Al-An'aam 6:137
الأنعاموَكَذَٰلِكَ زَيَّنَ لِكَثِيرٍ مِّنَ ٱلْمُشْرِكِينَ قَتْلَ أَوْلَـٰدِهِمْ شُرَكَآؤُهُمْ لِيُرْدُوهُمْ وَلِيَلْبِسُوا۟ عَلَيْهِمْ دِينَهُمْ ۖ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ مَا فَعَلُوهُ ۖ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ
Na kadhalika hao washirika wao wamewapambia wengi katika washirikina kuwaua watoto wao ili kuwaangamiza na kuwachanganyia dini yao. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelifanya hayo. Basi waache na hayo wanayozua ya uongo.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na kadhaalika hao washirika wao wamewapambia wengi katika washirikina kuwauwa watoto wao ili kuwaangamiza na kuwavurugia dini yao. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli penda wasinge fanya hayo. Basi waache na hayo wanayo yazua. [137]
[137] Kama ilivyo kuwa hayo mawazo yao yalivyo wapambia huo mgawanyo wa dhulma katika mazao ya mimea, na ngamia, na ng'ombe, na kondoo, alio umba Mwenyezi Mungu, basi kadhaalika mawazo yao yamewapambia, kutokana na hayo masanamu ambayo wanadai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, kuwauwa watoto wao pale wanapo zaliwa, na kuwa ati waliweka nadhiri kwa miungu yao kuwachinja watoto wao! Na hakika hayo mawazo yao yanawaangamiza na yanawavurugia mambo ya dini, kwa hivyo hawaielewi vilivyo! Na ilivyo kuwa mawazo yao yamezisaliti akili zao hadi hiyo, basi wewe waachilie mbali wao na hayo wanayo mzulia Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kukuzulia wewe. Nao watakuja pata malipo ya huo uzushi wao. Na hayo ndio matakwa ya Mwenyezi Mungu, kwani angeli taka wasingeli fanya hayo.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na kama ambavyo mashetani waliwapambia washirikina wamtengee Allah Mtukufu, Aliyetukuka, katika mazao na wanyama howa, fungu maalumu na fungu kwa washirika wao, vilevile mashetani wamewapambia wengi kati ya washirikina kuwaua watoto wao kwa kuchelea ufukara, ili wawaingize wazazi hawa kwenye maangamivu kwa kuziua nafsi ambazo Allah Mtukufu Ameharamisha kuuliwa isipokuwa kwa haki, na ili wawavurugie dini yao iwachanganyikie wapate kupotea na waangamie. Na lau Angalitaka Allah Mtukufu wasifanye hilo hawangalilifanya, lakini Yeye Amelikadiria liwe kwa kujua Kwake uovu wa hali yao na marejeo yao. Basi waache, ewe Mtume, na mambo yao, katika yale ya urongo wanayoyazua, na Allah Mtukufu Atahukumu baina yako na wao.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net