Al-An'aam 6:145
الأنعامقُل لَّآ أَجِدُ فِى مَآ أُوحِىَ إِلَىَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُۥٓ إِلَّآ أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُۥ رِجْسٌ أَوْ فِسْقًا أُهِلَّ لِغَيْرِ ٱللَّهِ بِهِۦ ۚ فَمَنِ ٱضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ رَبَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ
Sema: Sipati katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa ikiwa ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani huo ni uchafu; au kilichovukiwa mipaka (wakati wa kuchinjwa) kwa kutajiwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipo kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. [145]
[145] Ewe Nabii! Sema: Hivi sasa sipati katika panapo toka mambo ya kuhalalisha na kuharimisha katika niliyo funuliwa mimi wahyi juu ya chakula kilicho harimishwa kula mlaji, isipo kuwa kitu hicho kiwe ni nyamafu, kimekufa na hakikuchinjwa kwa njia za sharia; au damu inayo tiririka, au nyama ya nguruwe - kwani hivyo vilivyo tajwa vinadhuru, na vichafu, havijuzu kula. Na pia katika vitu vilivyo harimishwa kula vinavyo toka katika itikadi sahihi, kwa kuwa wakati wa kuchinjwa lilitajwa jina lisilo kuwa la Mwenyezi Mungu, kama sanamu au muabudiwa mwenginewe! Juu ya hivyo mwenye kulazimika kwa dharura kula kitu katika hivi vilivyo harimishwa, bila ya kuwa anatafuta utamu tu wa kula, na bila ya kupita mpaka wa ile dharura, basi huyo hana dhambi. Kwa sababu Mola wako Mlezi ni Mwenye kughufiria, na Mwenye kurehemu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Sema, ewe Mtume, mimi sipati, kati ya yale aliyoniletea wahyi Allah Mtukufu, kitu kilicho haramu kwa mwenye kukila, kati ya vile mnavyovitaja kwamba vimeharamishwa miongoni mwa wanyama howa, isipokuwa awe amekufa bila kuchinjwa, au ni damu itiririkayo, au iwe ni nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni najisi, au akawa ni mnyama ambaye kuchinjwa kwake kumetoka nje ya utiifu wa Allah Mtukufu, Aliyetukuka, kama akiwa mnyama aliyechinjwa ametajiwa jina la asiyekuwa Allah Mtukufu, wakati wa kuchinjwa. Basi mwenye kulazimika kula chochote kati ya hizo zilizoharamishwa kwa dharura ya njaa kali, pasi na kutaka kujifurahisha wala kukiuka mpaka wa dharura, hakika Allah Mtukufu, Aliyetukuka, ni mwenye kumsamehe, ni mwenye huruma naye. Na hakika imethibiti, baadaye, kwa mafundisho ya Mtume kuwa ni haramu kula kila mnyama mwitu anayewinda kwa kutumia meno, kila ndege anayewinda kwa kutumia kucha, punda na mbwa.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net