Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 8

Al-Maaida 5:8

المائدة

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ كُونُوا۟ قَوَّٰمِينَ لِلَّهِ شُهَدَآءَ بِٱلْقِسْطِ ۖ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَـَٔانُ قَوْمٍ عَلَىٰٓ أَلَّا تَعْدِلُوا۟ ۚ ٱعْدِلُوا۟ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ خَبِيرٌۢ بِمَا تَعْمَلُونَ

Maana

Enyi mlioamini! Kuweni wasimamao madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wenye kushuhudia kwa haki. Na wala kamwe kusiwapelekee kuchukiana na watu kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndivyo kuwa karibu mno na ucha Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. [8]

[8] Enyi Waumini! Jitahidini kutimiza haki za Mwenyezi Mungu, na shuhudieni kwa haki baina ya watu. Chuki zenu kubwa kwa watu fulani zisikupelekeeni mkaacha kuwafanyia uadilifu. Bali jilazimisheni uadilifu, kwani hiyo ndiyo njia ya kupelekea kumcha Mwenyezi Mungu, na kuepukana na ghadhabu yake. Na mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote; kwani Yeye, Sub hanahu, anayajua vilivyo yote mnayo yafanya, naye atakulipeni kwayo. Uislamu unalingania uadilifu moja kwa moja, sawa kwa rafiki na adui.Haifai chuki ikakupelekea kudhulumu. Na hayo unapo amiliana na watu, na kuamiliana baina ya dola ya Kiislamu na dola nyenginezo. Na kumfanyia uadilifu adui kunaambiwa na Qur'ani kuwa ni karibu zaidi na uchamngu na usafi wa kidini. Lau kuwa wasia huu ungeli tumiwa katika sharia za baina ya madola basi pasingeli kuwapo vita. Kama kila dini ina kitambulisho chake na alama, basi kitambulisho cha Uislamu ni Dini ya Mungu Mmoja na Uadilifu.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi mliomuamini Allah Mtukufu na Mtume Wake Muhammad, rehema za Allah Mtukufu na amani zimshukie,, kuweni wasimamizi wa haki kwa ajili ya kuzitafuta radhi za Allah Mtukufu, muwe mashahidi kwa uadilifu. Wala kusiwapelekee nyinyi kuwachukia watu kuacha kufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu baina ya maadui na vipenzi kwa daraja moja sawasawa. Kufanya uadilifu huko kuko karibu zaidi na kumuogopa Allah Mtukufu. Na jihadharini na kufanya udhalimu, hakika Allah Mtukufu ni Mtambuzi wa mnayoyafanya na Atawalipa kwa hayo.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net