Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 5 · Aya ya 103

Al-Maaida 5:103

المائدة

مَا جَعَلَ ٱللَّهُ مِنۢ بَحِيرَةٍ وَلَا سَآئِبَةٍ وَلَا وَصِيلَةٍ وَلَا حَامٍ ۙ وَلَـٰكِنَّ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ يَفْتَرُونَ عَلَى ٱللَّهِ ٱلْكَذِبَ ۖ وَأَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ

Maana

Mwenyezi Mungu hakuweka uharamu wowote juu ya "Bahira" wala "Saiba" wala "Wasila" wala "Hami". Lakini wale waliokufuru ndio humzulia uongo Mwenyezi Mungu, na wengi wao hawatumii akili.[1]

[1] Al-Bahira ni ngamia jike ambaye sikio lake hukatwa ikiwa atazaa idadi fulani ya ngamia, na As-Sa’iba ni ngamia jike ambaye anapofika umri fulani huachiwa masanamu yao, na Al-Wasiila ni ngamia jike anayezaa jike baada ya jike mwingine, na Al-Haami ni ngamia dume ambaye watazalishwa idadi fulani ya ngamia kutoka kwa mgongo wake.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Mwenyezi Mungu hakujaalia uharamu wowote juu ya "Bahira" wala "Saiba" wala "Wasila" wala "Hami". Lakini walio kufuru humzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na wengi wao hawatumii akili. [103]

[103] Mwenyezi Mungu hakukupeni ruhusa kuharimisha kitu alicho kuhalalishieni, na kwa hivyo mkenda mkawapasua ngamia masikio yao, na mkajizuia kuwatumia mkawaita "Bahira" mkawawacha kwa kuwekea nadhiri, na mkawaita "Saiba"; na mkaharimisha kula kondoo dume, na mkawatoa kuwa tunza kwa masanamu; na hata kondoo akizaa dume na jike mkamwita "Wasila", na mkakataa kumchinja dume lake. Wala Mwenyezi Mungu hakukufanyieni sharia ya kukuharimishieni msimtumie ngamia dume baada wakisha zalikana kutokana naye matumbo kumi, naye mkamwita "Hami"! Mwenyezi Mungu hakukutungieni sharia yoyote ya namna hiyo. Lakini walio kufuru wanazua uwongo na wanamsingizia Mwenyezi Mungu. Na wengi wao hawatumii akili. Wakati wa Jahiliya, kabla ya Uislamu, Waarabu wakijiharimshia wenyewe asiyo yaharimisha Mwenyezi Mungu. Katika hizo ni kuwa:- 1. Ngamia akizaa mara tano na mtoto wa mwisho akawa dume, basi wakimpasua sikio lake na wakaharimisha kumpanda, na akawa haijuzu kumfukuza kwenye kunywa maji au kula machunga. Na wakimwita: "Bahira", yaani aliyepasuliwa sikio. 2. Ilikuwa mtu husema: Nikirejea safarini, au nikipona maradhi yangu, basi ngamia wangu ni "Saiba", yaani aliye achwa, na anakuwa kama "Bahira". 3. Na walikuwa kondoo akizaa jike humfanya huyo mtoto ni wao, na akizaa dume humfanya ni wa miungu yao; na akizaa dume na jike basi hawamtoi mhanga huyo dume tena kwa miungu yao, na humwita huyo kondoo jike: "Wa'sila", yaani amemuwasilia nduguye dume. 4. Na pia walikuwa akitokana na fahali mizao kumi basi husema mgongo wake umehamika,yaani umehifadhika, na wakamwita "Hami". Huwa basi hapandwi, wala hatwikiwi mizigo.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Allah Mtukufu Hakuwawekea washirikina yale waliyoyazua ya kuacha kunufaika na baadhi ya wanyama wa mifugo na kuwafanya ni wa masanamu. Nao ni baḥîrah: anayekatwa sikio lake akiwa amezaa idadi fulani ya watoto, sãibah: anayeachiwa masanamu, waṣîlah: ambaye amezaa watoto wa kike mfululizo na ḥãmî: ngamia dume iwapo, kutokana na yeye, wamezaliwa idadi fulani ya ngamia. Lakini makafiri waliyanasibisha hayo kwa Allah Mtukufu, Aliyetukuka, kwa kumzulia urongo. Na wengi wa makafiri hawapambanui baina ya haki na batili.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Maaida

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net