Al-Ahqaf 46:15
الأحقافوَوَصَّيْنَا ٱلْإِنسَـٰنَ بِوَٰلِدَيْهِ إِحْسَـٰنًا ۖ حَمَلَتْهُ أُمُّهُۥ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا ۖ وَحَمْلُهُۥ وَفِصَـٰلُهُۥ ثَلَـٰثُونَ شَهْرًا ۚ حَتَّىٰٓ إِذَا بَلَغَ أَشُدَّهُۥ وَبَلَغَ أَرْبَعِينَ سَنَةً قَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِىٓ أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ ٱلَّتِىٓ أَنْعَمْتَ عَلَىَّ وَعَلَىٰ وَٰلِدَىَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَـٰلِحًا تَرْضَىٰهُ وَأَصْلِحْ لِى فِى ذُرِّيَّتِىٓ ۖ إِنِّى تُبْتُ إِلَيْكَ وَإِنِّى مِنَ ٱلْمُسْلِمِينَ
Na tumemuusia mwanadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thelathini. Hata anapofika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: 'Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayoyapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu.'
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu. [15]
[15] Na tumemuusia mwanaadamu kwa wazazi wake awafanyie wema mkubwa. Kwani mama yake amechukua mimba yake kwa mashaka, na akamzaa kwa mashaka. Na muda wa kuchukuliwa mimba mpaka kuachishwa ziwa ni miezi thalathini. Muda wote huo mama kapitikiwa na kila namna ya machungu. Mpaka huyo mtu alipo fikilia ukamilifu wa nguvu zake na akili yake, na akafikia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Nijaalie niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nijaalie nitende vitendo vyema utavyo viridhi Wewe, na ujaalie huo wema wapate pia dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako kwa kila dhambi, na mimi ni miongoni wa Waislamu, yaani walio zisalimisha nafsi zao kwako. Uchache wa mimba ni miezi sita, kwa kauli yake Mtukufu: " Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini." Na kauli yake Mtukufu: "Na kumwachisha ziwa kwake ni miaka miwili", na kauli yake Mtukufu: "Na wazazi wa kike huwanyonyesha wana wao miaka miwili kaamili, kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha." Basi ukitoa muda wa kuachisha ziwa kutokana na muda wa mimba na kunyonyesha inabakia muda wa mimba ni miezi sita. Na haya yanawafikiana na iliyo thibiti kwa ilimu za sayansi kwamba mtoto mchanga akizaliwa baada ya mimba ya miezi 6 anaweza kuishi.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Na tumemuusia binadamu asuhubiane na wazazi wake wawili kwa vizuri, kwa kuwatendea wema wanapokuwa hai na baada ya kufa kwao. Kwa kuwa mama yake alimbeba tumboni kwa mashaka na tabu, na akamzaa kwa mashaka na tabu pia. Na muda wa kubeba mimba mpaka kumaliza kumnyonyesha ni miezi thelathini. Katika kutaja mashaka haya anayoyabeba mama, na siyo baba, pana dalili kuwa haki yake juu ya mtoto wake ni kubwa zaidi kuliko haki ya baba. Mpaka alipofikia binadamu upeo wa nguvu zake za kimwili na kiakili na akafikia miaka arubaini, huwa akimuomba Mola wake kwa kusema, «Mola wangu! Niafikie nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu wawili, na nijaalie nifanye matendo mema unayoridhika nayo, na uwaongoze wanangu. Hakika mimi nimetubia dhambi zangu kwako, na hakika mimi ni miongoni mwa wanyenyekevu kwako kwa utiifu, na ni miongoni mwa wenye kujisalimisha kufuata amri zako na kuepuka makatazo yako, wenye kufuata hukumu yako».
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net