Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 44

Al-Maaida 5:44

المائدة

إِنَّآ أَنزَلْنَا ٱلتَّوْرَىٰةَ فِيهَا هُدًى وَنُورٌ ۚ يَحْكُمُ بِهَا ٱلنَّبِيُّونَ ٱلَّذِينَ أَسْلَمُوا۟ لِلَّذِينَ هَادُوا۟ وَٱلرَّبَّـٰنِيُّونَ وَٱلْأَحْبَارُ بِمَا ٱسْتُحْفِظُوا۟ مِن كِتَـٰبِ ٱللَّهِ وَكَانُوا۟ عَلَيْهِ شُهَدَآءَ ۚ فَلَا تَخْشَوُا۟ ٱلنَّاسَ وَٱخْشَوْنِ وَلَا تَشْتَرُوا۟ بِـَٔايَـٰتِى ثَمَنًا قَلِيلًا ۚ وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْكَـٰفِرُونَ

Maana

Hakika Sisi tuliiteremsha Taurati yenye uongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walionyenyekea Kiislamu, na wacha Mungu, na wanachuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwa maana walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu, nao wakawa ni mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali niogopeni Mimi. Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache. Na wasiohukumu kwa aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Hakika Sisi tuliteremsha Taurati yenye uwongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walio nyenyekea kiislamu, na wachamngu, na wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali niogopeni Mimi. Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache. Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri. [44]

[44] Hakika Sisi tumemteremshia Musa Taurati. Ndani yake mna uwongofu unao endea Haki, na mna bayana yenye kutoa mwangaza unao nawirisha hukumu wanazo zihukumia Manabii, na wale walio safisha nafsi zao kwa ajili ya Mola wao Mlezi, na wanazuoni wenye kufwata njia ya Manabii, na wale walio chukua ahadi kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu kisibadilishwe, kwa kukilinda na kushuhudia kuwa hicho ndiyo Haki. Basi msiwakhofu watu mnapo hukumu, na nikhofuni Mimi tu, Mimi Mola wenu Mlezi, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Wala msizibadilishe Aya zangu nilizo ziteremsha kwa thamani duni ya kutaka starehe ya dunia, kama vile mrungura au kutaka cheo! Na wote wasio hukumu kwa mujibu alivyo teremsha Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa makafiri.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Hakika tumeiteremsha Taurati. Ndani yake muna uongozi wa kumuepusha mtu na upotevu na ufafanuzi wa hukumu ambazo Mitume wamezitumia katika kuhukumu. Mitume ambao waliitii na kuikubali hukumu ya Allah Mtukufu kati ya Mayahudi na wasitoke nje ya hukumu Yake wala wasiipotoshe. Pia walihukumu, kutumia sheria hiyo, wafanyi ibada wa Kiyahudi na wasomi wao ambao wanawalea watu kwa sheria za Allah Mtukufu. Hilo ni kwamba Manabii wao waliwaamini kwa kuwapa majukumu ya kuifikisha Taurati, kukielewa Kitabu cha Allah Mtukufu na kukitumia. Na wacha-Mungu na wanavyuoni walikuwa ni mashahidi ya kwamba Manabii wao walihukumu kati ya Mayahudi kwa Kitabu cha Allah Mtukufu. Na Allah Mtukufu, Aliyetukuka, Anasema kuwaambia wasomi wa Kiyahudi na wanavyuoni wao, «Msiwaogope watu katika kupitisha hukumu yangu, kwani wao hawawezi kuwanufaisha nyinyi wala kuwadhuru. Lakini niogopeni, kwani mimi Ndiye Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru. Wala msichukue, kwa kuacha kuhukumu kwa sheria nilizoziteremsha, badali twevu.» Kwani kuhukumu kwa ambayo hayakuteremshwa na Allah Mtukufu ni katika vitendo vya makafiri. Na wenye kubadilisha hukumu ya Allah Mtukufu Aliyoiteremsha kwenye Kitabu Chake, wakaificha, wakaikana na wakahukumu kwa isiyokuwa hiyo wakiitakidi uhalali wake na kufaa kwake, basi hao ndio makafiri.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net