An-Nisaa 4:90
النساءإِلَّا ٱلَّذِينَ يَصِلُونَ إِلَىٰ قَوْمٍۭ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَـٰقٌ أَوْ جَآءُوكُمْ حَصِرَتْ صُدُورُهُمْ أَن يُقَـٰتِلُوكُمْ أَوْ يُقَـٰتِلُوا۟ قَوْمَهُمْ ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَسَلَّطَهُمْ عَلَيْكُمْ فَلَقَـٰتَلُوكُمْ ۚ فَإِنِ ٱعْتَزَلُوكُمْ فَلَمْ يُقَـٰتِلُوكُمْ وَأَلْقَوْا۟ إِلَيْكُمُ ٱلسَّلَمَ فَمَا جَعَلَ ٱللَّهُ لَكُمْ عَلَيْهِمْ سَبِيلًا
Isipokuwa wale waliofungamana na kaumu ambao kuna ahadi baina yenu na wao, au wanawajia hali ya kuwa vifua vyao vina dhiki juu ya kupigana nanyi, au kupigana na kaumu yao. Na lau angelipenda Mwenyezi Mungu, angeliwapa mamlaka juu yenu na wangelipigana nanyi. Kwa hivyo, wakijitenga nanyi, na wasipigane nanyi, na wakawaletea amani, basi Mwenyezi Mungu hakuwapa nyinyi njia dhidi yao.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Isipokuwa wale walio fungamana na watu ambao mna ahadi baina yenu na wao, au wanakujieni na vifua vyao vina dhiki kupigana nanyi, au kupigana na watu wao. Na lau angeli penda Mwenyezi Mungu angeli wasaliti juu yenu wakapigana nanyi. Basi wakijitenga nanyi, wasipigane nanyi, na wakakuleteeni amani, basi Mwenyezi Mungu hakukupeni njia kupigana nao. [90]
[90] Katika wanaafiki, wanao stahiki kuuliwa kwa fisadi yao kuwafisidi umma wa Waumini, watoe wale ambao wamefungamana na kaumu ambao baina yao na Waumini yapo mapatano ya kuzuia kuuliwa aliye fungamana na upande mmoja wapo. Au vile vile ambao wametatizwa hawajui wapigane pamoja na watu wao, ambao ni maadui wa Waislamu wasio na mkataba nao, au wapigane pamoja na Waumini? Kwani hakika wale wa kwanza inakatazwa kuwauwa kwa ajili ya mkataba, na wengine inakatazwa kuwauwa kwa kuwa hawajui moja wapo la kutenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amependa angeli wajaalia hao wakupigeni vita. Ilivyo kuwa wamekhiari kukaa tu wasikupigeni na wakaingiana nanyi kwa salama na amani, basi haikufaliini nyinyi kuwauwa. Hapana ruhusa kufanya hayo.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Lakini wale wanaofungamana na watu ambao baina yenu na wao pana ahadi na mapatano, msipigane nao. Pia msipigane na wale waliowajia na nyoyo zao zina dhiki, hawataki kupigana na nyinyi na pia hawataki kupigana na watu wao, wakawa hawako na nyinyi wala hawako na watu wao, basi msipigane nao. Na lau Allah Mtukufu angetaka, Angaliwapa nguvu juu yenu wakashirikiana na maadui zenu washirikina katika kupigana na nyinyi. Lakini Allah Mtukufu Aliwaepusha nanyi kwa fadhila Zake na uwezo Wake. Basi wakiwaacha wasipigane na nyinyi na wakawafuata na kujisalimisha kwenu, hamna njia yoyote ya kupigana na wao.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net