An-Nisaa 4:6
النساءوَٱبْتَلُوا۟ ٱلْيَتَـٰمَىٰ حَتَّىٰٓ إِذَا بَلَغُوا۟ ٱلنِّكَاحَ فَإِنْ ءَانَسْتُم مِّنْهُمْ رُشْدًا فَٱدْفَعُوٓا۟ إِلَيْهِمْ أَمْوَٰلَهُمْ ۖ وَلَا تَأْكُلُوهَآ إِسْرَافًا وَبِدَارًا أَن يَكْبَرُوا۟ ۚ وَمَن كَانَ غَنِيًّا فَلْيَسْتَعْفِفْ ۖ وَمَن كَانَ فَقِيرًا فَلْيَأْكُلْ بِٱلْمَعْرُوفِ ۚ فَإِذَا دَفَعْتُمْ إِلَيْهِمْ أَمْوَٰلَهُمْ فَأَشْهِدُوا۟ عَلَيْهِمْ ۚ وَكَفَىٰ بِٱللَّهِ حَسِيبًا
Na wajaribuni mayatima mpaka wanapofikia umri wa kuoa. Mkiona uamuzi wa busara ndani yao, basi wapeni mali zao. Wala msizile kwa kupitiliza na mapema mapema kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na yule ambaye ni tajiri, basi na ajizuilie. Na yule ambaye ni fakiri, basi na ale kwa wema. Na mtakapowapa mali zao, basi washuhudisheni mashahidi juu yao. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu.
Maana: Swahili Translation - Rowad Translation Center. Issued by the Islamic Content Service Association in Languages Toleo 1.0.5, 2025-12-17. QuranEnc.com
Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri basi naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu. [6]
[6] Na kabla ya hao mayatima kufika umri wa kubaalighi wajaribuni, mpate kujua akili zao na hali zao na maarifa yao katika kuendesha mambo. Hata wakifika wakati wa kusilihi kuoa na mkauona uwekevu wao, na matayarisho kuchukua jukumu, basi hapo wapeni mali yao wenyewe. Wala nyinyi msiyale mali yao kwa fujo, mkifanya haraka mpatilize kabla hawajabaalighi wakawa watu wazima ikabidi haki yao kurudi. Na akiwa katika mawasii anajitosha kwa utajiri, basi ajizuie asichukue chochote kuwa ni ujira kutazama mali ya mayatima. Na akiwa fakiri muhitaji basi ajitosheleze kuchukua ujira wa uangalizi kwa kadri ya ada ilivyo. Na mnapo wakabidhi mayatima mali yao wekeni mashahidi wa kushuhudia. Na mjue kuwa Mwenyezi Mungu daima yupo nyuma yenu, na Yeye ndiye Mhasibu, na Yeye ndiye Muangalizi. Na Yeye anatosha kuwa Mhasibu na Muangalizi.
Maana: Swahili Translation - Ali Mohsin Al-Barwani. Translated by Ali Mohsen Al-Barwani Toleo 1.0.1, 2025-06-25. QuranEnc.com
Wajaribuni mayatima walio chini ya mikono yenu mpate kuujua uwezo wao wa kutumia vizuri mali zao. Mpaka watakapofika miaka ya kubaleghe, mkawajua kuwa ni wema katika dini yao na wana uwezo wa kuhifadhi mali zao, basi wapeni mali zao. Wala msizifuje kwa kuzitumia mahali ambapo si pake kwa kupita mpaka wa matumizi na kukimbilia kuzila kabla hawajazichukua kutoka kwenu. Na mwenye mali katika nyinyi, ajizuie na atosheke na utajiri alionao, na asichukue chochote katika mali ya yatima. Na ambaye ni fukara, basi achukue kadiri ya haja yake wakati wa dharura. Na mtakapojua kuwa wao wana uwezo wa kuzihifadhi mali zao baada ya kubaleghe kwao na mkawapa mali zao, wawekeni mashahidi wakiwa ni dhamana kuwa mali yao yamewafikia kikamilifu, ili wasipate kulikanusha hilo. Na yawatosha nyinyi kwamba Allah Mtukufu ni shahidi juu yenu na Atawahesabu kwa mliyoyafanya.
Maana: Swahili Translation - Abdullah Muhammad and Nasser Khamis. Translated by Dr. Abdullah Muhammad Abu Bakr & Shaykh Nasser Khamis Toleo 1.0.1, 2026-03-12. QuranEnc.com
Kiarabu ni maandishi ya Tanzil, bila kubadilishwa. Maana ni matoleo ya wachapishaji wake, bila kubadilishwa; wahakiki wa Sabīl wenyewe bado hawajazikagua. Kiarabu: maandishi ya Uthmani ya Tanzil, toleo la 1.1. Chanzo: tanzil.net