Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 48

Al-Maaida 5:48

المائدة

وَأَنزَلْنَآ إِلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ بِٱلْحَقِّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلْكِتَـٰبِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ عَمَّا جَآءَكَ مِنَ ٱلْحَقِّ ۚ لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةً وَٰحِدَةً وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِى مَآ ءَاتَىٰكُمْ ۖ فَٱسْتَبِقُوا۟ ٱلْخَيْرَٰتِ ۚ إِلَى ٱللَّهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ

Maana

Na tulikuteremshia wewe Kitabu hiki kwa haki, kinachosadikisha yale yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha haki iliyokujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sheria yake na njia yake. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelitaka, angeliwafanya nyote umma mmoja, lakini ni ili awajaribu kwa yale aliyowapa. Basi yakimbilieni mambo ya heri. Kwa Mwenyezi Mungu ndiyo marejeo yenu nyote, kisha atawaambia yale mliyokuwa mkihitilafiana juu yake.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha Haki iliyo kujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka ange kufanyeni nyote umma mmoja, lakini ni kukujaribuni kwa aliyo kupeni. Basi shindaneni kwa mambo ya kheri. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo yenu nyote, na atakuja kuwaambieni yale mliyo kuwa mkikhitalifiana. [48]

[48] Na wewe, ewe Nabii, tumekuteremshia Kitabu kikamilifu, nacho ni Qur'ani, chenye kushikamana na haki katika hukumu zake zote na khabari zake, chenye kuwafikiana na kuthibitisha Vitabu vyetu vilivyo tangulia, na kinavishuhudia kuwa ni Vitabu vya Mwenyezi Mungu, na kinalinda yaliyo sahihi, kwa sababu hii Qur'ani haibadiliki. Basi hukumu baina ya Watu wa Kitabu, Mayahudi na Wakristo, wakikutaka uwahukumu kwa mujibu alivyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Wala katika hukumu yako usifuate matamanio yao na matakwa yao, usije ukapotoka ukaacha Haki iliyo kujia. Kila umma katika nyinyi watu, tumeujaalia kuwa na njia yake ya kuitambua Haki, na njia iliyo wazi ya Dini ya kuifuata. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka angeli kufanyeni nyote kundi moja lililo wafikiana, lenye mwendo mmoja, hazikhitalifiani njia zake za kupita kwa zama zote. Lakini Yeye amekujaalieni hivi ili iwe kama mtihani kwenu katika hizo Sharia alizo kupeni, atambulikane mwenye kut'ii na mwenye kuasi. Basi tumieni fursa hii, na mfanye haraka kuwania kutenda vitendo vya kheri. Kwani marejeo yenu nyote yatakuwa kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Hapo atakwambieni hakika ya hayo mliyo kuwa mkikhitalifiana, na kila mmoja wenu atalipwa kwa a'mali yake.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Na tumekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani. Na yote yaliyomo ndani yake ni haki, yanatoa ushahidi juu ya ukweli wa Vitabu kabla yake na kwamba –vitabu hivyo- vinatoka kwa Allah Mtukufu, hali ya kuuthibitisha usahihi uliomo, kuufafanua upotovu uliomo na kuzifuta baadhi ya sheria zake. Kwa hivyo, wahukumu kati ya wale Mayahudi wanaoshitakiana kwako kwa sheria zile ulizoteremshiwa katika hii Qur’ani, wala usiiepuke haki, ambayo Mweyezi Mungu Amekuamrisha uitumie, ukafuata matakwa yao na yale waliyoyazoea. Kwani kila kundi la watu tumewawekea sheria na njia iliyo wazi ya wao kuifuata. Na lau Allah Mtukufu Angalitaka, Angalizifanya sheria zenu kuwa ni moja, lakini Yeye, Aliyetukuka, Alizifanya zitafautiane ili awape mtihani, ili mtiifu na mwenye kuasi wajulikane waziwazi. Basi yakimbilieni yale yaliyo bora kwenu katika Makao Mawili yenu(duniani na Akhera), kwa kuyafuata yaliyomo kwenye Qur’ani kivitendo. Kwani mwisho wenu ni kurudi kwa Allah Mtukufu; huko Atawapa habari ya yale mliyokuwa mkitafautiana juu yake, na hapo Atamlipa kila mmoja kwa amali yake.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net