Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 89

Al-Maaida 5:89

المائدة

لَا يُؤَاخِذُكُمُ ٱللَّهُ بِٱللَّغْوِ فِىٓ أَيْمَـٰنِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ ٱلْأَيْمَـٰنَ ۖ فَكَفَّـٰرَتُهُۥٓ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَـٰكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَـٰثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّـٰرَةُ أَيْمَـٰنِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚ وَٱحْفَظُوٓا۟ أَيْمَـٰنَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ ٱللَّهُ لَكُمْ ءَايَـٰتِهِۦ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

Maana

Mwenyezi Mungu hawachukulii dhambi kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atawachukulia dhambi kwa mnavyoapa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnachowalisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Na asiyepata, basi na afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini viapo vyenu. Namna hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kushukuru.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kushukuru. [89]

[89] Mwenyezi Mungu hakutiini adabu kwa sababu ya kuapa kiapo msicho kusudia. Bali hakika Yeye hukutieni adabu kwa sababu ya kuvunja viapo mlivyo vikusudia na yamini mliyo jifunga nayo. Basi ikiwa mmevunja kiapo itakupaseni mfanye jambo la kukughufirieni dhambi zake. Na mambo yenyewe ni: kuwalisha mafakiri kumi kwa siku moja, kwa chakula cha kawaida mnacho kila nyinyi na jamaa zenu mnao waangalia, yaani watu wenu wa nyumbani bila ya israfu wala ubakhili. Au kuwavika mafakiri kumi kwa kivazi kilicho zowewa. Au kumkomboa mtu kutoka utumwani. (Na mfano wa mtumwa ni mtu alioko kifungoni kwa dhulma, au chini ya utawala wa dhulma.) Ikiwa mwenye kuapa hawezi kutenda lolote katika hayo, basi itampasa afunge siku tatu. Na kila moja katika mambo haya hufuta dhambi za mwenye kuapa kiapo cha kutilia niya na akakivunja. Nanyi zilindeni yamini zenu, msiape katika mambo yasiyo kuwa laiki yake, na wala msiache kutenda kitendo cha kughufiria dhambi pindi mkivunja kiapo. Kwa mpango huu Mwenyezi Mungu anakufafanulieni hukumu zake ili mpate kushukuru neema zake kwa kuzijua na kuzifuata vilivyo. Katika hukumu ya yamini pana mawili yafaa tuyazingatie. Kwanza: Uislamu umeraghibisha sana kukomboa watumwa. Sababu nyingi zinazo wajibisha hayo. Kafara nyingi za dhambi zinahitaji kukomboa. Kafara ya kula mchana Ramadhani yahitaji ukombozi, n.k. Na katika hayo yanaonyesha Uislamu unachukia utumwa. Uislamu uliukiri utumwa kwa kuwa maadui wao walikuwa wakiwatia utumwani Waislamu, basi na Uislamu ukaruhusu kuwatendea wao vivyo hivyo. Pili: Uislamu unakazania kulisha masikini kila ikipatikana fursa.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Allah Mtukufu Hatawapa mateso, enyi Waislamu, kwa mayamini mliyoapa bila ya kukusudia, mfano wa vile baadhi yenu wanavyosema, «Sivyo, naapa kwa Allah Mtukufu», «Kwa Nini? Naapa kwa Allah Mtukufu.» Lakini Yeye Atawapa mateso, kwa sababu ya mayamini mliyoyakusudia ndani ya nyoyo zenu. Basi mkiwa hamtekelezi yamini, dhambi lake litafutwa na Allah Mtukufu, kwa kafara mtakayotoa mliyowekewa na Allah Mtukufu ya kuwalisha masikini kumi, kila masikini mmoja apewe nusu ya pishi[kadiri ya kilo mbili na nusu] ya chakula cha kati na kati kinachotumiwa na watu wa mji aliyoko, au kuwavisha kwa kumpa kila maskini mavazi yanayomtosha kulingana na desturi, au kuacha huru mmilikiwa kumtoa kwenye utumwa. Basi mwenye kuapa ambaye hakutekeleza yamini lake ana hiari afanye mojawapo ya mambo matatu. Asipopata chochote kati ya hayo, ni juu yake afunge siku tatu. Kufanya hayo ndio kafara ya kutoyatekeleza mayamini yenu. Na yachungeni mayamini yenu, enyi Waumini, kwa kujiepusha na kuapa au kutekeleza kiapo mnapoapa au 1 Neno la kiarabu hapa ni murãqabah lenye maan kuchunga, kulinda n.k. Makusudio hapa ni kuwa n akusikia na azijua harakati zako zote, yakini am Mtukufu.Kwa maelezo zaidi, ang. ‘Uthaimîn,M.S kutoa kafara msipotekeleza kiapo. Na kama alivyowaelezea Allah Mtukufu hukumu ya mayamini na namna ya kujivua nayo, ndivyo Anavyowaelezea hukumu za dini Yake, ili mumshukuru Yeye kwa kuwaongoza nyinyi kwenye njia iliyolingana sawa.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net