuawa, isipokuwa kwa njia ya haki, nayo ni kuchukuliwa kisasi kwa aliyeua, au kwa uzinifu baada ya kuoa au kuolewa, au kuacha Uislamu. Hayo yaliyotajwa ni miongoni mwa yale ambayo Allah Mtukufu amewakataza nayo na Akawapa maagizo muyaepuke na ni miongoni mwa yale Aliyowaamrisha nyinyi kwayo. Amewausia nayo Mola wenu ili mpate kuyatia akilini maamrisho Yake na Makatazo Yake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net