An-Nisaa 4:95
النساءلَّا يَسْتَوِى ٱلْقَـٰعِدُونَ مِنَ ٱلْمُؤْمِنِينَ غَيْرُ أُو۟لِى ٱلضَّرَرِ وَٱلْمُجَـٰهِدُونَ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ بِأَمْوَٰلِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ ۚ فَضَّلَ ٱللَّهُ ٱلْمُجَـٰهِدِينَ بِأَمْوَٰلِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ عَلَى ٱلْقَـٰعِدِينَ دَرَجَةً ۚ وَكُلًّا وَعَدَ ٱللَّهُ ٱلْحُسْنَىٰ ۚ وَفَضَّلَ ٱللَّهُ ٱلْمُجَـٰهِدِينَ عَلَى ٱلْقَـٰعِدِينَ أَجْرًا عَظِيمًا
Hawawi sawa wanaokaa tu miongoni mwa Waumini wasiokuwa na dharura, na wale wanaopigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Mwenyezi Mungu amewaboresha kwa daraja wale wanaopigana kwa mali zao na nafsi zao juu ya wale wanaokaa tu. Na kila mmoja wao Mwenyezi Mungu amemuahidi mazuri mno. Lakini Mwenyezi Mungu amewaboresha kwa ujira mkubwa wale wanaopigana kuliko wale wanaokaa tu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Hawawi sawa Waumini wanao kaa tu wala hawanadharura, na wale wanao pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Mwenyezi Mungu amewatukuza cheo wale wanao pigana kwa mali yao na nafsi zao kuliko wale wanao kaa tu. Ingawa Mwenyezi Mungu amewaahidi wote mashukio mema, lakini Mwenyezi Mungu amewafadhili wanao pigana kwa ujira mkubwa kuliko wanao kaa tu. [95]
[95] Na hakika Jihadi pamoja na kuchukua hadhari inayo takikana ina fadhila kubwa sana. Basi hawawi sawa wanao kaa majumbani mwao wasende kupigana Jihadi na wale Mujaahidiina, wanao pigana kwa mali yao na nafsi zao. Kwani Mwenyezi Mungu amewanyanyua wale Mujaahidiina daraja, cheo cha juu kuwashinda wale wanao kaa nyuma; ila ikiwa wale wanao kaa nyuma wana udhuru unao wazuia kutoka kwenda vitani. Hapo inakuwa udhuru wao unawatoa lawamani, juu ya kuwa wanao pigana wana fadhila na cheo makhsusi. Mwenyezi Mungu amewaahidi makundi yote mawili mashukio mema, na matokeo mazuri.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Wenye kusalia nyuma wakaacha kuhudhuria jihadi katika njia ya Allah Mtukufu, isipokuwa wenye nyudhuru kati yao, hawalingani na wenye kupigana jihadi katika njia ya Allah Mtukufu kwa mali yao na nafsi zao. Allah Mtukufu, Aliyetukuka, Amewafadhilisha wenye kupigana jihadi juu ya wenye kukaa na Ameitukuza daraja yao Peponi kwa kiwango cha juu. Na Allah Mtukufu Amewaahidi wote: wenye kupigana jihadi kwa mali yao na kwa nafsi zao na wenye kukaa, miongoni mwa watu wenye nyudhuru, kwa kutoa kwao na kujitolea katika njia ya haki. Na Allah Mtukufu Amewafadhilisha wale wenye kupigana jihadi juu ya wenye kukaa kwa kuwapa thawabu nyingi.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net