Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 110

Al-Maaida 5:110

المائدة

إِذْ قَالَ ٱللَّهُ يَـٰعِيسَى ٱبْنَ مَرْيَمَ ٱذْكُرْ نِعْمَتِى عَلَيْكَ وَعَلَىٰ وَٰلِدَتِكَ إِذْ أَيَّدتُّكَ بِرُوحِ ٱلْقُدُسِ تُكَلِّمُ ٱلنَّاسَ فِى ٱلْمَهْدِ وَكَهْلًا ۖ وَإِذْ عَلَّمْتُكَ ٱلْكِتَـٰبَ وَٱلْحِكْمَةَ وَٱلتَّوْرَىٰةَ وَٱلْإِنجِيلَ ۖ وَإِذْ تَخْلُقُ مِنَ ٱلطِّينِ كَهَيْـَٔةِ ٱلطَّيْرِ بِإِذْنِى فَتَنفُخُ فِيهَا فَتَكُونُ طَيْرًۢا بِإِذْنِى ۖ وَتُبْرِئُ ٱلْأَكْمَهَ وَٱلْأَبْرَصَ بِإِذْنِى ۖ وَإِذْ تُخْرِجُ ٱلْمَوْتَىٰ بِإِذْنِى ۖ وَإِذْ كَفَفْتُ بَنِىٓ إِسْرَٰٓءِيلَ عَنكَ إِذْ جِئْتَهُم بِٱلْبَيِّنَـٰتِ فَقَالَ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ مِنْهُمْ إِنْ هَـٰذَآ إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ

Maana

Na pale Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa mwana wa Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipokutia nguvu kwa Roho Mtakatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utu uzimani. Na nilivyokufunza kuandika na hekima na Taurati na Injili. Na ulipokuwa unatengeneza kutoka katika udongo kama umbo la ndege, kwa idhini yangu, kisha unapuliza ndani yake na linakuwa ndege kwa idhini yangu. Na ulipowaponya vipofu na wakoma kwa idhini yangu. Na ulipowafufua wafu kwa idhini yangu. Na nilipokukinga kutokana na Wana wa Israili ulipowajia na hoja zilizo wazi, na wakasema wale waliokufuru miongoni mwao: Haya si lolote isipokuwa uchawi ulio wazi!

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu!. [110]

[110] Na wakati huo, Mwenyezi Mungu atamwambia Isa mwana wa Maryamu miongoni mwa Mitume: Kumbuka neema niliyo kuneemesha wewe na mama yako katika dunia, nilipo kutia nguvu kwa Wahyi,(Ufunuo), na nikakutamkisha nawe ni mtoto mchanga ili kumuondolea tuhuma aliyo tuhumiwa mama yako, kama nilivyo kutamkisha nawe ni mtu mzima kwa ufunuo niliyo kufunulia; na nilipo kuneemesha kwa kukufunza kuandika, na nikakuwezesha kusema na kutenda yaliyo sawa, na nikakufunza Kitabu cha Musa na Injili niliyo kuteremshia wewe, na nikakuwezesha kutenda miujiza asiyo weza mtu mwingine kuitenda, ulipo tengeneza ndege kwa udongo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, ukapuliza akawa ndege aliye hai kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, si kwa uweza wako, na ukamponesha mtoto kipofu, na ukamponesha mkoma kwa idhini na uweza wa Mwenyezi Mungu, na yakawa kwa kupitia mikononi mwako makadara ya kufufuka maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na kudra yake, na pale nilipo wazuia Mayahudi wasikuuwe na kukusalibu nilipo waletea miujiza wapate kuamini, nao baadhi yao walikanya na wakadai kuwa hiyo miujiza si lolote ila ni dhaahiri uchawi tu. (Katika Injili ya Luka inasemwa "Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu." Luka 22.43. Na katika Injili ya Yohana 5.30 Yesu anakiri: "Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.")

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Atakaposema Allah Mtukufu, Siku ya Kiyama, «Ewe ‘Ǐsâ mwana wa Maryam! Kumbuka neema yangu kwako, nilipokuumba bila ya baba, na kwa mamako, nilipomteua juu ya wanawake wa ulimwengu na nikamuepusha na hatia aliyobandikwa nayo.» Miongoni mwa neema hizi kwa ‘Ǐsâ ni kwamba Allah Mtukufu Alimpa nguvu na Akamsaidia kwa Jibrili, amani imshukie, akasema na watu na yeye ni mchanga wa kunyonya kabla ya wakati wa kusema na akawaita wao kuja kwa Allah Mtukufu na yeye ni mkubwa, nguvu zake zimeshikana, na ubarobaro wake umekamilika, kwa wahyi wa tawḥîd ambao Allah Mtukufu Alimletea. Na miongoni mwa hizo ni kwamba Allah Mtukufu, Aliyetukuka, Alimfundisha kuandika na (kusoma) maandishi bila ya mwalimu, Alimpa nguvu ya kufahamu na kuelewa, Alimfundisha Taurati Aliyomteremshia Mûsã, amani imshukie, Injili Aliyomteremshia yeye ili kuwaongoza watu. Na miongoni mwa neema hizi ni kwamba yeye anasinyanga kwa udongo kama umbo la ndege na kisha anapuliza kwenye umbo hilo na likawa ni ndege kwa idhini ya Allah Mtukufu. Na miongoni mwazo ni kwamba yeye anamponyesha aliyezaliwa kipofu akawa anaona na anamponyesha mwenye mbalanga ikarudi ngozi yake kuwa na uzima kwa idhini ya Allah Mtukufu. Na miongoni mwazo ni kwamba yeye anamuomba Allah Mtukufu Awahui wafu, na wakainuka kutoka kwenye makaburi yao wakiwa hai. Yote hayo ni kwa matakwa Allah Mtukufu, Aliyetukuka, na idhini Yake. Nayo ni miujiza yenye kushinda, inautilia nguvu unabii wa ‘Ǐsâ, amani imshukie. Kisha Allah Mtukufu, Aliyetukuka na kuwa juu, Anamkumbusha neema Yake kwake alipowazuia Wana wa Isrãîl walipotaka kumuua na akawajia wao na miujiza iliyo wazi yenye kuonyesha dalili za unabii wake. Hapo walisema waliokufuru kati yao, «Hakika haya aliyokuja nayo ‘Ǐsâ, miongoni mwa dalili zilizo wazi, ni uchawi uliofichuka.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net