Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 48 · Aya ya 29

Al-Fath 48:29

الفتح

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ ٱللَّهِ ۚ وَٱلَّذِينَ مَعَهُۥٓ أَشِدَّآءُ عَلَى ٱلْكُفَّارِ رُحَمَآءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَىٰهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ ٱللَّهِ وَرِضْوَٰنًا ۖ سِيمَاهُمْ فِى وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ ٱلسُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِى ٱلتَّوْرَىٰةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِى ٱلْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْـَٔهُۥ فَـَٔازَرَهُۥ فَٱسْتَغْلَظَ فَٱسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِۦ يُعْجِبُ ٱلزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ ٱلْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ ٱللَّهُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًۢا

Maana

Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na wale walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kutokana na athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea ulio toa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Muhammad ni Mtume wa Allah Mtukufu, na wale walio pamoja naye katika dini yake, ni wakali juu ya makafiri, wanahurumiana wao kwa wao, utawaona wakirukuu na kumsujudia Allah Mtukufu katika Swala yao, wakimtarajia Mola wao Awatunuku fadhila Zake, Awatie Peponi na Awe radhi nao. Alama ya utiifu wao kwa Allah Mtukufu iko wazi kwenye nyuso zao kwa alama ya kusujudu na kuabudu. Hii ndio sifa yao kwenye Taurati. Na sifa yao katika Injili ni kama sifa ya mmea wa nafaka uliotoa kijiti chake na tawi lake, kisha matawi yakawa mengi baada ya hapo, na mmea ukashikana, ukapata nguvu na ukasimama juu ya kigogo chake ukiwa na mandhari mazuri yanayowapendeza wakulima, ili kuwatia hasira kwa Waumini hawa, kwa wingi wao na uzuri wa mandhari yao, makafiri. Katika aya hii pana dalili ya ukafiri wa wenye kuwachukia Maswahaba, radhi za Allah Mtukufu ziwashukie, kwa kuwa yule ambaye Allah Mtukufu amemtia chuki ya kuwachukia Maswahaba basi ishapatikana kwake natija ya chuki hiyo, nayo ni ukafiri. Allah Mtukufu Amewaahidi waumini kusamehewa dhambi zao na kupewa malipo mema, nayo ni Pepo. (Na ahadi ya Allah Mtukufu ni ya ukweli unaoaminiwa usioenda kinyume. Na kila mwenye kufuata nyayo za Maswahaba, radhi za Allah Mtukufu ziwashukie, basi yeye anaingia kwenye hukumu yao ya kustahiki msamaha na malipo makubwa, na wao wana ubora, na kutangulia, na ukamilifu ambao hakuna yoyote katika ummah huu atakayewafikia, radhi za Allah Mtukufu ziwashukie na awaridhie).

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

Al-Fath

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net