Ruka hadi kwenye maudhui
Sura ya 4 · Aya ya 94

An-Nisaa 4:94

النساء

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوٓا۟ إِذَا ضَرَبْتُمْ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ فَتَبَيَّنُوا۟ وَلَا تَقُولُوا۟ لِمَنْ أَلْقَىٰٓ إِلَيْكُمُ ٱلسَّلَـٰمَ لَسْتَ مُؤْمِنًا تَبْتَغُونَ عَرَضَ ٱلْحَيَوٰةِ ٱلدُّنْيَا فَعِندَ ٱللَّهِ مَغَانِمُ كَثِيرَةٌ ۚ كَذَٰلِكَ كُنتُم مِّن قَبْلُ فَمَنَّ ٱللَّهُ عَلَيْكُمْ فَتَبَيَّنُوٓا۟ ۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا

Maana

Enyi mlioamini! Mnaposafiri katika Njia ya Mwenyezi Mungu, basi chunguzeni sawasawa, wala msimwambie anayewatolea salamu: 'Wewe si Muumini'; kwa kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii, hali ya kuwa kwa Mwenyezi Mungu ndiko zipo ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyokuwa nyinyi zamani, na Mwenyezi Mungu akawaneemesha. Basi chunguzeni sawasawa. Hakika, Mwenyezi Mungu kwa yale mnayoyatenda anazo habari zote.

Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com

Maana

Enyi mlio amini! Mnapo safiri katika Njia ya Mwenyezi Mungu basi hakikisheni, wala msimwambie anaye kutoleeni salamu: Wewe si Muumini; kwa kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii, hali ya kuwa kwa Mwenyezi Mungu zipo ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyo kuwa nyinyi zamani, na Mwenyezi Mungu akakuneemesheni. Basi chunguzeni sawa sawa. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda [94]

[94] Kutahadhari msije mkamuuwa Muumini ni waajibu katika wakati wa kwenda vitani. Mkisafiri kwa ajili ya Jihadi ya Njia ya Mwenyezi Mungu jijuvyeni hakika ya hao mnao pigana nao kabla ya kupambana. Je, hao wamesilimu au bado ni washirikina. Wala msimwambie anaye kutoleeni salamu kuwa ni ishara ya amani: Wewe si Muumini, kwa kuwa mnataka kumnyang'anya mali yake na kondoo wake. Bali ipokeeni salamu yake, kwani kwa Mwenyezi Mungu amekuahidini kupata ngawira nyingi nyenginezo. Na nyinyi, enyi Waumini! Mlikuwa hivyo hivyo katika ukafiri kabla ya hayo, na Mwenyezi Mungu amekuhidini. Basi hakikisheni mambo ya hao mnao wakuta. Na Mwenyezi Mungu anajua baraabara, na hapana chochote kinacho fichikana kwake. Na Yeye hakika ni Mwenye kuhisabu kwa mujibu wa ujuzi wake.

Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com

Maana

Enyi mliomuamini Allah Mtukufu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, mnapotoka kwenye ardhi hali ya kupigana jihadi katika njia ya Allah Mtukufu, kuweni na uangalifu wa mnayoyafanya na mnayoyaacha. Na msimkanushie Imani yoyote ambaye imedhihiri kwake chochote katika alama za Uislamu na akawa hakuwapiga vita nyinyi, sababu pana uwezekano ya kuwa yeye ni Muumini anayeificha Imani yake. Msifanye hivyo kwa kutaka starehe za uhai wa kilimwengu kwani kwa Allah Mtukufu pana nyongeza na vipewa vinavyowatosha. Na nyinyi mlikuwa hivyo mwanzo wa Uislamu, mkiificha Imani yenu kwa jamaa zenu washirikina, kisha Allah Mtukufu Akawaneemesha na Akawatukuza kwa Imani na kwa nguvu Alizowapa. Basi kuweni kwenye ubainifu na ujuzi katika mambo yenu. Allah Mtukufu ni Mjuzi wa matendo yenu yote, ni Mwenye kuyaona mambo yenu ya ndani, na Atawalipa kwayo.

Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com

An-Nisaa

Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net