Al-Maaida 5:97
المائدةجَعَلَ ٱللَّهُ ٱلْكَعْبَةَ ٱلْبَيْتَ ٱلْحَرَامَ قِيَـٰمًا لِّلنَّاسِ وَٱلشَّهْرَ ٱلْحَرَامَ وَٱلْهَدْىَ وَٱلْقَلَـٰٓئِدَ ۚ ذَٰلِكَ لِتَعْلَمُوٓا۟ أَنَّ ٱللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِى ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَمَا فِى ٱلْأَرْضِ وَأَنَّ ٱللَّهَ بِكُلِّ شَىْءٍ عَلِيمٌ
Mwenyezi Mungu ameifanya Al-Kaaba, hii Nyumba Tukufu, kuwa ya kuwakimu watu, na Miezi Mitakatifu, na dhabihu walioletwa Makka kama zawadi, na dhabihu waliofungwa vigwe. Hayo ni ili mjue ya kwamba hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika mbingu na yaliyo katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Mwenyezi Mungu ameifanya Al Kaaba, hii Nyumba Tukufu, ni simamio la watu, na kadhaalika Miezi Mitukufu, na wanyama wa dhabihu, na vigwe. Hayo ili mjue ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. [97]
[97] Mwenyezi Mungu ameijaalia Al Kaaba, nayo ni hiyo nyumba aliyo itukuza na akaharimisha watu na wanyama kufanyiwa uadui ndani yake na karibu yake, ameijaalia kuwa yenye kusimama na yenye kutukuzwa, na yenye kuwapa amani watu, na iwe ndiyo Kibla cha kuelekea watu katika Swala zao, na watu waiendee kwa Hija wawe ni wageni wa Mwenyezi Mungu, na ili watende yale ya kuupa nguvu umoja wao. Hali kadhaalika ameufanya mwezi wa Hija na wanyama wanao tolewa dhabihu, na khasa wale wanao vishwa vigwe ili watambuliwe na wanao waona kuwa hao wametolewa hidaya kwenye hiyo Nyumba. Na natija ya kuweka yote hayo ni kuwa mpate kuyakinika kuwa ujuzi wake Mwenyezi Mungu umeenea kila kitu kilioko mbinguni kunakotoka wahyi (ufunuo) wa sharia, na umeenea duniani, anako weka sharia ya kuwaletea watu maslaha yao. Na hakika ujuzi wa Mwenyezi Mungu umeenea juu ya kila kitu.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Allah Mtukufu Amewafadhili waja Wake kwa kuijaalia Alkaba, Nyumba takatifu, ni utengenefu wa Dini yao na amani ya uhai wao. Hivyo ni kwa kuwa wamemuamini Allah Mtukufu na Mtume Wake na wakasimamisha faradhi Zake. Na Ameharamisha uadui na kupigana katika miezi mitakatifu (nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungone na Rajabu) ili mtu yoyote asimfanyie mwingine uadui katika miezi hiyo. Na Ameharamisha, kuwavamia wanyama howa wanaotolewa kuwa ni tunu kwa Haram. Kadhalika, Ameharamisha kuvivunjia heshima qalãid, navyo ni vitu vilivyovishwa shingoni mwa hao wanyama kuonyesha kuwa wanakusudiwa kuchinjwa kwa ibada. Hivyo basi, ni mupate kujua kuwa Allah Mtukufu Anayajua yote yaliyo mbinguni na ardhini, miongoni mwayo ni sheria Alizoziweka kuwahami viumbe Wake wasidhuriane wao kwa wao. Na pia mupate kujua kwamba Allah Mtukufu kwa kila kitu ni Mjuzi, hakuna chochote chenye kufichika Kwake.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net