Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 64

Al-Maaida 5:64

المائدة

وَقَالَتِ ٱلْيَهُودُ يَدُ ٱللَّهِ مَغْلُولَةٌ ۚ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا۟ بِمَا قَالُوا۟ ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَآءُ ۚ وَلَيَزِيدَنَّ كَثِيرًا مِّنْهُم مَّآ أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ طُغْيَـٰنًا وَكُفْرًا ۚ وَأَلْقَيْنَا بَيْنَهُمُ ٱلْعَدَٰوَةَ وَٱلْبَغْضَآءَ إِلَىٰ يَوْمِ ٱلْقِيَـٰمَةِ ۚ كُلَّمَآ أَوْقَدُوا۟ نَارًا لِّلْحَرْبِ أَطْفَأَهَا ٱللَّهُ ۚ وَيَسْعَوْنَ فِى ٱلْأَرْضِ فَسَادًا ۚ وَٱللَّهُ لَا يُحِبُّ ٱلْمُفْسِدِينَ

Maana

Na Mayahudi walisema: 'Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba.' Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyoyasema. Bali mikono yake iko wazi. Hutoa apendavyo. Kwa yakini yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na kufuru. Na Sisi tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Kiyama. Kila mara wanapowasha moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndiyo iliyo fumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyo yasema. Bali mikono yake iwazi. Hutoa apendavyo. Kwa yakini yaliyo teremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidisha wengi katika wao uasi na kufuru. Na Sisi tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Kiyama. Kila mara wanapo washa moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu. [64]

[64] Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba, haukukunjuka ukatoa! Mwenyezi Mungu ameifumba mikono yao wao, na amewatenga mbali na rehema yake! Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, anajitosha. Yeye hutoa apendavyo. Na hakika wengi wa watu kwa kupita kiasi katika upotovu wao, haya yalio teremka kwako huwazidisha udhalimu na ukafiri, kwa sababu ya chuki na husda yao. Na Sisi tumetia baina yao kwa wao uadui na bughdha mpaka Siku ya Kiyama. Kila wanapo washa moto kumpiga vita Mtume na Waumini, Mwenyezi Mungu huuzima kwa kumpa ushindi Nabii wake na wafuasi wake. Na wao wanajitahidi kueneza fisadi katika nchi, na kufanya vitimbi, na kutia fitina, na kuchochea vita. Na Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Allah Mtukufu Anamjulisha Mtume Wake sehemu ya makosa ya Mayahudi, kitu walichokuwa wakikizungumza kwa siri baina yao, kuwa wao walisema, «Mkono wa Allah Mtukufu umefungwa kutotenda mema, Ametufanyia ubahili riziki kwa kutubania na kutotupanulia.» Walisema hilo wakati walipopatwa na ukame na ukosefu wa mvua. Mikono yao ndiyo iliyofungwa, kwa maana: mikono yao imezuiliwa kutenda mema, na Allah Mtukufu Amewafukuza kutoka kwenye rehema Yake kwa sababu ya neno lao. Mambo sivyo kama wanavyomzulia Mola wao, bali mikono Yake miwili imekunjuliwa, haikuzuiliwa wala hakuna pingamizi ya kumzuia kutoa. Kwani Yeye ni Mpaji, ni Karimu, Anatoa kulingana na hekima na yale yenye maslahi kwa waja. Kwenye aya hii kuna thibitisho la sifa ya Mikono miwili kwa Allah Mtukufu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu na kutukuka, kama inavyolingana na Yeye, pasi na kufananisha wala kueleza namna ilivyo. Lakini wao watazidi ukiukaji mipaka na ukafiri kwa sababu ya chuki yao na uhasidi wao kwa kuwa Allah Mtukufu Amekuchagua wewe kuwa mtume. Allah Mtukufu Anayatolea habari makundi ya Mayahudi kwamba wao wataendelea, mpaka Siku ya Kiyama, kufanyiana uadui wao kwa wao na kuchukiana wao kwa wao. Kila wanapopanga njama ya kuwafanyia vitimbi Waislamu, kwa kuzusha fitina na kuuwasha moto wa vita, Allah Mtukufu Anavikomesha vitimbi vyao na kuutenganisha mkusanyiko wao. Na Mayahudi hawataacha kuendelea kumuasi Allah Mtukufu kwa kufanya yanayoleta uharibifu na misukosuko katika ardhi. Na Allah Mtukufu, Aliyetukuka, Hawapendi waharibifu.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net